Arusha. Baadhi ya wananchi waliopata hasara ya biashara zao kuporwa na nyumba kuteketezwa kwa moto kufuatia maandamano yaliyofanyika Oktoba 29, 2025, wameiomba Serikali iwafute machozi ili waweze kurejesha maisha yao kama yalivyokuwa awali na waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Pia, wameishauri Serikali iweke utaratibu utakaowezesha wananchi wenye nia ya kufikisha kero zao kwa njia ya maandamano watekeleze haki yao kikatiba bila kuathiri shughuli za kibiashara na maisha ya kawaida ya watu wengine.
Mmoja wa wakazi wa Kata ya Moivo Wilaya ya Arumeru, aliyezungumza na Mwananchi, Evelyne Mmari amesema athari walizopata kibiashara itachukua muda mrefu kurejea katika hali waliyokuwa wamefikia, hivyo wanaomba kupewa unafuu wa kurejesha mikopo.
Mmari ambaye alikuwa akimiliki duka la jumla na huduma za kifedha, ameeleza kupata hasara ambayo hajui namna atakavyoweza kurejea tena na kuendelea na shughuli za kiuchumi baada ya vijana waliokua wakiandamana siku ya uchaguzi kuteketeza kwa moto maduka ambayo yeye alikuwa mpangaji.
“Nimepoteza kila kitu kilichokuwemo dukani, siku chache kabla ya uchaguzi niliingiza bidhaa za zenye thamani ya Sh7 milioni, nilikuwa wakala wa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi na benki mbalimbali, hakuna kilichosalimika zikiwemo mashine, fedha na simu za kutolea huduma,” amesema Evalyne.
Naye Benjamini Laizer, mjasiriamali aliyekuwa akiuza chakula na vinywaji akiwa ameajiri wafanyakazi saba, amesema mali zilizoteketea ni zaidi ya Sh20 milioni huku wafanyakazi wake wanane wakiachwa bila kazi katika kipindi hiki.
Amesema alichokishudia hakikuwa maandamano ya amani bali ni makundi ya vijana waliokuwa na nia ya kupora na kuharibu mali za wananchi wema walioamua kujibidiisha kwa ajili ya familia zao na kutengeneza ajira kwa vijana.
“Maandamano yanapaswa kuwa ya amani na waandamanaji wanakuwa na mabango yanayoonyesha ujumbe wanaotaka kuufikisha kwa Serikali, lakini hatukuona hayo yote bali ni uporaji, kuumiza watu na kuteketeza mali, jambo ambalo haliendani na haki ya kikatiba ya kuandamana,” amesema Laizer.
Ameongeza kuwa uwepo utaratibu wa kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii, anaamini ilikuwa chanzo cha kuchochea vijana wengi kufanya maandamano yasiyokua ya amani na kutokuheshimu biashara za wananchi wenzao.
Pia, wakazi wengine wa eneo hilo, Nicodemus Peter na Bertha Moe wameeleza masikitiko yao kutokana na hasara waliyopata kwenye shughuli zao za kiuchumi wakitaka kuwepo na ustahimilivu wa kusikiliza na kuheshimu mawazo tofauti ya kisiasa ili kuwe na haki na amani.
“Tumetoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu,tumekuja arusha kutafuta maisha tofauti za misimamo ya kisiasa zisitugawe na kuzuia wengine tushindwe kufanya shughuli za kiuchumi kwa lengo la kujipatia kipato cha kuendesha familia zetu, tunaposhindwa kufanya kazi hali ya uhalifu inaongezeka mtaani,” amesema Moe.
Maeneo yaliyoathirika ni ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Moivo, yenye fremu za biashara, nyumba za biashara za watu binafsi, Mahakama ya Mwanzo Enaboishi, ofisi za serikali za mitaa na baadhi ya makazi binafsi ya wananchi.