Saa 24 za moto Ligi Kuu

MASHABIKI wa soka nchini, wanatarajiwa kuendelea kupata uhondo wa Ligi Kuu Bara inayorejea baada ya kusimama kwa muda, huku kukiwa na vita nzito ya saa 24 kwa vigogo waliopo CAF.

Ndio wikiendi hii ni ya moto kwa klabu tano kati ya nane zitakazorejea uwanjani kuanzia leo Jumamosi hadi kesho Jumapili, ambapo kila moja ikitumia vyema dakika 90 ina uhakika wa kukaa kileleni angalau kwa muda wa saa 24 au vinginevyo.

Uhondo huo wa wikiendi Ligi Kuu Bara unaenda sambamba na burudani nyingine za Ligi Kuu Tano Bora za Ulaya ambazo nazo zinaendelea kama kawaida, kwani pale England ‘Kwa Babu’ kuna kitupe cha Tottenham dhidi ya Man United ya moto.

Pia kule Italia kuna Dabi ya Turin wakati Juventus inakwaruzana na Torino katika Ligi Kuu ya Serie A, mbali na burudani kutoka La Liga na Bundesliga ambazo zitawafanya mashabiki kutoruhusu watoto kuchezea rimoti.

Tuanze na leo Jumamosi. Kuna mechi mbili za kibabe zinapigwa jijini Mwanza na Dar es Salaam ambazo timu nne zinazomenyana zina nafasi sawa ya kukaa kileleni japo kwa muda kama zitashinda kwa kuishusha Mbeya City inayoongoza kwa sasa na pointi nane.

LIG 01


Mapema saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, wenyeji Pamba Jiji itakuwa wenyeji wa Singida Black Stars iliyotoka kutinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na yeyote atakayeshinda atakaa kileleni japo kwa muda kabla ya mechi ya saa 1:00 usiku.

Mechi hiyo ya usiku itazikutanisha JKT Tanzania yenye pointi saba na Simba yenye sita ambapo itakayozitumia vyema dakika 90 itakwea pia kileleni na kusubiria mechi za kesho Jumapili ambapo saa 10 jioni itakuwa ni zamu ya Yanga na KMC kabla ya Azam kuvaana na Namungo. KMC inaburuza mkia ikiwa na pointi tatu, huku Azam ikiwa na nne na Namungo ina pointi tano  zikitofautiana idadi ya mechi ilizocheza kila moja.

LIG 02


Jijini Mwanza rekodi zinaonyesha Pamba na Singida zilikutana mara mbili msimu uliopita, huku wageni wakivuna pointi nne dhidi ya moja ya wenyeji kwani ilishinda 1-0 kisha kutoka sare ya 2-2. Singida iliyocheza mechi mbili tu za Ligi msimu huu ina pointi sita na kama itashinda itafikisha pointi tisa na kuishusha Mbeya City, lakini kama itapoteza basi Pamba yenye nane itaongoza misimamo kwa kufikisha pointi 11 na iwapo ngoma itaisha kwa sare basi uwiano wa mabao utaiweka pia kileleni kwani itafikisha tisa.

Hili ni pambano la kibabe kutokana na timu zote kuwa na mastaa wakali wanaoweza kuamua mechi Singida ikiwa na Elvis Rupia, Malanga Horso Mwaku, Khalid Aucho na Morice Chukwu wakati Pamba ikitambia Peter Lwasa, Mathew Momanyi na Abdoulaye Yonta Camara.

Mechi hii lolote linaweza kutokea, licha ya rekodi kuibeba Singida iliyo chini ya kocha Miguel Gamondi, kwani vijana wa Francis Baraza nao sio wepesi.

LIG 03 (1)


Baada ya mechi hiyo ya jioni kazi itahamia jeshini saa 1:00 usiku wakati  JKT Tanzania na Simba zitakazoumana, huku wenyeji wakiwa na rekodi ya kinyonge mbele ya Mnyama waliocheza mechi mbili na kuvuna pointi sita na mabao sita.

Msimu uliopita Simba ilishinda nje ndni mbele y JKT yenye pointi saba ambapo ushindi wowote unaweza kuiweka kileleni na kama itapoteza na matokeo ya mechi ya jioni kwenda na sare, nasi mnyama atakaa kilele kwa saa 24 kabla ya mapambano ya kesho. JKT inatambia nyota wanaoongoza kwa mabao katika Ligi Kuu Paul Peter na Saleh Karabaka, mbali na kina Hassan Dilunga, Edward Songo ambao watakuwa na kazi ya kuivunja ngome ya Simba ya Rushine de Reuck, Chamou Karaboue na Wilson Nangu.

Hata hivyo Simba iliyoshinda mechi mbili za awali kwa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate na Namungo itaendelea kuwategemea Jonathan Sowah, Selemani Mwalimu, Jean Charles Ahou na Steven Mukwala kuichachafya ngome ya JKT Tanzania. Simba itaendelea kuwakosa kipa namba moja, Moussa Camara na beki wa kati Abdulrazak Hamza walio majeruhi, huku kiungo Mohammed Bajaber aliyerejea kutoka majeruhi huenda asicheze. Makocha wa timu zote wametambiana, Gamondi na Baraza kila mmoja akikiri mechi haitakuwa rahisi sawa na walivyosema Dimitar Pantev wa Simba na Ahmad wa JKT Tanzania.

LIG 03


Utamu wa ligi utaendelea kesho Jumapili kwa Yanga kuikaribisha KMC inayoumiliki Uwanja wa KMC Complex, ambapo hilo litakuwa pambano la pili kwa kocha Pedro Gonçalves wa Yanga akisaka pointi nyingine tatu kurejea kileleni mwa ligi.

Yanga ina pointi saba baada ya mechi tatu, wakati KMC inaburuza mkia ikiwa na tatu licha ya kushuka uwanjani mara tano.

Yanga ni moja ya timu ambazo haziruhusu bao lolote hadi sasa, lakini ikiwa imefunga matano na pia inabeba na rekodi tamu dhidi ya KMC inayonolewa na Marcio Maximo, ambaye yupo katika hatihati klabuni kutokana na matokeo mbaya kwa timu hiyo. Mara baada ya mechi hiyo ya jioni kwenye Uwanja wa Majaliwa,  Ruangwa Lindi, Azam FC iliyotinga makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika itakuwa wageni wa Namungo.