TIMU nne za Tanzania zinazoshiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika zimeshajua zinakutana na wapinzani gani katika mechi sita zikiwa ni Yanga, Simba, Azam FC na Singida Black Stars.
Yanga iko Ligi ya Mabingwa ikiangukia kundi B linalojumuisha timu kama Al Ahly (Misri), JS Kabylie (Algeria) na AS FAR Rabat (Morocco). Mabingwa hao mara nne mfululizo wa Bara wameonekana kama wameangukia kundi gumu zaidi.
Wakati Simba ambayo inashiriki mashindano hayo ikipangwa kundi D lenye timu za Esperance de Tunis (Tunisia), Stade Malien (Mali) na Petro de Luanda ya Angola.
Azam ipo Shirikisho ikiwekwa kundi B pamoja na AS Maniema (DR Congo), Wydad Athletic (Morocco) na Nairobi United (Kenya), wakati Singida Black Stars ambauo iko katika mashindano hayo ikipangwa kundi C lenye timu za Stellenbosch (Afrika Kusini), CR Belouizdad (Algeria) na Otoho d’Oyo (Kongo Brazaville).
Kila timu kwenye hatua hiyo itacheza mechi sita zikiwemo tatu za nyumbani na tatu ugenini kusaka tiketi ya kwenda kucheza hatua ya robo fainali, ambapo Bara ikibahatika kwa mara ya kwanza kupeleka nne hatua ya makundi.
Kupangwa kwa ratiba hiyo kumeleta habari njema kwamba, wapo wachezaji na makocha ambao waliwahi kufanya kazi hapa nchini na sasa watarejea kwa sura nyingine kuchuana na timu za nchini wakiwa kama wapinzani.
Hebu waangalie mastaa sita ambao mechi hizo za makundi zitakapoanza watakuja nchini kwa nyakati tofauti kuziongoza timu zao kusaka ushindi wakiwa wamewahi kufanya kazi Tanzania na timu mbalimbali.
BABACAR SARR (JS KABYLIE)
Kiungo Babacar Sarr, raia wa Senegal anarudi kivingine nchini na safari hii akiwa na kikosi cha JS Kabylie ya Algeria inayoshiriki Ligi ya Mabingwa na ataendelea kuwa mpinzani mkubwa wa Yanga ambayo atakutana nayo kwenye mechi za mashindano hayo.
Sarr alisajiliwa na Simba Januari 6, 2024 wakati huo ikifundishwa na kocha Abdelhak Benchikha, lakini kiungo huyo alidumu kwa miezi sita akaachana na wekundu hao mara baada ya ligi kumalizika kisha akatua kwa Waalgeria hao.
Kiungo huyo ni nguzo muhimu ya Kabylie na juzi tu amefunga bao la kwanza wakati timu yake ikishinda mchezo wa ligi nyumbani dhidi ya El Bayadh kwa mabao 4-1 Septemba 3, 2025 ambapo atakutana na Yanga hapa nchini kwenye mchezo wa mwisho wa makundi mwakani Februari 13, 2026 lakini akitangulia kukutana nayo nyumbani Novemba 28,2025 kwenye mchezo wa pili wa makundi.
SEAD RAMOVIC (CR BELOUIZDAD)
Mashabiki wa Yanga wanamkumbuka kocha Sead Ramovic, aliyewaachia soka flani likipewa jina la ‘gusa, achia twende kwao’ ambaye alifanya kazi kwa kipindi kifupi kisha akawakimbia akitua CR Belouizdad ya Algeria.
Ramovic, raia wa Ujerumani anarudi nchini, lakini safari hii akiwa mpinzani wa Singida Black Stars ambayo atakuta nayo hapa nchini Februari 8, 2026 kule Zanzibar kwenye mchezo wa tano wa makundi, lakini timu hizo zitatangulia kukutana Novemba 23, 2025 kwenye mchezo wa kwanza wa makundi nchini Algeria.
STEPHANIE AZIZ KI (WYDAD ATHLETIC)
Sio rahisi kuwa shabiki wa soka usimjue kiungo Stephanie Aziz KI ambaye alifanya kazi Yanga mpaka karibu na mwisho wa msimu uliopita, lakini sasa anarudi nchini tena akikutana na Azam FC ambayo anaijua vizuri.
Aziz KI alipoondoka Yanga aliuzwa Wydad Athletic, ambayo anakuja nayo nchini kukutana na matajiri wa Chamazi ambao amewahi kuwafunga Bara.
Kiungo huyo atakuwa nchini akikutana na Azam Novemba 30, 2025 Zanzibar kisha baadaye atamalizana nao kwenye mchezo wa mwisho wa makundi Februari 15, 2026 kule nchini Morocco.
MPHO MARUPING (CR BELOUIZDAD)
Yanga iliwahi kuwa na mtaalamu wa kusoma mikanda ya video kutoka Afrika Kusini ambaye ni huyo Mpho Maruping ambaye alitua nchini wakati wa utawala wa aliyekuwa kocha Miguel Gamondi na sasa anarudi tena Bongo akiwa na kikosi cha CR Belouizdad.
Mpho alichukuliwa na Ramovic akiungana naye kwenye kikosi cha Waalgeria hao na sasa anarudi na bosi wake huyo wa zamani wakiwa wapinzani wa Singida Black Stars.
Watakaokuta nao hapa nchini Februari 8,2026 kule Zanzibar kwenye mchezo wa tano wa makundi, lakini timu hizo zitatangulia kukutana Novemba 23, 2025 kwenye mchezo wa kwanza wa makundi nchini Algeria.
Singida Black Stars imewahi kuwa na wachezaji wengi mahiri kutoka sehemu mbalimbali duniani, lakini watatu ambao waliomba uraia Tanzania wakiwemo Emmanuel Keyekeh, Mohammed Damaro na huyu Arthur Bada. Lakini baadaye Bada aliondoka nchini na kutimkia JS Kabylie ya Algeria mwisho wa msimu uliopita.
Mchezaji huyo anarejea nchini safari hii akiwa mpinzani wa Yanga ambayo iliwahi kutaka kumsajili wakati akiwa Singida Black Stars, na atakutana na Yanga hapa nchini kwenye mchezo wa mwisho wa makundi Februari 13, 2026.
Lakini, ikumbukwe kwamba watatangulia kukutana nyumbani Novemba 28, 2025 kwenye mchezo wa pili wa makundi, ambapo mchezo wa mwisho kuichezea timu hiyo ni ule wa ligi dhidi ya Khenchela Oktoba 21,2025 timu yake ikishinda kwa bao 1-0 lakini akikosa mechi tatu zilizofuata.
MUSTAPHA KODRO (CR BELOUIZDAD)
Kocha Mustapha Kodro wa CR Belouizdad atakuja kama msaidizi wa kwanza wa Ramovic kwenye kikosi cha Waalgeria hao.
Kondro aliwahi kuja nchini pia na Ramovic na atakuwa kwenye benchi la Mjerumani huyo litakalokutana na Singida Black Stars Februari 8, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar katika mchezo wa tano wa makundi, lakini timu hizo zitatangulia kukutana Novemba 23, 2025 kwenye mchezo wa kwanza wa makundi kule Algeria.