Kocha Yanga hataki utani! Abadili gia angani

KOCHA mkuu mpya wa Yanga, Pedro Goncalves hataki utani, baada ya kubadili gia angani kwa mastaa wa klabu hiyo kwa kuwafanyia sapraizi akiwaacha njia panda huko kambini Avic Town, inapojifua kujiandaa na mechi ya kesho dhidi ya KMC.

Kama mnakumbuka leo Ijumaa tumewajulisha alivyoshtukia jambo kikosini kuhusu utimamu wa mwili wa wachezaji na kuamua kuwakimbiza ili kuwa fiti na sasa amejilipua kwa kuwaongezea dozi akirudisha ratiba ya kujifua mara mbili kwa siku.

Alichofanya Pedro ameongeza dozi kwa kuwapa wachezaji wake ratiba ya kujifua mara mbili kwa siku kwa ratiba ya asubuhi na jioni, ambayo awali haikuwepo.

Kama haitoshi dozi hiyo imeanza mbele ya Rais wa klabu hiyo, Hersi Said pamoja na mabosi wengine walipofika kuangalia maendeleo ya mazoezi hayo kwa timu hiyo inayoshikilia ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA kwa misimu minne mfululizo.

YANG 01


Kinachofanyika kwa sasa ni kwamba kuna mbio kavu fupifupi kisha mbio za kukimbia na mpira ambazo ndizo zimewatesa mastaa wa timu hiyo iliyofuzu kwa msimu wa minne mfululizo katika michuano ya CAF ikiwa katika Ligi ya Mabingwa.

Kocha huyo amewasisitiza mastaa kwamba ratiba ya mazoezi makali wanayoyafanya hayawezi kuwaathiri kwenye mechi zao za ligi, lakini yatawasaidia wiki mbili zijazo wakati watakapoanza ratiba ya mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha huyo amekuwa akiwagawanya wasaidizi wake kusimamia makundi mawili ya wachezaji, huku mwenyewe akifuatilia kuhakikisha hakuna anayetegea.

YANG 02


Nje ya maandalizi hayo, kocha huyo amekubaliana na mabosi wa klabu hiyo kwamba mara baada ya mechi ya keshokutwa Jumapili ya Ligi Kuu Bara, kikosi kinatakiwa kwenda kuweka kambi ya zaidi ya wiki moja Zanzibar.

Yanga itakaa huko hadi itakapoanza mechi ya kwanza ya makundi ikiwasubiri AS FAR Rabat ya Morocco katika mchi ya kwanza ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.

“Tukimaliza hizi mechi za Ligi hapa tutakwenda Zanzibar, tunafikiria tukajikite huko hadi mechi yetu ya kwanza wa makundi na kocha amekubaliana na ratiba hiyo,” amesema bosi mmoja wa juu wa Yanga kufichua ombi la Pedro, raia wa Ureno.