Dar es Salaam. Licha ya kuzua mjadala, kujitoa kwa Dk Tulia Ackson kwenye kinyang’anyiro cha uspika kunaweza kufananishwa na ilivyokuwa wakati wa mabadiliko ya maspika wengine, kulingana na mazingira mapya ya uongozi wa nchi.
Dk Tulia ameacha alama kadhaa ikiwamo msisitizo wake katika utawala wa sheria, uwezo wake wa kuleta utulivu bungeni, na zaidi ya yote, mafanikio katika diplomasia ya Bunge kwa kushinda urais wa Muungano wa Mabunge Duniani (IPU) Oktoba 2023.
Hivyo, kama ilivyokuwa kwa maspika wa zamani, mabadiliko haya yanaweza kutafsiriwa kama sehemu ya mzunguko wa kawaida wa mageuzi katika taasisi ya Bunge, ambapo kila uongozi huacha chapa yake kulingana na mazingira yake ya kihistoria na kisera.
Uamuzi huo wa Tulia umeelezwa na baadhi ya wachambuzi kwamba licha ya kujiondoa, bado kiongozi huyo ana sifa za kimataifa na anaweza kupata nafasi zingine za uongozi ndani ya Serikali.
Seif Nassor Amour, mchambuzi wa masuala ya siasa, amesema Dk Tulia ana sifa nyingi za kuwa kiongozi kuanzia ndani na nje ya nchi kupitia mashirika, taasisi na asasi za kimataifa kwa sababu ana sifa na vigezo vyote.
Amour amefafanua kuwa Dk Tulia ana umuhimu wake ndani ya Bunge, hivyo anajua akiacha kuwania usipika kuna nafasi anaweza kuipata kubwa zaidi.
“Utendaji kazi wake katika Bunge la 12 ulikuwa mzuri ni miongoni mwa mambo yanayombeba Dk Tulia, hivyo anastahili fursa ya kupata nafasi nyingine zaidi ikiwemo mashirika ya kimataifa. Ni mtu ambaye ana misimamo na kanuni nzuri ya kiuongozi.
“Nahisi analenga kwenda mashirika ya Umoja wa Mataifa, ninachokiona. Unajua angeingia na kushindwa mbele ya Zungu (Mussa Hassan Zungu), mrejesho wake ungekuwa si mzuri, ni kama vile mchezaji mpira anatakiwa aache mpira akiwa bado na kiwango, sio unachaa mpira ukiwa umeshachoka, Tulia bado anauzika,” ameeleza Amour.
Mchambuzi wa siasa na uchumi, Gabriel Mwang’onda amesema ni vigumu kuzungumzia uamuzi wa Dk Tulia kujitoa kuwania kuwania uspika kwa sababu ni masuala binafsi na mhusika hakutoa sababu za kufikia hatua hiyo.
“Sina ‘comment’ (maoni) hapo kwa sababu ni ngumu kusema, angetoa sababu ningekuwa na uwezo wa kujua anataka nini. Lakini ni ngumu kujua anafikiri nini, tuna tabiri tabiri tu,” amesema.
Walivyoondoka maspika wenzake
Uchaguzi wa Spika wa mwaka 2005 ulifanyika baada ya Uchaguzi Mkuu uliomuingiza madarakani, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.
Pius Msekwa alikuwa ni spika aliyekalia kiti hicho kwa mihula miwili kamili (kuanzia 1995 hadi 2005). Alikuwa akitazamwa kama kiongozi mwenye uzoefu mkubwa, huku mpinzani wake Samuel Sitta alikuwa mwanasiasa na waziri mstaafu mwenye uzoefu serikialini.
Hata hivyo, tofauti kati yao ilikuwa kati ya mfumo wa kuendeleza mazoea (Msekwa) na mfumo wa mabadiliko (Sitta), ambao uliendana na kauli mbiu ya “ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya” ya Rais Kikwete na vuguvugu la wanamtandao.
Kulingana na utayari wa CCM kwenye mabadiliko, iliamua kuachana na kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu (Msekwa) na kumchagua Sitta, ambaye alionekana kuwa na ari mpya inayolingana na kasi ya Serikali mpya.
Uchaguzi Mkuu wa 2010, ambao ulishuhudia CCM ikipata ushindi na Rais Jakaya Kikwete akianza muhula wake wa pili. Sitta pia alikuwa anatafuta muhula wa pili kwenye Spika.
Sitta katika nafasi yake ya Spika alikuwa amejijengea sifa ya kuibana Serikali kwa falsafa yake ya ‘speed and standard” kwa maana ya Bunge lenye kasi na viwango.
Licha ya Sitta kuimarisha taasisi ya Bunge kwa kusisitiza uwazi na uwajibikaji, na hata kusimamia kikao kilichopelekea Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa, kujiuzulu kufuatia kashfa ya Richmond na hivyo kupata heshima na umaarufu mkubwa miongoni mwa wananchi, bado alihudumu kwa muhula mmoja pekee wa 2005–2010.
Hata kwa rekodi hiyo yenye uzito wa kiuongozi, jina lake halikupenya katika vikao vya CCM, hali iliyodhihirisha changamoto za kisiasa zilizozunguka nafasi ya uongozi ndani ya chama hicho.
Ingawa Sitta alipongezwa na umma kwa kulifanya Bunge liwe imara lenye meno, baadhi ya viongozi wa Serikali na ndani ya chama (CCM) waliona utendaji wake kama wenye mamlaka kupita kiasi.
Uongozi wake ulihusisha misimamo mikali, hasa katika kamati zake, ambazo zilifichua ufisadi na udhaifu serikalini.
Pia, katika kipindi hicho, kulikuwa na hisia kwamba Sitta alikuwa akijijenga kwa ajili ya kugombea urais mwaka 2015, hivyo ulipofika uchaguzi wa Spika na akajitokeza Andrew Chenge na kusababisha mvutano wa kimakundi.
Hata hivyo, uongozi wa juu wa CCM na Serikali walihitaji Spika ambaye angekuwa na uwezo wa kusawazisha makundi hayo na kurejesha uhusiano kati ya Bunge na Serikali, ukasema safari hii tunakwenda na mwanamke
Naibu Spika Anne Makinda ndiye alitazamwa kama kiongozi ambaye angeleta utulivu zaidi na kuepusha migogoro ya mara kwa mara.
Pia, uamuzi wa kumchagua Makinda ulikuwa na sura ya kihistoria. Ilikuwa ni fursa ya kumweka mwanamke wa kwanza katika historia ya Tanzania katika kiti cha Spika wa Bunge.
Hili lilikuwa uamuzi wa kimkakati wa kisiasa kwa CCM kuonyesha utayari wake wa kuwainua wanawake katika ngazi za juu za uongozi.
Pia, Makinda aliongoza Bunge kwa utulivu na kwa kufuata kanuni, akipunguza kasi ya Bunge yenye migongano mikali na Serikali ambayo ilikuwepo chini ya Sitta.
Makinda baada ya kuongoza Bunge kwa kipindi cha miaka mitano, alitangaza kustaafu na hivyo hakukombea ubunge wala uspika, hivyo Job Ndugai aliyekuwa Naibu Spika aligombea nafasi hiyo na jina lake kupenya ndani ya vikao vya CCM.
Uchaguzi wa Spika wa 2015 ulifanyika baada ya Dk John Magufuli kuchaguliwa kuwa Rais. Kulikuwa na ari mpya ya utawala iliyosisitiza Hapa Kazi Tu, uwajibikaji mkali, na kupambana na urasimu na ufisadi.
Bunge lilihitaji Spika ambaye angeendana na kasi hiyo mpya ya Serikali ya Awamu ya Tano, ambaye angekuwa imara na asiyeyumbishwa katika kuongoza Bunge lenye upinzani wenye nguvu na lenye hoja kali.
Ndugai, kama Naibu Spika, alikuwa amejijengea taswira ya mtu mwenye msimamo thabiti, wa moja kwa moja, na ambaye alionekana kuwa tayari zaidi kuongoza Bunge kwa mkono wa chuma kama yalivyokuwa mahitaji ya Serikali chini ya Magufuli.
Job Ndugai alijiuzulu uspika kutokana na mzozo wa kisiasa uliotokana na kauli yake kuhusu deni la taifa, uliotafsiriwa kama ukosoaji wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Shinikizo la kisiasa kutoka ndani ya CCM, pamoja na hamu yake ya kulinda heshima ya Bunge na utulivu wa taifa, vilimfanya achukue hatua ya kujiondoa kwa hiari.
Januari 6, 2022, Ndugai aliandika barua rasmi ya kujiuzulu kwa Katibu wa Bunge akieleza kuwa ameamua kuachia nafasi ya Spika kwa hiari yake binafsi.
Baada ya barua hiyo kupokelewa, taarifa rasmi ilitolewa kwa umma kupitia Ofisi ya Bunge na Ofisi ya CCM, kuthibitisha kuwa uongozi wa Bunge ulikuwa sasa chini ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, hadi uchaguzi wa Spika mpya ufanyike.
Mojawapo ya alama kuu za Tulia ni mwelekeo wake wa kuliongoza Bunge ambalo linazingatia sheria na taratibu, huku akijitahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali bila kuliachia Bunge kudhalilika.
Pia, Tulia amekuwa akisisitiza utii kamili kwa Katiba na Kanuni za Kudumu za Bunge. Ametumia mamlaka yake kuzuia vurugu na lugha chafu ndani ya Bunge, akisisitiza mijadala inayoheshimika.
Akiwa Spika chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan (Awamu ya Sita), Tulia amejitahidi kuonyesha usawa katika kutoa fursa kwa wabunge wa upinzani na wabunge wa CCM kuchangia, jambo ambalo limepokelewa vyema na wengi kama hatua ya kuimarisha demokrasia ya kibunge.
Pia, katika uongozi wake amesisitiza Kamati za Bunge kufanya kazi kwa kina na uchambuzi zaidi, hasa katika masuala ya bajeti na ukaguzi wa miradi ya Serikali. Hili linasaidia kulifanya Bunge kuwa na mchango wa kitaalamu zaidi.
Kama mwanamke wa pili kushika nafasi hiyo baada ya Anne Makinda, amejitahidi kuongeza heshima na weledi katika kiti cha Spika, akitangaza Bunge lenye utulivu na ambalo linaheshimika ndani na nje.