Taha kuongeza mauzo ya mbogamboga, matunda hadi Sh5 trilioni

Dodoma. Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Maua Tanzania (Taha) kimetangaza mpango wa kuongeza fursa za biashara ya mboga na matunda kutoka mauzo ya Dola za Marekani 600 milioni (Sh1.47 trilioni) hadi kufikia dola 2 bilioni (Sh4.93 trilioni) kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2025 hadi 2035.

Chama hicho kimesema kilimo cha mbogamboga na matunda ni fursa muhimu ya kujiongezea kipato kutokana na uhitaji uliopo ndani na nje ya nchi, hata hivyo kinaeleza kwamba Watanzania wengi hawajaifahamu fursa hiyo na kuitumia.

Mazao yaliyopo kwenye mnyororo wa thamani wa mbogamboga na matunda ni matunda ya aina zote, mboga za aina zote, viungo na vikolezi pamoja na mazao ya asili ya karanga miti na mazao ya mizizi kama vile viazi

Hayo yamebainishwa Novemba 6, 2025 jijini Dodoma na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taha, Jackline Mkindi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa biashara na uwekezaji wa kilimo bustani (HOBIS), unaotarajiwa kufanyika Novemba 12 na 13, 2025 jijini Dar es Salaam.

Mkindi amesema mkutano huo utawaleta pamoja wadau zaidi ya 400 wa ndani na nje ya nchi, Serikali na sekta binafsi.

Katibu mkuu wa Wizara ya kilimo Gerald Mweli (katikati) akizungumza na waandishi wa habari Novemba 6, 2025 Jijini Dodoma. Kulia ni Ofisa Mtendaji mkuu wa TAHA, Jackline Mkindi na kushoto ni Mkurugenzi mkuu wa COPRA, Irene Mlola. Picha na Rachel Chibwete



Amesema kilimo cha mbogamboga na matunda ni sekta inayokua kwa kasi ndani na nje ya nchi na kwa Tanzania inakuwa kwa asilimia tisa.

“Kwa hiyo, ukuaji huo unakuja na fursa nyingi na sisi tumekuwa tukishiriki maonyesho makubwa ya kimataifa ya nje na tumeona kuwa fursa ni nyingi lakini Watanzania wengi hawazifahamu, kwa hiyo kongamano kubwa kama hili litaifungua Tanzania.

“Lakini kwenye eneo la uwekezaji, kutakuwa na kampuni zitakazoongelea masuala ya uwekezaji, hasa kwenye masuala ya fedha kwa sababu Watanzania wengi unapoongelea uwekezaji na fedha wanawaza tu benki, lakini kuna taasisi nyingine za kuwafanya wapate fedha za uwekezaji,” amesema.

Amesema kwenye mkutano huo, pia wataangalia ukuaji wa sekta unavyoendelea,  hasa kwenye eneo la uhifadhi na usafirishaji kwa kuwa mboga na matunda ni mazao yanayoharibika kwa muda mfupi.

Mkindi amesema mkutano huo ni moja ya mikakati ya kuifanya Tanzania kufikia mapato ya dola 2 bilioni kwa kipindi cha miaka 10 (2025-2035) kutoka mapato ya dola 570 hadi 600 milioni kwa sasa kupitia mazao ya mbogamboga na matunda.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesema mambo yanayotarajiwa kujadiliwa kwenye mkutano huo ni pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika miaka minne katika kilimo hasa kwenye sekta ya mbogamboga na matunda na changamoto zilizopo kuanzia kwenye uzalishaji mpaka mezani au sokoni.

“Makatibu wakuu watakuwepo kuwasikiliza wananchi na wadau wa kilimo wa ndani na nje ya nchi kuhusu changamoto na kuzijadili kwa pamoja na kuweka mikakati ya kuzitatua ili kuwawezesha kufanya biashara kwa kuzingatia sheria na kuondoa vikwazo,” amesema Mweli.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola amesema Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wakulima na wafanyabiashara wa sekta ya mboga na matunda ili kuwawezesha kufanya biashara kwa mujibu wa sheria ndani na nje ya nchi.