Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema linaendelea na msako mkali kuwatafuta wanaotuhumiwa kupanga, kuratibu na kutekeleza matukio ya vurugu, uporaji wa mali na uvunjifu wa amani uliotokea Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa polisi, Oktoba 29 kulitokea matukio ya vurugu, uporaji wa mali, uvunjifu wa amani katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya. Pia mikoa ya Shinyanga, Geita, Songwe, Ruvuma, Mara, Dodoma, Kilimanjaro na Iringa.
Vilevile, jeshi hilo limesema linawasaka ili kuwakamata watu 10 ambao limeorodhesha majina yao.
Licha ya kuwa Jeshi la Polisi halijaeleza kwa kina ushiriki wa watu hao, ila miongoni mwa hao wamo viongozi na makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mbali ya hao, anatafutwa pia Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na Award Kalonga.
Viongozi wa Chadema wanaotafutwa ni Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, Amani Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara), Godbless Lema (Mjumbe wa Kamati Kuu) na Boniface Jacob ‘Boni Yai’ (Mwenyekiti wa chama hicho, Kanda ya Pwani).
Wengine ni Brenda Rupia (Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa umma wa chama hicho) na Hilda Newton (kada wa chama hicho).
Yumo pia Machumu Maximilian maarufu Mwanamapinduzi na Deogratius Mahinyila (Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia Novemba 8, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, msako huo unafuatia uchunguzi na ushahidi uliokusanywa hadi sasa.
“Jeshi la Polisi linawataka kujisalimisha katika vituo vya polisi mara watakapoona taarifa hii popote walipo,” limeeleza jeshi hilo.
Hayo yametokea huku ukimya ukizidi kutawala miongoni mwa mamlaka za Serikali, likiwemo Jeshi la Polisi, hukusu idadi ya watu waliopoteza maisha au kujeruhiwa katika matukio hiyo.
Kuhusu kadhia iliyotokea Oktoba 29, Misime amesema matukio hayo yalisababisha madhara kwa binadamu, uharibifu wa mali za umma na binafsi na kuleta athari kubwa.
Mbali na athari za uhai na maisha ya watu, amesema mali za umma zilizochomwa moto, zikiwamo ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mahakama.
Uharibifu mwingine amesema ulitokea kwenye vituo vya mabasi yaendayo haraka kutoka Kimara Mwisho hadi Magomeni na Morocco, ATM za baadhi ya benki, ofisi za serikali za mitaa, barabara za lami na zege zilizomwa moto na baadhi ya majengo ya CCM, huku magari ya umma na binafsi yakiharibiwa.
“Mali za watu binafsi ziliharibiwa na kuchomwa moto, ikiwemo vituo vya mafuta, maduka, magari makubwa na madogo. Walifanya uporaji wa mali na fedha za watu kutoka katika maeneo ya biashara,” amesema.
Polisi katika taarifa hiyo limesema waliopanga na kutekeleza uhalifu huo wamekamatwa na kuanza kufikishwa mahakamani na kwamba, likishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea na msako mkali kuwatafuta wengine waliopanga na kuratibu.
Jana Ijumaa Novemba 7, 2025 watu 240 akiwamo mfanyabiashara Jennifer Jovin maarufu Niffer walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya uhaini kutokana na matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025.
Mbali ya hao, wengine 172 walifikishwa mahakamani jijini Mwanza na kusomewa mashtaka mbalimbali yakiwamo ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kuharibu mali kwa makusudi na kufanya maandamano bila kibali.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Oktoba 29 na 30 katika maeneo mbalimbali wilayani Nyamagana, mkoani Mwanza.
Katika taarifa ya Jeshi la Polisi, limeonya mtu au kikundi cha watu wanaopanga kufanya uhalifu wa namna yoyote likisema halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.
Pia limewatoa hofu Watanzania likiwataka kuendelea na shughuli zao, huku likiwaomba kutoa taarifa pale wanapoona dalili yoyote ya uhalifu au uvunjifu wa amani mahali popote ili hatua zichukuliwe.