Dar es Salaam. Chanjo mpya ya majaribio ya malaria iitwayo SUM-101 imeonyesha matokeo ya kutia moyo katika jaribio la kwanza miongoni mwa watu wazima nchini Tanzania, ambao tayari walikuwa wamewahi kuambukizwa ugonjwa huo.
Utafiti huo ulioongozwa na Aina-ekisha Kahatano na Maxmillian Mpina kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), ulibaini kuwa chanjo hiyo ni salama, inavumilika vizuri na inaweza kuchochea mwitikio mkubwa wa kinga ya mwili, jambo linaloashiria hatua muhimu katika mapambano ya dunia dhidi ya malaria.
Matokeo haya yanaonyesha kuwa chanjo hiyo inaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuboresha kizazi kijacho cha chanjo za malaria, ikisaidia zile zilizopo kama RTS’s na R21 ambazo tayari ziliidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) miaka michache iliyopita zinazotoa ulinzi wa kiasi.
Licha ya maendeleo makubwa katika kuzuia na kudhibiti malaria, ugonjwa huo bado unasababisha madhara makubwa hasa Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako bado ni miongoni mwa visababishi vikuu vya magonjwa na vifo.
Tanzania pekee inarekodi mamilioni ya idadi ya wagonjwa kila mwaka. Chanjo bora zaidi inayolenga hatua tofauti ya vimelea vya malaria inaweza kuongeza ufanisi wa ulinzi kwa kiwango kikubwa.
Watafiti Kahatano na Mpina, ambao ni waandishi wenza wakuu kutoka Taasisi ya Ifakara, wamesema matokeo haya yanaonyesha matumaini makubwa ya kuboresha chanjo za malaria, hasa katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi.
“Utafiti huu unaongeza ushahidi kuwa mchanganyiko wa chanjo zinazolenga hatua ya damu na hatua ya awali ya vimelea, unaweza kutoa ulinzi mpana na wa kudumu zaidi,” amesema Kahatano.
Kilichobainika katika utafiti
Utafiti huu wa kitabibu ulifanyika Bagamoyo, Tanzania, ukiwahusisha watu wazima 40 wenye afya, wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 45 wote wakiishi katika maeneo yenye maambukizi ya kawaida ya malaria.
Washiriki waligawanywa kwa nasibu katika makundi mawili, kundi moja lilipokea chanjo ya malaria ya SUM-101 na jingine likapewa chanjo ya kawaida ya kichaa cha mbwa kwa ajili ya kulinganisha.
Akitaja matokeo makuu, Kahatano amesema hakuna madhara makubwa, athari nyingi baada ya chanjo zilikuwa ndogo, kama vile maumivu madogo katika sehemu ya sindano, maumivu ya kichwa au uchovu wa muda mfupi.
“Kulikuwa na mwitikio mkubwa wa kinga, SUM-101 ilizalisha kiwango kikubwa cha kingamwili (IgG na IgM), kilichofikia kilele karibu siku ya 84 na kubaki juu kwa miezi kadhaa,” amesema.
Amesema kulikuwa na ulinzi dhidi ya aina tofauti za vimelea, kingamwili zilizozalishwa ziliweza kutambua na kushambulia aina mbalimbali za vimelea vya malaria.
Kulikuwa na uimarishwaji wa kinga ya asili. “Watu ambao tayari walikuwa na kinga fulani dhidi ya malaria walionyesha mwitikio bora zaidi baada ya chanjo,” amesema.
Watafiti waliokuwa wakisimamia jaribio hili Dk Ally Olotu kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara na Dk Claudia Daubenberger kutoka Taasisi ya Afya ya Umma na Kitropiki ya Uswisi, walisema chanjo ya SUM-101 haikuwa tu salama, bali pia iliimarisha kinga ya asili ya mwili dhidi ya malaria.
Jaribio hili la kitabibu la awamu ya kwanza (Phase Ib) lililochapishwa katika eClinicalMedicine, sehemu ya The Lancet Discovery Science Novemba, 2025 linaonyesha nguvu ya ushirikiano wa kisayansi wa kimataifa.
Utafiti uliendeshwa kwa pamoja na watafiti kutoka Taasisi ya Afya Ifakara kutoka Tanzania, Taasisi ya Afya ya Umma na Kitropiki ya Uswisi, Chuo Kikuu cha Basel (Uswisi), Sumaya Biotech GmbH & Co. KG (Ujerumani) na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Heidelberg (Ujerumani).
Utafiti huu ulipata ufadhili wa sehemu kutoka Sumaya Biotech GmbH & Co. KG kupitia msaada wa EU Malaria Fund Berlin.
Mwandishi mwenza wa Taasisi ya Afya Ifakara, Mpina amesema timu ya utafiti inaamini matokeo hayo yanafungua njia ya kufanyika kwa majaribio makubwa zaidi ili kupima ufanisi wa SUM-101 katika makundi mapana zaidi ya watu, wakiwamo watoto ambao ndio waathirika wakuu wa malaria.
“Tunayo matumaini kuwa chanjo hii inaweza kuwa sehemu ya kizazi kipya cha chanjo za malaria salama zaidi, zenye nguvu zaidi na zenye uwezo wa kuokoa mamilioni ya maisha,” amesema.
Kadri taasisi hiyo inavyoendelea kuongoza tafiti za aina hii za kibunifu, utafiti huo unaonyesha jinsi Tanzania inavyozidi kuchangia katika uvumbuzi wa afya duniani na katika kufanikisha ndoto ya dunia isiyo na malaria.