-Aongoza mjadala mpana kuhusu ulinzi na namna bora ya uuzaji wa Nishati ya mafuta.
-Atoa pole kwa wakazi wa mkoa huo hususani wadau wa Nishati ya mafuta
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Novemba 07,2025 amekutana na wadau wa Nishati ya Mafuta ya Disel na Petroli katika kikao maalum ambacho kiliratibiwa na EWURA katika ukumbi wa Jengo la PSSSF Sinza Wilayani Ubungo

RC Chalamila katika kikao hicho ameongoza mjadala mpana wa ulinzi na usalama wa vituo vya kuuzia Nishati mafuta kufuatia tukio la hivi karibuni la uhalifu lililofanywa na vikundi vya vijana wasio itakia mema nchi yetu ambapo vituo mbalimbali vya mafuta vilichomwa moto uliopekea hasara kubwa kwa wafanyabiashara hao ambapo kupitia mjadala huo wadau wamepata fursa ya kutoa maoni na ushauri wenye lengo la kuimarisha sekta hiyo kufuatia athari zilizotokea.
Aidha RC Chalamila amewapa pole wadau hao na kuendelea kuwatia moyo kuwa Serikali bado iko bega kwa bega na wafanyabiashara hao kwa kuwa wana mchango mkubwa katika mnyororo wa uchumi wa mtu mmoja mmoja lakini pia Taifa kwa ujumla.

“Ni vema sasa kuratibu vizuri uuzwaji wa mafuta kwenye vidumu, kwa kuwa huwezi kuzuia kabisa kwa kuwa yako maeneo au vyombo vinavyotumia nishati hiyo huitaji mafuta yapelekwe kama vile minara ya simu na boti” Alisema Chalamila
Vilevile RC Chalamila amewataka wadau na jamii kwa ujumla kuendelea kutoa elimu kwa vijana hususani katika makundi yao kama vile pikipiki, na bajaji kutambua umuhimu wa kulinda na kudumisha amani katika Mkoa huo kwa kuwa Dar es Salaam inahudumia nchi nyingi zisizo na bandari pamoja na kuwepo kwa shughuli nyingi za kujipatia kipato na huduma za afya za kibingwa.

Mwisho wadau hao wameishukuru Serikali na kuiomba kuongea na mabenki ambayo walikopa fedha kuwapa muda kidogo wa kuweza kujipanga kurejesha mikopo hiyo, Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe Edward Mpogolo ametoa rai kwa wafanyabiasha hao kuongeza ulinzi lakini pia katika vituo vya mafuta pasiwe na biashara tena zingine ili kujihakikishia usalama zaidi.

