Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameteua wanane kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiwemo wawili waliokatwa majina yao na kamati za uteuzi za Chama cha Mapinduzi (CCM), wakati wa mchakato wa kuwapata wagombea.
Miongoni mwa walioteuliwa ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustapha.
Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari usiku huu wa leo Alhamis Novemba 6, 2025 ikiwa imesainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Zena Said, uteuzi huo unaanza leo.
Wengine walioteuliwa ni Masoud Ali Mohamed ambaye alikuwa mwakilishi wa Ole na Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambaye jina lake lilikatwa katika mchakato wa uteuzi wa ndani ya chama.
Mwingine ambaye alishindwa katika kura za maoni za CCM lakini kateuliwa na Rais ni Nadir Abdulatif ambaye kipindi kilichopita alikuwa mwakilishi wa Kijini na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.
Taarifa hiyo imemtaja pia Tawfiq Salim Turky ambaye alikuwa Mbunge wa Mpendae lakini na yeye jina lake lilikatwa na vikao vya CCM vya uteuzi wakati wa mchakato wa kugombea katika uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka huu.
Aliyeteuliwa mwingine Shariff Ali Shariff ambaye katika kipindi kilichopita pia aliteuliwa kuwa mwakilishi na kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji.
Taarifa hiyo pia imetaja Dk Saada Mkuya ambaye naye katika kipindi kilichoisha alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Fedha na Mipango.
Wengine walioteuliwa ni Said Ali Juma na Dk Juma Malik Akil ambaye alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango.
Kutokana na uteuzi huo, bado nafasi mbili kati ya 10 alizonazo Rais. Nafasi zilizobaki zitatokana na Chama cha ACT Wazalendo ambacho kitapendekeza majina kwa Rais kisha kuwateua.
Hilo ni kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo inataka kufanyika hivyo ili kuleta umoja wa kitaifa kisiwani humo.