Dar es Salaam. Rais wa China, Xi Jinping amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushinda na kuapishwa kuiongoza Tanzania, akiahidi ushirikiano zaidi miongoni mwa mataifa hayo mawili.
Mbali na salamu za Jinping, pia Rais Samia alipokea ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin uliowasilishwa kwake na Sergei Kiriyenko, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, juzi akimpongeza kwa hatua hiyo.
Samia ametangazwa kushinda urais, Novemba 1, mwaka huu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na kuapishwa Novemba 3, mwaka huu.
Katika uchaguzi huo, Rais Samia ameshinda kwa kupata kura 31,913,866 sawa na asilimia 97.66, akiwashinda wagombea wenzake 16 wa nafasi hiyo.
Rais huyo wa China, ametoa pongezi hizo juzi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani twitter).
Katika ujumbe huo ameandika, “natuma salamu maalumu za pongezi kwa Samia Suluhu Hassan kufuatia kuanza kwako rasmi majukumu ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naahidi kukupa ushirikiano kati ya China na Tanzania.”
Katika salamu hizo, Rais Xi Jinping alisema anathamini uhusiano wa muda mrefu kati ya China na Tanzania, akibainisha kuwa yuko tayari kufanya kazi kwa karibu na Rais Samia katika kuimarisha na kuongeza wigo wa maeneo ya ushirikiano kwa manufaa ya mataifa hayo.
“Nathamini ukuaji wa mahusiano kati ya China na Tanzania, na niko tayari kushirikiana na Rais Samia kutekeleza matokeo ya Mkutano wa Ushirikiano wa China na Afrika (Focac) uliofanyika Beijing, kukuza ushirikiano wetu wa kimkakati na wa kina katika ngazi za juu zaidi na kuchangia ujenzi wa ushirika imara wa China na Afrika wenye mustakabali wa pamoja katika enzi mpya,” ameeleza.
China na Tanzania zimekuwa washirika wa karibu kwa miongo kadhaa, uhusiano ambao umeanzia kwenye miradi mikubwa ya kihistoria kama reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), hadi maeneo ya sasa ya uchumi, miundombinu, elimu, afya na uwekezaji.
Katika miaka ya karibuni, miradi inayofadhiliwa au kuungwa mkono na China nchini Tanzania ikiwemo ya ujenzi na ya nishati, imeendelea kuongeza kasi ya maendeleo ya ndani na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kauli ya Rais Xi inatarajiwa kuakisi msimamo wa kuendeleza ushirikiano huo kupitia mpango wa Focac unaolenga kuongeza uwekezaji, biashara, ustawi wa watu na kukuza hadhi ya Afrika katika ramani ya kiuchumi duniani.
Uhusiano wa Tanzania na Urusi
Ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi una historia ndefu inayorudi hadi enzi za Vita Baridi, wakati Umoja wa Kisovieti (USSR) ulikuwa mshirika muhimu wa mataifa mengi ya Kiafrika, ikiwemo Tanzania ambayo wakati huo ilikuwa Tanganyika, na baadaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika miaka ya 1960 na 1970, Umoja wa Kisovieti ulikuwa miongoni mwa washirika wakuu wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Afrika na katika kujenga taasisi za taifa jipya.
Kupitia uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania ilipokea msaada mkubwa wa kisiasa na kiuchumi.
Pia, katika sekta ya elimu ilibaki kuwa mhimili muhimu wa ushirikiano huo ambapo maelfu ya Watanzania walipata ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu vya Kisovieti, wakibobea katika taaluma kama uhandisi, tiba, kilimo, na sayansi.
Uwekezaji huu katika elimu uliimarisha sana rasilimali watu ya Tanzania katika kipindi cha mwanzo cha kujitegemea.
Hata baada ya kuvunjika kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991, uhusiano huo uliendelea chini ya Urusi kwa nchi hizi mbili kuendelea kushirikiana katika nyanja za biashara, elimu, diplomasia na utalii.