MSHAMBULIAJI wa Mbeya City, Matheo Antony amesema nyota njema huonekana asubuhi akiamini msimu huu kwake utakuwa wa kurejesha kiwango bora baada ya uliopita kukosa nafasi ya kucheza mechi nyingi za Ligi Kuu Bara.
Matheo aliyewahi kuichezea Yanga, Polisi Tanzania, KMC, Mtibwa Sugar na JKT Tanzania amesema ushindani uliopo katika nafasi anayocheza kama Eliud Ambokile unamfanya aendelee kupambana zaidi ili kupata namba.
“Msimu uliopita sikuanza vizuri, kwani sikucheza mechi nyingi za Ligi Kuu, ingawa bado ni mapema ila naona mwanga wa kutamani kufunga mabao mengi kwa sasa nina mawili,” amesema Matheo na kuongeza:
“Japo nauona ni msimu mgumu, kama mchezaji sina budi kupambana na kujiongeza na mazoezi binafsi ya kuniweka fiti, ili kocha akinipanga niweze kufanya kile anachokihitaji uwanjani.”
Amesema anatamani msimu huu angalau afunge mabao si chini ya 10, hivyo anajiona ana kazi kubwa ya kupambania ndoto yake kuwa halisi, ambapo hadi sasa wakati Mbeya City ikiwa imechezea mechi sita mwenyewe amefunga mabao mawili akiiweka timu kileleni.