MABOSI wa TRA United wanaendelea kusuka mambo kimyakimya ili kuwasapraizi wapinzani wao katika Ligi Kuu Bara msimu huu ikidaiwa wameanza kupiga hesabu ya kuimarisha ukuta wa kikosi hicho kwa kusaka mabeki.
Mmoja wa mabeki wanaotajwa kuingia kwenye rada za timu hiyo ni beki wa zamani wa Yanga na FC Lupopo ya DR Congo, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na kama mambo yakienda vizuri atatua kikosini.
Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kuwa TRA United inahitaji huduma ya beki huyo aliyepo kwa sasa Transit Camp ya Ligi ya Championship.
Ninja hajaanza kucheza kwani alikuwa anasubiri kibali cha uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka FC Lupopo aliyoichezea 2023/24, kisha akavunja mkataba na kurejea Tanzania ishu ikitajwa kuwa ni suala la maslahi.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya TRA United kilisema huduma ya Ninja ilianzia kusakwa wakati wa usajili wa dirisha kubwa lililopita na uongozi umeamua kurejea tena kwake.
“Ni beki mzuri na ana uzoefu mkubwa kutokana na timu alizocheza. Endapo tukifanikiwa kuipata saini yake ataongeza nguvu katika kikosi chetu,” kilisema chanzo hicho.
“Ingawa bado ni mapema, lakini tunataka kutumia dirisha dogo kuboresha kikosi kwa sababu malengo yetu tunatamani kumaliza nafasi tatu za juu katika msimamo wa ligi.” Msimu uliopita ikitumia jina la Tabora United kabla ya kubadilisha jina, TRA ilimaliza nafasi ya tano. Ninja mwenyewe alipotafutwa juu ya taarifa hiyo, alijibu kwa kifupi: “Mimi ni mwajiriwa wa Transit Camp, hivyo siwezi kuzungumzia hilo.”