KIUNGO wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana amesema ongezeko la wachezaji ndani ya kikosi hicho baada ya uongozi kukamilisha usajili kwenye mfumo limeongeza chachu ya ushindani huku akiitahadharisha Pamba Jiji.
Fountain Gate imerejea mazoezini Jumatano wiki hii tayari kwa ajili ya kujiweka sawa na mechi zijazo za Ligi Kuu Bara huku ikielezwa kurudi kwao mapema ni kutengeneza muunganiko na utimamu wa mwili kwa nyota ambao walikuwa nje ya mfumo na kukosa baadhi ya michezo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kulandana alisema ana imani kubwa na timu hiyo kufanya vizuri msimu huu kutokana na usajiri alioutaja kuwa ni bora na anaamini ushindani uliopo ndani ya timu utafanya hadi kwa timu pinzani pindi watakapokutana.
“Hatujaanza vizuri msimu kutokana na kuanza na idadi ndogo ya wachezaji, sasa tupo kamili wapinzani wajipange tunaendelea na mazoezi ushindani ni mkubwa wenyewe kwa wenyewe, kila mchezaji anaitaka namba kikosi cha kwanza, hivyo ni wazi tutakuwa bora,” alisema.
“Timu yetu ina vipaji vingi vikubwa na usajili umezingatia nafasi, hivyo kusajiliwa kwenye mfumo kwa wachezaji tuliowakosa mwanzo wa msimu na kuungana nasi kwenye uwanja wa mazoezi ni kazi kwa kocha kuamua nani aanze na nani amsubiri mwingine benchi, lakini ninachoweza kusema timu ipo imara na tayari kwa ushindani.”
Kulandana alisema tayari wameanza kuonyesha ushindani kwa kupata ushindi wa kwanza kwenye uwanja wao wa nyumbani wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC, matokeo ambayo anasema yamerudisha morali na matumaini ya kufanya vizuri mechi ijayo dhidi ya Pamba Jiji itakayofanyika Novemba 23 mwaka huu.
“Tutakuwa ugenini Novemba 23, hautakuwa mchezo rahisi kutokana na aina ya mpinzani tunayetarajia kukutana naye, lakini kama wachezaji tupo tayari kupambania pointi tatu muhimu na kikosi kina morali nzuri na ushindani wa kutosha,” alisema.