Dar es Salaam. Mfanyabiashara Jenifer Jovin (26), maarufu Niffer na wenzake 239 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na kesi ya uhaini inayotokana na maandamano ya kupinga uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Niffer, aliyekamatwa mapema kabla ya siku ya kupiga kura na wenzake hao waliokamatwa siku ya kupiga kura Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, wamepandishwa kizimbani mahakamani hapo leo Ijumaa, Oktoba 7, 2025.
Washtakiwa hao ambao walifikishwa mahakamani hapo saa 5:54 asubuhi wakiwa ndani ya mabasi matatu ya Jeshi la Magereza, baadhi yao walikuwa wakitembea kwa kuchechemea ikidaiwa ni kutokana na majeraha ya kipigo na mengine ya risasi, huku wengine wakidaiwa kuwa bado wanatembea na risasi mwilini.
Miongoni mwao wamo waendesha bodaboda, wanafunzi, wajasiriamali, kama vile utingo, kondakta wa daladala, fundi ujenzi, wakala wa huduma za pesa kwa njia ya simu, muongoza sherehe (MC), fundi makenika na wapambaji kumbi za sherehe.
Pia wamo watu wenye fani mbalimbali kama mwanahabari, Simon Makaranga (26), mkazi wa Mbagala; walimu, Lucianus Luchius (28) Mkazi wa Mbweni na John Mawakili (30) mkazi wa Temboni; mhasibu, Paulo Malima (28), Mkazi wa Changanyikeni na mtaalamu wa maabara, Benadetha Laizer (26).
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka ya kula njama na ya uhaini katika makundi matano tofauti na mbele ya mahakimu watatu tofauti.
Hata hivyo, katika kesi hizo zote mahakimu wote wamewaeleza washtakiwa kuwa hawatakiwi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hizo, bali zitasikilizwa na Mahakama Kuu baada ya upelelezi kukamilika.
Pia mahakimu wamewaeleza washtakiwa kwa kuwa wanakabiliwa na shtaka la uhaini ambalo halina dhamana wataendelea kukaa mahabusu mpaka upelelezi wa kesi zao utakapokamilika.
Katika kesi zote, upande wa mashtaka umeieleza mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Kundi la kwanza lililomhusisha Niffer, lilikuwa na jumla ya washtakiwa 22 akiwemo yeye.
Katika kesi hiyo uchunguzi wa awali (PI) namba 26388 ya mwaka 2025, Niffer na wenzake wamesomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.
Katika kesi hiyo yenye mashtaka matatu, Niffer anakabiliwa na mashtaka mawali, moja la kula njama kutenda kosa la uhaini linalomhusisha yeye na wenzake 21 na lingine la uhaini linalomhusu yeye peke yake.
Wenzake 21 kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka la uhaini linalowahusu wao pekee (bila Niffer).
Katika shtaka la kwanza, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato amedai washtakiwa wote (Niffer na wenzake) kwa nyakati tofauti kati ya Aprili mosi na Oktoba 29, 2025 walikula njama za kutenda kosa la uhaini.
Katika shtaka la pili, amedai washtakiwa 21 wenzake na Niffer, Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali wilayani Ubungo, Dar es Salaam wakiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitengeza nia ya kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kato amedai walitengeneza nia hiyo kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuithibitisha nia hiyo kwa kusababisha hasara kwa mali za Sarikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.
Kesi ya pili ya uchunguzi wa awali (PI) namba 26395 ya mwaka 2025 iliwajumuisha washtakiwa 75, Paulina Palangyo (28) mfanyabiashara, Mkazi wa Mbezi na wenake 74.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube, ya kula njama na uhaini yanayowahusu washtakiwa wote.
Katika mashtaka hayo, Wakili Kato amedai washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Aprili mosi na Oktoba 29, 2025.
Mawakili wanaowatetea washtakiwa wamewasilisha hoja mahakamani hapo wakidai wateja wao waliteswa wakati wakiwa chini ya Jeshi la Polisi.
Jopo la mawakili hao, Peter Kibataka, Dickson Matata na Paul Kisabo waliwasilisha hoja hizo mbele ya mahakama.
Katika kesi ya Niffer na wenzake, Kibatala alidai Novemba 6, 2025 Niffer akiwa chini ya Jeshi la Polisi Kituo cha Polisi Oysterbay alifanyiwa vitendo vya ukatili kwa kupigwa na maofisa wa jeshi hilo na kulazimishwa asaini maelezo yake.
“Pia Novemba 5, 2025 washtakiwa 21, nao walipigwa na Jeshi la Polisi na mheshiwa hakimu kuna washtakiwa hapa wana majeraha na vidonda mwilini, hivyo tunaomba taarifa hii iingie katika kumbukumbu za mwenendo wa kesi hii,” alidai Kibatala.
Alidai kutokana na washtakiwa hao kudaiwa kupigwa na polisi, anaiomba mahakama itoe amri watakapokabidhiwa kwa Jeshi la Magereza wapatiwe matibabu ya kitabibu na ripoti yake ipelekwe mahakamani hapo, ili iwe sehemu katika maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Kibatala amedai shtaka la kula njama lina upungufu kisheria kwa sababu linamezwa na shtaka la uhaini, hivyo ameomba liondolewe.
Baada ya kuwasilisha hoja hizo, upande wa Jamhuri umeomba muda ili kuzijibu.
Hakimu Lyamuya ameelekeza washtakiwa wapelekwe hospitali zilizopo ndani ya Magareza na ripoti za matibabu ziwasilishwe mahakamani hapo.
Kuhusu kuondoa shtaka la kula njama, hakimu Lyamuya na Hakimu Beda kwa nyakati tofauti wamesema mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Hakimu Lyamuya ameelekeza washtakiwa wote warudishwe rumande ya magereza hadi Novemba 11, 2025, siku ambayo Jamhuri itajibu hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi.
Kesi ya tatu iliwahusu washtakiwa John Alexander John na wenzake 12, ambao wamesomewa mashtaka ya kula njama kutenda kosa la uhaini na uhaini, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
Mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Fadhili John katika kosa la kwanza amedai washtakiwa walilitenda kati ya Machi na Oktoba 29, 2025. Kwenye shtaka la pili, wakati na maelezo ya shtaka yanafanana na mengine.
“Kesi hii itatajwa Novemba 20, 2025 kuangalia kama upelelezi umekilika,” amesema Nyaki.
Katika kesi ya nne ambayo pia washtakiwa wamesomewa mashtaka mawili ya kula njama na uhaini mbele ya Nyaki inawahusu washtakiwa 28, waliosomewa mashtaka na Wakili John.
Wakili wa washtakiwa, Dickson Matata, ameieleza mahakama kuwa wateja wake walikamatwa na Jeshi la Polisi na wana zaidi ya siku tano.
Amedai wote wanasema walipokamatwa walipigwa na kuteswa na wote wanadai maelezo kama yapo waliyoandika au waliyoyasaini walilazimishwa.
Pia amedai wakati wote hawakupewa haki ya kuonana na ndugu au wakili na kwamba, muda wote ambao wamekuwa chini ya Polisi hawajapewa huduma za kibinadamu, ikiwamo muhimu ya matibabu.
Amemsimamisha mshtakiwa mmoja (Baraka), akasema alipigwa risasi mguuni na mpaka sasa imo ndani haijatolewa hali inayosababisha mguu wake kuoza.
“Siyo huyo tu, bali na wengine lakini nimemtolea huyo kama mfano. Kutokana na hali hiyo tuna ombi mahakama yako itoe amri watakaporudishwa mahabusu wapelekwe hospitali za Magereza na ikibidi wapewe rufaa kulingana na majeraha yao,” amesema.
Ameomba taarifa ya matibabu ya kila mmoja iwasilishwe mahakamani kuwa sehemu ya kumbukumbu za kesi hiyo.
Wakili Matata amepinga hati ya mashtaka akidai ina kasoro za kisheria kwa kuchanganya mashtaka mawili tofauti ambayo hayapaswi kuchanganywa.
Vilevile, ameomba mahakama iuelekeze upande wa mashtaka ueleze ni lini utakamilisha upelelezi.
Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Magreth Bernard, amesema hoja kama washtakiwa walipigwa na kulazimishwa kuandika au kusaini maelezo ni suala la kiushahidi, ambalo litawasilishwa wakati wa usikilizwaji.
Kuhusu matibabu kwa washtakiwa, amesema hawawezi kulipinga lakini Jeshi la Magereza lina utaratibu wake wa kuwapatia tiba mahabusu na wafungwa.
Akizungumzia upelelezi kuchelewa, amesema kwa mujibu wa Sheria ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka hakuna ukomo wa upelelezi kwa makosa makubwa.
Hata hivyo, amesema si nia ya ofisi hiyo kuchelewesha upelelezi wa kesi ya mshtakiwa yeyote, huku akiahidi kuhakikisha unakamilika haraka.
Akitoa uamuzi hakimu Nyaki amesema mahakama hiyo haina mamlaka kuzungumzia suala la hati ya mashtaka.
Kuhusu matibabu ameelekeza gereza ambako washtakiwa watapelekwa wapatiwe matibabu na baada ya hapo ripoti ya Mkuu wa Gereza kuhusu matibabu yaliyotolewa iwasilishwe mahakamani.
Akizungumzia upelelezi, amesema upande wa mashtaka una wajibu wa kuhakikisha unakamilika kwa wakati.
Katika kesi ya tano washtakiwa 95 wamesomewa mashtaka mawili ya kula njama kutenda kosa la uhaini na la uhaini yenye maelezo yaleyale kama mashtaka ya kesi nyingine, ambao wamesomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Hassan Makube. Kesi hiyo itatajwa Novemba 19, 2025.