Mwanza. Jumla ya watuhumiwa 172 wamesomewa mashitaka mbalimbali yakiwemo ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kuharibu mali kwa makusudi, kufanya maandamano bila kibali na fujo, katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Watuhumiwa hao wamesomewa mashtaka hayo leo Ijumaa Novemba 7, 2025 kwa nyakati tofauti mbele ya mahakimu mbalimbali, washitakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Oktoba 29 na 30, 2025 katika maeneo mbalimbali wilayani Nyamagana Mkoa wa Mwanza.
Upande wa Jamhuri umewakilishwa na wakili Jaines Kihwelo akisaidiwa na Hellen Mabula na Sara Perias, huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na mawakili kutoka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Chemba ya Mwanza wakiongozwa na Erick Mutta, Lugano Kitanga, Emmanuel John na Salehe Nassoro.
Ambapo, watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo kusomewa hati ya mashtaka yanayowakabili kuanzia saa 8 mchana hadi saa 11 jioni na kurudishwa rumande kutokana na shitaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha kutokuwa na dhamana.
Baadhi ya washtakiwa wakiwa nje ya Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza leo Novemba 7, 2025 kwa ajili ya kusomewa mashtaka yanayowakabili. Picha na Damian Masyenene
Katika shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu 287 A cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023, huku shitaka la kuharibu mali kwa makusudi wakishtakiwa kwa mujibu wa kifungu cha 326 (1) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.
Akiwasomea mashitaka watuhumiwa 86 wanaokabiliwa na mashitaka mawili ya uharibifu wa mali na unyang’anyi kwa kutumia silaha mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Amani Sumari, Wakili wa Serikali, Jaines Kihwelo amesema Oktoba 30, 2025 katika eneo la Isamilo wilayani Nyamagana watuhumiwa wote kwa makusudi waliharibu jengo la Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Amesema baada ya hapo washitakiwa hao waliiba viti 13 vya plastiki mali ya Halmshauri ya Jiji la Mwanza na kumtishia mlinzi kwa panga na mawe ili waweze kujipatia mali hizo.
Wakili Kihwelo amesema upelelezi wa mashitaka hayo haujakamilika hivyo akaomba tarehe nyingine ili shauri hilo litajwe, huku wakili wa upande wa utetezi, Erick Mutta akiomba mahakama kuitaka Jamhuri iharakishe upepelezi ili shtaka litakapotajwa liende hatua inayofuata.
Hata hivyo, Hakimu Sumari amelihairisha shitaka hilo hadi Novemba 19, 2025 litakapotajwa tena, huku washitakiwa wakirudishwa rumande.
Katika shauri lingine linalowakabili washitakiwa 36 kwa makosa mawili ya kuharibu mali kwa makusudi kinyume na kifungu cha 326 (1) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023, na unyang’anyaji wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287 A cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Jaines Kihwelo amesema mnamo Okotba 30, 2025 katika eneo la Mabatini wilayani Nyamagana, Mwanza washitakiwa kwa pamoja na watu wengine ambao hawajapatikana kwa makusudi na kinyume cha sheria waliharibu kwa makusudi kwa kuchoma moto kituo cha polisi Mabatini ambacho ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema katika shitaka la pili, tarehe tajwa katika eneo la mabatini washitakiwa kwa pamoja na watu wengine ambao hawajapatikana waliiba radio call na sare za jeshi la polisi kisha walimtishia askari aliyekuwa zamu, Edward Magembe kwa kutumia panga na vipande vya nondo ili waweze kuondoka na vitu hivyo.
Hata hivyo, Wakili Kihwelo amesema upelelezi wa mashitaka hayo haujakamilika hivyo akaomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo, huku Wakili wa utetezi, Erick Mutta akiiomba mahakama kuitaka Jamhuri iharakishe upelelezi ili shauri litakapotajwa tena liende hatua inayofuata.
Baadhi ya washtakiwa wakiwa nje ya Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza leo Novemba 7, 2025 kwa ajili ya kusomewa mashtaka yanayowakabili. Picha na Damian Masyenene
Baada ya kusikiliza zote mbili, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Amani Sumari amehairisha kesi hiyo hadi Novemba 21, 2025 litakapotajwa tena, huku washitakiwa wote 36 wakirudishwa rumande.
Katika shauri linguine, washtakiwa 11 wamefikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka mawili ya kufanya maandamano bila kibali na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Vilevile, washitakiwa wengine sita wamesomewa mashtaka mawili ya kufanya fujo kinyume na kifungu cha 74 (1) (2), 76, na 35 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023, na uyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287 A cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.
Aidha, washitakiwa wengine 11 wamesomewa mashitaka mawili ya kuchoma vitu kinyume na kifungu cha 319 (a) (b) cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023, ambapo walitenda kosa hilo mnamo Oktoba 30, 2025 katika eneo la Igoma kwa kuchoma kituo cha mafuta cha Lake Oil.
Pia, wanakabiliwa na shtaka la unyanganyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287 A cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023. Huku washtakiwa wengine sita nao wakikabiliwa na kosa la kufanya maandamano kinyume na kifungu cha 74 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.
Washitakiwa wote wamerejeshwa rumande kutokana na shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha kutokuwa na dhamana.
Akizungumzia mashitaka hayo, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) chapta ya Mwanza, Erick Mutta amesema wameamua kufika mahakamani hapo kutoa msaada wa kisheria kwa washtakiwa hao ikiwa ni sehemu ya msaada unaotolewa na chama hicho mkoani humo.
Amesema washitakiwa hao ambao wamegawanywa katika makundi mbalimbali hadi saa 11 jioni Novemba 7, 2025 jumla ya washhtakiwa 172 wamepandishwa kizimbani mbele ya mahakimu mbalimbali wakishtakiwa kutokana na matukio ya vurugu na maandamano yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu KATI YA Okotba 29 hadi 31, mwaka huu.
“Kwa ujumla washitakiwa waliopandishwa kizimbazi ni 172 na mashtaka yanayowakabili kwa mahakimu tofauti ni kuchoma moto, kuharibu mali kwa mkusudi, unyang’anyi wa kutumia silaha na kufanya fujo,” amesema Mutta.
Ameongeza; “Bahati mbaya katika makundi yote haya hakuna kundi hata moja lina mshtakiwa yeyote ambaye amepata dhamana kwa sababu pia kuna makosa ambayo hayana dhamana hasa la unyang’anyi kwa kutumia silaha.”