SIMBA iliyo chini ya Meneja Dimitar Pantev inatarajiwa kushuka uwanjani usiku wa leo Jumamosi kukabiliana na JKT Tanzania, lakini mabosi wa klabu hiyo wameanza mapema hesabu za usajili wa dirisha dogo zikisalia siku 39 kabla dirisha kufunguliwa.
Katika harakati hizo za kuligeukia dirisha dogo, kuna kiungo mmoja fundi ambaye hajaitumikia timu hiyo katika mechi yoyoye ya mashindano kutokana na kuwa majeruhi, aliyewekwa mtu kati akipigiwa hesabu kutolewa kwa mkopo ili kuspisha mashine mpya.
Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa kuwa, tayari Pantev amewasilisha ripoti ya awali iliyoifanya Simba iingie sokoni mapema kusaka makipa wawili wapya akiwemo mmoja wa kigeni kufuatia kuumia Moussa Camara, pia akitafutwa kiungo mshambuliaji mbunifu.
Panga la kuruhusu nyota wapya limetajwa kuanzia kwa kiungo mshambuliaji Mkenya, Mohammed Bajaber aliyekuwa akisumbuliwa na majeraha tangu ajiunge na timu hiyo.
Chanzo kutoka ndani ya Simba kimeeleza kuwa maamuzi yaliyopo kwa sasa ni kumtoa kwa mkopo mchezaji huyo mwenye mkataba wa miaka mitatu na tayari mazungumzo baina ya pande hizo mbili yameanza.
“Bajaber ni mchezaji mwenye kipaji lakini bahati mbaya amekuwa akipata majeraha ya mara kwa mara. Tumejaribu kumpa muda arudi kwenye ubora, lakini bado hajafikia kiwango cha ushindani,” kilisema chanzo hicho.
Simba imekuwa ikitafuta njia bora ya kuhakikisha mchezaji huyo mwenye uwezo wa kucheza winga ya kushoto, kulia na hata namba 10, anapata muda wa kucheza zaidi na mpango wa mkopo unaonekana kuwa suluhisho.
Taarifa zinadai kuwa klabu hiyo imepanga kumpeleka kwa maafande wa JKT Tanzania ikiwa ni pendekezo la Pantev ili aendelee kusalia hapa hapa nchini na apate muda mzuri wa kufuatilia maendeleo yake.
Hata hivyo, mchezaji mwenyewe hajaonyesha utayari wa kuondoka, akiamini bado ana nafasi ya kupigania namba ndani ya kikosi cha Simba.
“Bajaber hajakata tamaa. Anaamini anaweza kurejea na kuonyesha thamani yake akiwa ndani ya Simba. Anataka kuendelea kupigania nafasi yake,” kilisema chanzo cha karibu na mchezaji huyo.
Kwa upande mwingine, viongozi wa Simba wanasema uamuzi huo ni sehemu ya mpango mpana wa kupunguza idadi ya wachezaji waliokuwa nje kwa muda mrefu bila mchango wa moja kwa moja kwenye kikosi.
Wakati Simba ikijipanga kumtoa kwa mkopo, klabu mbalimbali zimeanza kuonyesha nia ya kumhitaji kiungo huyo, miongoni mwazo ni pamoja na waajiri wake zamani, Polisi Kenya.
Kwa upande mwingine, TRA United inayoongozwa na kocha Etienne Ndayiragije ambaye aliwahi kufanya kazi na Bajaber wakati huo wakiwa Polisi nayo inatajwa kuvutiwa na mchezaji huyo ambaye kabla ya kutua Simba aliisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi nchini Kenya huku akifunga mabao sita na asisti nne.
Kwa sasa Simba inaendelea na tathmini ya mapendekezo yote, lakini msimamo wa awali ni kuachana na wachezaji wawili wa kigeni, mmoja ikiwa ni Camara ambaye ni majeruhi huku Bajaber ikiwa ni kwa mkopo wa nusu msimu ili kutoa nafasi kwa maingizo mengine mpya. Wakati mpango huo ukiendelea, benchi la ufundi la Simba tayari limeanza kusaka kiungo mshambuliaji atakayejaza nafasi ya Bajaber.