Moshi. Jana katika simulizi ya mauaji ya muuguzi mstaafu wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Patricia Ibreck (66) tuliwaletea ushahidi wa mashahidi mbalimbali walioelezea taarifa za kutoweka kwake zilivyojulikana na hatimaye mwili wake kupatikana.
Mauaji yalifanywa na mganga wa jadi, Omary Mahmoud Rang’ambo, ambaye alimuua mwaka 2021 kwa kumnywesha dawa zisizojulikana kisha kumzika nyuma ya nyumba yake na kumweleza mwanaye kuwa amechukuliwa na mizimu.
Mauaji hayo yalitikisa mji wa Moshi na vitongoji vyake hasa ikizingatiwa kuwa, awali miongoni mwa walioshikiliwa kwa mahojiano ni mtoto wa marehemu, Wende Mrema, ambaye ilionekana baadaye hakuhusika.
Ni mauaji yaliyotokea tarehe na mwezi usiofahamika mwaka 2021 katika eneo la Rau Mrukuti, nje kidogo ya mji wa Moshi, lakini ilifahamika yuko India kwa matibabu. Baadaye iligundulika aliuawa na kuzikwa pembeni ya nyumba yake.
Mwili wake ulifukuliwa Januari 9, 2022 ikiwa ni baada ya mwaka mmoja kupita na ndani ya shimo alimozikwa, kulikutwa pia jambia lililotumika katika mauaji, shuka lililotumika kufunika mwili wake na sidiria ikiwa kifuani mwa marehemu.
Ni kutokana na ushahidi uliokusanywa, Omary alifikishwa mahakamani na kushitakiwa kwa mauaji ya kukusudia na Novemba 5, 2025, Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu Moshi alimtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kifo.
Katika simulizi ya leo, tunawaletea ushahidi wa Wende, mtoto wa marehemu aliyeeleza namna alivyokutana na waganga wa jadi, kisha wakasalitiana wao kwa wao na wakabaki na mganga aliyefanya mauaji hayo.
Katika ushahidi alioutoa mahakamani akiwa shahidi wa sita wa Jamhuri, Wende anaeleza yeye ndiye alikuwa akiishi na mama yake na hakuwa na uhakika kama amekufa, ila aliambiwa alikufa mwaka 2021.
Aliieleza mahakama kabla ya kifo chake, mama yake alikuwa na jeraha kubwa mguuni kiasi kwamba mguu ulioza na kwamba alitibiwa katika hospitali mbalimbali nchini bila mafanikio.
Mwaka 2016 wakati anasoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) katika kituo kilichopo Majengo mjini Moshi, alimwelezea dada mmoja masaibu anayopitia mama yake, ndipo akamtambulisha kwa mganga wa jadi.
Alimtaja mganga huyo kuwa Waziri Selemani Ally, aliyekuwa akiishi eneo la Njoro, mjini Moshi ambaye alimtibu yeye (Wende) na mama yake. Baadaye yeye na mganga huyo wa jadi walikuja kuwa na mahusiano ya kimapenzi.
Mganga huyo alikuwa akiishi mwenyewe Njoro, lakini Korogwe alikuwa akiishi na mkewe, watoto na mshtakiwa katika kesi hiyo, Omary Mahmoud, ambaye naye alikuwa akifanya kazi za uganga na Waziri wakiwa Njoro na Korogwe.
Waziri alimtambulisha Omary kama mwanafunzi wake wa shughuli za uganga na alikuwa akiishi katika Mji wa Bomang’ombe uliopo wilayani Hai. Mwaka 2020, Wende alikwenda Korogwe kwa Waziri na aliishi huko kwa muda fulani.
Baadaye alirudi Moshi ambako siku moja Omary alimpigia simu akamuuliza kama amerudi Moshi, akamjibu ndiyo amerudi, ndipo Omary alimwambia yeye ndiye amemsaidia kutoka salama kwa mganga ambaye ni Waziri.
Omary alimweleza Wende kuwa bosi wake katika uganga (Waziri) alikuwa amemfanyia mambo mabaya na alikuwa anamtaka auze shamba na baadaye Waziri angemuua yeye (Wende) na mtoto wake na baadaye kuwafanya misukule.
Katika ushahidi, alieleza Omary alimweleza kuwa, bosi wake hana uwezo wa kumtibu mama yake, hivyo alimtaka ampe kiasi fulani cha pesa ili amsaidie kumtibu. Aliuza shamba kwa Sh30 milioni na kumtumia Omary.
Wende alieleza kuwa Omary alimjulisha angekwenda Moshi akiongozana na mtoto wake aitwaye Abdul. Alifika akawatibu yeye na mama yake, akamwachia dawa kwa ajili ya mama yake na kuondoka ila waliendelea kuwasiliana.
Baadaye, Omary aliendelea kuwasiliana naye kuhusu maendeleo ya mguu wa mama yake na alikuwa akimtaka mara kwa mara amtumie fedha kwa ajili ya kufanya matambiko katika nyumba ya mama yake iliyopo Rau mjini Moshi.
Shahidi aliendelea kuuza mali zake na kumtumia fedha Omary.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, hali ya mama yake haikubadilika, hivyo akamtaka amwambie Omary kuwa hataki aendelee kumtibu tena na amweleze Omary na washirika wake ni waongo na ni matapeli.
Alieleza mama yake pia alimwambia, Omary na wenzake walikuwa wanadai pesa nyingi. Wende alivyomwambia Omary alichukizwa na hilo, akamwambia mizimu haijafurahishwa, hivyo ingemwadhibu au kumuua.
Katika ushahidi wake ameeleza alimuomba radhi Omary kwa niaba ya mama yake ili asije akadhurika kwa njia yoyote na hakuwasiliana tena na Omary kwa kipindi.
Wende aliiambia mahakama kuwa mwanzo mwa mwaka 2021, Omary alimpigia simu akimweleza kuwa anataka kwenda nyumbani kwao kwamba kuna dawa alitaka kuwapelekea na kumaliza kazi ya uganga ambayo alikuwa anaifanya.
Kweli Omary akaenda nyumbani kwao na kumpa dawa na kumtaka ampe kikombe na kijiko ili awape dawa ambayo yeye na mama yake wangeinywa.
Kwa mujibu wa Wende, mama yake alikataa kunywa dawa hiyo na alipomweleza Omary, akamtaka yeye (Wende) abaki nje ya nyumba ili aingie sebuleni kwa lengo la kuzungumza na mama yake juu ya uamuzi wake.
Baada ya muda mfupi, Omary alimfuata shahidi huyo nje alipokuwa akamweleza kuwa mama yake amekubali kunywa dawa ambayo amewaletea. Akamimina dawa hiyo na kumtaka Wende anywe na akachukua nyingine akampelekea mama yake.
Mganga huyo akamtaka Wende kusubiria nje, baadaye mama yake alikwenda maliwatoni na akamwita Wande akamsaidie. Alipokwenda alimkuta mama yake akiwa amechoka na anatokwa jasho.
Mama yake alimwambia anajihisi kutapika, hivyo ampeleke nje. Ni katika wakati huo, Wende alimwita Omary na kumuuliza ni kwa nini hali ya mama yake imebadilika ghafla, naye akamwambia ana matatizo makubwa.
Kwa mujibu wa ushahidi wa Wende, alimchukua mama yake na kumpeleka sebuleni akamkalisha kwenye kochi, lakini mganga akataka yeye ampeleke chumba chake cha kulala kwani anahitaji kupumzika.
Alimpeleka mama yake chumbani ambako alimpa ndoo na alitapika sana.
Akamweleza Omary hali ya mama yake imebadilika sana lakini akamjibu hiyo inasababishwa na dawa alizompa na zinaonyesha kufanya kazi.
Omary akaenda nje na kurejea na dawa kwenye kikombe akampa mama yake, akieleza itamsaidia kuacha kutapika. Alimlazimisha kunywa kwa kuwa mama yake alikataa kuinywa.
Usikose mwendelezo wa simulizi hii kesho ambapo tutaeleza kilichoendelea na namna mauaji yalivyofanyika, kisha mganga kumzika Patricia.