Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) leo Novemba 7, 2025, imetangaza orodha ya Wabunge Wanawake wa Viti Maalumu 115 walioteuliwa kushiriki katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uteuzi huo umefanywa kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 66(1)(b) na 78(1) za Katiba ya mwaka 1977, pamoja na kifungu cha 112 cha Sheria ya Uchaguzi wa mwaka 2024.
Miongoni mwa walioteuliwa ni Cecilia Daniel Paresso na Bonnah Ladislaus Kamoli wote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo Bonnah awali alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea. Wengine ni Devotha Minja na Sigrada Mligo kutoka Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), waliopata nafasi hizo kupitia orodha ya viti maalumu.
Kwa mujibu wa taarifa ya INEC, idadi kamili ya wabunge wa viti maalumu inapaswa kuwa 116, ambapo uteuzi wa nafasi moja bado unasubiri kukamilika kwa uchaguzi wa ubunge katika majimbo ya Fuoni (Zanzibar) na Siha (Tanzania Bara).
Tume imesema uteuzi huo umezingatia uwiano wa kura zilizopatikana na vyama vya siasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, sambamba na masharti ya kikatiba yanayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi wa kisiasa.
INEC imewapongeza wote walioteuliwa na kuwataka kutumia nafasi hizo kwa uadilifu, uwajibikaji na kujenga umoja wa kitaifa kupitia mchango wao ndani ya Bunge.

Related
