Sadc yampongeza Rais Samia, yatoa pole kwa familia za waliopoteza maisha

Dar es Salaam. Mkutano mkuu maalumu wa wakuu wa nchi na Serikali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) umempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine waliochaguliwa katika chaguzi za Septemba na Oktoba 2025.

Vilevile, Sadc imetoa salamu za rambirambi kwa familia za watu waliopoteza maisha kwenye maandamano ya Septemba hadi sasa nchini Madagascar na Tanzania hivi karibuni wakati wa uchaguzi mkuu.

Mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao jana Novemba 7, 2025, ulihudhuriwa na viongozi wa kitaifa kutoka mataifa 15 wanachama huku Tanzania ikiwakilishwa na makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi.

Itakumbukwa kwamba Oktoba 29, 2025, Watanzania walipiga kura kuchagua Rais, wabunge na madiwani ambapo katika mkutano huo, Rais Samia aliibuka mshindi kwa muhula wake wa pili, kisha akaapishwa Novemba 3, 2025 jijini Dodoma.

Mbali na Rais Samia, mkutano huo, pia, umempongeza Profesa Arthur Peter Mutharika ambaye katika uchaguzi wa Septemba 16, 2025, alichaguliwa kuwa Rais wa Malawi kwa muhula wa pili, akimwangusha aliyekuwa akikalia kiti hicho, Lazarus Chakwera.

Mwingine aliyepongezwa na viongozi hao wa Sadc ni Dk Patrick Herminie, Rais wa Jamhuri ya Shelisheli ambaye alichaguliwa katika uchaguzi wa Septemba 27, 2025, akiahidi kupunguza gharama za maisha kwa wananchi wake.

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja (Communique) iliyotolewa na Sadc, viongozi hao wamepongezwa kwa kushinda uchaguzi katika mataifa yao.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba mkutano huo ulitoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao wakati wa maandamano yaliyotokea Madagascar, Septemba 2025 na hivi karibuni nchini Tanzania.

“Mkutano ulielezea masikitiko makubwa kwamba matukio haya yalisababisha sio tu upotevu wa maisha, bali pia uharibifu wa mali za umma na miundombinu muhimu katika mataifa yote mawili,” imeeleza taarifa hiyo ya wakuu wa nchi.

Wakati huohuo, mkutano ulitambua uamuzi wa Madagascar wa kuachia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Sadc kufuatia hali ya kisiasa ya hivi karibuni ambayo imeathiri uwezo wake wa kutekeleza majukumu katika nafasi hiyo.

Mkutano huo ulitambua kwamba, kwa mujibu wa Kifungu cha 9A(2)(b) na 10(4) cha Mkataba wa Sadc, Mwenyekiti Anayeingia (Naibu Mwenyekiti) atachukua uongozi wa muda endapo Mwenyekiti aliyepo hatoweza kutekeleza majukumu yake.

“Kwa muktadha huu, Jamhuri ya Afrika Kusini iliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa muda wa Sadc hadi Agosti 2026. Sekretarieti ya Sadc itashirikiana na nchi wanachama, kwa kuzingatia kanuni ya mzunguko wa uongozi ili kumtambua Mwenyekiti Anayeingia (Naibu Mwenyekiti) mpya kufikia Novemba 30, 2025,” inaeleza taarifa hiyo.