Madhara tohara isipofanywa kwa njia salama

Nairobi. Mama mmoja alimpeleka mwanawe wa miaka 11 katika kliniki ya karibu ili atahiriwe.

Kama kinamama wengi, alijua kuwa tohara ilikuwa sehemu ya mpango mkubwa wa taifa wa kupambana na maambukizi ya virusi vya VVU.

Lakini hakuwahi kufikiria kuwa siku hiyo ingeishia kuwa mwanzo wa maumivu kwa mtoto wake.Miezi kadhaa baada ya upasuaji huo, mtoto alianza kuugua.

“Alianza kupata maumivu makali ya sehemu zake za siri, ikafuatwa na maambukizi ambayo hayakutibika kwa dawa za kawaida,” anasema mama huyo.

Hatimaye, aligundulika kuwa na fistula ya uume, hali ambayo mara nyingi huhusishwa na wanawake baada ya kujifungua, lakini sasa inaonekana kuathiri wavulana wadogo, kutokana na tohara zisizotekelezwa kwa viwango vya kitaalamu.

Kwa muda mrefu, tohara ya wanaume imekuwa ikihusishwa na manufaa ya kiafya, ikiwemo kupunguza uwezekano wa maambukizi ya VVU.

Ripoti iliyochapishwa Februari 12, 2021 na mashirika ya kimataifa ikiwemo CDC, WHO, USAID, na wengine, ilifichua kuwa kuwapo kwa wagonjwa 41, wengi wao isipokuwa mmoja wakiwa wavulana wa chini ya miaka 15.

Dk Khisa Wakasiaka, mtaalam wa upasuaji wa fistula ya uume nchini Kenya anasema: “Fistula ya uume ni hali ya kiafya inayotokea pale ambapo tishu au ngozi katika sehemu za siri, hupata maambukizi au upungufu wa damu kiwango cha kuangamiza tishu.

Anasema inaweza kusababisha harufu mbaya, maumivu makali, na hata kuhitaji upasuaji wa haraka ili kuondoa tishu zilizokufa.”
“Kwa kawaida, tunawaona wanawake wanaopata fistula baada ya kujifungua, hasa katika maeneo yenye huduma duni za afya,” anasema.

Lakini sasa, anasema wavulana wadogo nao wanakumbwa na hali hii kutokana na tohara zisizofanywa kwa viwango vya usalama wa kimatibabu.
Uchambuzi wa hivi karibuni ulibaini kuwa wavulana kati ya miaka 10 hadi 11 walikuwa katika hatari zaidi.

Hii ni kwa sababu sehemu zao za siri bado ni changa, ngozi yao ni nyepesi, na miili yao haiwezi kustahimili maumivu au maambukizi kama mtu mzima.

Matukio mengi ya wagonjwa yalitokea katika mazingira ya upasuaji yenye ukosefu wa vifaa vya kisasa, madaktari wasiohitimu vya kutosha, au uhaba wa dawa na huduma za dharura.

Katika baadhi ya matukio, watoto walitahiriwa bila ufuatiliaji wa kutosha, na hivyo maambukizi yakaendelea bila kugunduliwa mapema.

Wataalamu wanakubaliana kuwa kwa kweli tohara kwa wanaume ni muhimu. Tohara ya hiari ni moja ya mikakati iliyopendekezwa na WHO kama njia mojawapo ya kudhibiti maambukizi ya HIV, kwa kuwa inaaminika kupunguza hatari ya maambukizi kwa wanaume.
Lakini pia wataalam wanatoa wito wa kuwepo na marekebisho wa mfumo wa utekelezaji wa tohara. Wanasema kwamba lazima kila upasuaji ufanywe na mtaalamu aliyehitimu, katika mazingira salama, na kwa vifaa vinavyofaa.

Aidha, kuna pendekezo la kuhakikisha wazazi wanapata taarifa sahihi kabla ya kuruhusu watoto wao kutahiriwa, pamoja na huduma ya ufuatiliaji wa afya ya mtoto kwa wiki kadhaa baada ya upasuaji.

Tafiti za kimataifa zinaonyesha kuwa matukio hayo huwatokea zaidi watoto walio chini ya umri wa miaka 15, hasa pale tohara inapofanywa na wahudumu wasiofunzwa au wale wa jadi.

Ripoti moja ilionyesha kuwa asilimia 98 ya wagonjwa wa fstula ya umme ilitokea kwa wavulana chini ya miaka 15, jambo linaloonyesha hatari kubwa kwa kundi hili.

Wataalamu wa afya wanapendekeza kuwepo kwa mfumo madhubuti wa kuripoti madhara ya tohara, kufuatilia wagonjwa na kutoa mafunzo kwa wahudumu wote wa tohara ili kuzuia hali hii.