Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi anatarajiwa kuhutubia na kulizindua Baraza la 11 la Wawakilishi Jumatatu Novemba 10, 2025.
Taarifa iliyotolewa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid leo Ijumaa Novemba 7, 2025 katika kikao cha pili cha Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Wawakilishi amesema Rais atalihutubia Baraza saa 5:00 asubuhi.
“…Tumepokea barua ya Mheshimiwa Rais ya kulihutubia baraza siku ya Jumatatu saa tano asubuhi, tunaombwa wote tuhudhurie kuja kumsikiliza,” amesema Spika Zubeir.
Hatua hiyo ni kutekeleza matakwa ya kifungu cha 84 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo inamtaka Rais kulizindua Baraza la Wawakilishi baada ya uchaguzi mkuu.
Wakati huohuo, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamemchagua Mwanaasha Khamis Juma kuwa Naibu Spika wa Baraza hilo.
Mwanaasha ambaye alikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo akiwa mwakilishi wa Dimani, amechaguliwa leo wakati wa mkutano wa baraza baada ya kupigiwa kura 63 za ndiyo kati ya wajumbe 77 waliohudhuria mkutano huo huku kura 14 zikiharibika.
Akizungumza baada kuapishwa kushika nafasi hiyo Mwanaasha ambaye katika Baraza lililopita alikuwa Mwenyekiti wa baraza, amesema tayari amekuwa na uzoefu wa kuendesha vikao hivyo kwa hiyo imani yake wataendelea kushirikiana na Spika katika kuhakikisha Zanzibar inasonga mbele kwa maendeleo.
Katika Baraza hilo pia wameapishwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanane walioteuliwa na Rais Mwinyi katika nafsi 10 alizopewa kwa mujibu wa katiba.
Miongoni mwa walioteuliwa na kuapishwa leo ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustapha.
Wengine ni Masoud Ali Mohamed ambaye alikuwa mwakilishi wa Ole na Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambaye jina lake lilikatwa katika mchakato wa uteuzi wa ndani ya chama.
Mwingine ambaye alishindwa katika kura za maoni za CCM lakini kateuliwa na Rais ni Nadir Abdulatif ambaye kipindi kilichopita alikuwa mwakilishi wa Chaani na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.
Pia Tawfiq Salim Turky ambaye alikuwa Mbunge wa Mpendae lakini na yeye jina lake lilikatwa na vikao vya CCM vya uteuzi wakati wa mchakato wa kugombea katika uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka huu.
Aliyeteuliwa mwingine Shariff Ali Shariff ambaye katika kipindi kilichopita pia aliteuliwa kuwa mwakilishi na kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji.
Taarifa hiyo pia imetaja Dk Saada Mkuya ambaye naye katika kipindi kilichoisha alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango.
Wengine walioteuliwa ni Said Ali Juma na Dk Juma Malik Akil ambaye alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango.
Kutokana na uteuzi huo, bado nafasi mbili kati ya 10 alizonazo Rais. Nafasi zilizobaki zitatokana na Chama cha ACT Wazalendo ambacho kitapendekeza majina kwa Rais kisha kuwateua.
Hilo ni kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo inataka kufanyika hivyo ili kuleta umoja wa kitaifa kisiwani humo.