Mbeya. Wakati msimu wa kilimo ukianza, wakulima 3,200 wa Nyanda za Juu Kusini wanatarajia kupatiwa mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kulima na kuzalisha kwa tija yatakayotolewa na Malaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) katika kanda hiyo.
Mbali na wakulima hao, wafanyabiashara wa mbolea 640 nao watakuwa sehemu ya wanufaika wa mafunzo hayo yanayolenga kuelimisha matumizi sahihi ya mbolea na kuongeza uzalishaji kwenye mazao.
Akizungumza leo Novemba 7, 2025, Meneja wa TFRA Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’ondya, amesema mafunzo hayo yanatarajia kuanza Novemba 10 wakianzia mkoani Songwe, Njombe, Katavi na Rukwa Novemba 27 hadi 28.
Amesema mkakati wa Wizara ya Kilimo ni kuhakikisha watoa huduma za pembejeo, wanapata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, kutambua sheria na kutoa ushauri ili kuweza kutoa huduma bora kwa wakulima walio pembezoni mwa miji.
Amesema mafunzo hayo yatahusisha pia vyama vya wakulima kila Mkoa, akieleza kuwa matarajio yao ni kuona mkulima anafaidika na kilimo chake na kuongeza thamani kwenye mazao hali inayoweza kuongeza bei sokoni.
Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti Mbolea (TFRA), Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ngyondya akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Novemba 7, 2025 ofisini kwake jijini Mbeya.
“Mbali na mafunzo ya nadharia, tutafika pia mashambani kuwatembelea wakulima kwakuwa kila Mkoa mafunzo yatakuwa siku mbili, lengo ni kuhakikisha wakulima wanafaidika na kilimo chao”
“Tuna uhakika msimu huu wa kilimo mbolea ikitumika kwa usahihi, uzalishaji utaongezeka na thamani na bei ya mazao itakuwapo, mkakati wa mamlaka ni kuona tunafikia malengo hayo” amesema Meneja huyo.
Amengeza kuwa mafunzi hayo ni sehemu ya mwendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya ‘mali shambani silaha mbolea’, na kwamba elimu hiyo itaelekeza kutumia mbegu bora, visumbufu mimea na ushauri wa utunzaji shamba.
“Tunatarajia huduma bora kuongezeka, uzalishaji bora na wenye tija unaoendana na mabadiliko ya teknolojia na tutaondokana na kilio cha bei ya mazao kwa wakulima” amesema Ng’ondya.
Kwa upande wake mmoja wa wafanyabiashara wa mbolea katika mji wa Makambako, Olaf Stanley amesema mafunzo hayo ni muhimu kwani yanaenda kusaidia kuibua wafanyabaishara wapya na kuinua uchumi.
“Tuishukuru na kuipongeza TFRA Nyanda za Juu Kusini kuwekeza zaidi kwa wadau wa kilimo, mafunzo haya yataongeza uelewa katika matumizi sahihi ya mbolea hatimaye kuongeza uzalishaji wenye tija na kuinua uchumi wa Taifa,” amesema Stanley.
Naye mkulima wa zao la kahawa, Ephraim Wiliam amesema wako tayari kushiriki mafunzo hayo wakitarajia kujifunza teknolojia na mbinu za kukabiliana na visumbufu mimea.
“TFRA Nyanda za Juu Kusini, wamekuwa sehemu ya faraja sana kwa wakulima haswa kipindi cha msimu wa kilimo, tuko tayari kwa mafunzo hayo na kutoa ushirikiano,” amesema Wiliam.