Latra Mbeya yaonya watakaopandisha nauli, wadau watoa mwelekeo

Mbeya. Wakati shughuli zikirejea rasmi jijini Mbeya baada ya vurugu wakati wa uchaguzi, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) imetoa onyo kwa wamiliki na wadau wa usafirishaji kutopandisha nauli, vinginevyo sheria zitachukua mkondo wake.

Hatua hii inakuja baada ya uwapo wa baadhi ya wasafirishaji kupandisha nauli tangu siku moja kabla ya uchaguzi mkuu, Oktoba 29, 2025 ambapo nauli ya kwenda Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya zilionekana kupanda kufikia Sh10,000 badala ya Sh4,000.

Oktoba 29, 2025, Watanzania walitimiza haki yao ya kikatiba kuwachagua viongozi ikiwa ni Rais, wabunge na madiwani ambapo Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), alishinda tena kiti hicho kwa asilimia 98.

Katika uchaguzi huo ilizuka vurugu katika maeneo mengi nchini huku baadhi wakipoteza maisha, wengine kujeruhiwa na kufanya wananchi kujifungia ndani kwa zaidi ya siku tano.

Akizungumza leo Novemba 7, Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka hiyo mkoani Mbeya, Shaban Mdende amesema baada ya shughuli kurejea, hakuna mabadiliko yoyote ya nauli na watakaokaidi, sheria itachukua mkondo wake.

Amesema wanafahamu kipindi kigumu kilichotokea ambapo hakuna Mwananchi aliyefanya uzalishaji, hivyo wamiliki na wadau wote wa usafirishaji mkoani humo, wanapaswa kuzingatia sheria za leseni.

“Tayari tumefuatilia na kuweka matangazo stendi kuu ya mabasi Mbeya kuhusu kutokuwapo mabadiliko ya nauli, tumewasiliana na baadhi ya viongozi na mawakala wa usafirishaji tunatarajia huduma iendelee kutolewa kwa kuzingatia utaratibu uleule.

“Wale watakaokiuka, wakibainika kanuni zipo na masharti yapo kwenye leseni, hivyo anayeenda kinyume sheria zipo wazi, tunaomba tusifike hatua ya kuanza kutoa adhabu,” amesema Mdende na kuongeza:

“Nilipata taarifa kuhusu nauli za Chunya, nilifuatilia kwa wahusika wakanieleza kwamba magari walikuwa wamepaki hivyo ilikuwa ni makubaliano kutokana mazingira yalivyokuwa nikawashauri ikitokea tena tujulishane.”

Mmoja wa abiria katika stendi ya mabasi Chunya, Isack Charles amesema Oktoba 28, 2025 aliamua kutumia Sh10,000 kutokana na huduma hiyo kukosa akieleza kuwa kwa sasa huenda hali imetulia.

“Sijasafiri tena lakini jioni ya kuamkia Oktoba 29, nilitumia Sh10,000 kufika Mbeya kutokea Chunya, niombe mamlaka kulifuatilia kwakuwa hata sisi wananchi hatujafanya kazi,” amesema Charles.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mawakala wa Mabasi na Usafirishaji Stendi Kuu ya Mbeya, Emanuel Wiliam amesema changamoto zilizojitokeza kwa siku za nyuma ilitokana na uhaba wa mafuta, akieleza kuwa kwa sasa hali ni shwari.

Amesema hakuna mabadiliko ya nauli na huduma zinazotolewa zinazingatia sheria, kanuni na taratibu akiwaomba abiria kuendelea na shughuli zao kwa kuwa hali imetulia.

“Malalamiko yaliyojitokeza ilikuwa ni kutokana na usafiri kutokuwapo na uliopatikana huduma ya mafuta haikuwapo kwa maana hiyo, mtu alikuwa anaamua mwenyewe ila kwa sasa ni shwari hakuna mabadiliko ya nauli” amesema Wiliam.

Naye Katibu wa Shirika la Kutetea Haki za Abilia nchini (Shikuha), Hashim Omary amesema tayari wameelekeza viongozi wa shirika hilo katika mikoa yote nchini kupita kwenye stendi kuhakikisha haki inatendeka.

Amesema shirika hilo halitasita kuwaripoti wale wanaokiuka sheria kwa kupandisha nauli au kukatisha safari na kuwafaulisha abilia akieleza kuwa wanachohitaji ni kuona haki inatendeka kwa kuzingatia bei elekezi.

“Kwa siku mbili za tukio la vurugu hali haikuwa nzuri, baadhi ya sheli zilichomwa na nyingine kufungwa na kusababisha adha ya usafiri lakini kwa sasa hali imerejea vizuri hivyo tunatarajia bei elekezi izingatiwe,” amesema Omary.