JKT Queens kazi inaanza leo CAF

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara, JKT Queens leo watakuwa katika Uwanja wa Suez Canal uliopo Ismailia, Misri kuianza safari ya ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika Wanawake dhidi ya Gaborone United ya Botswana.

Katika hatua ya makundi ya michuano hiyo, JKT Queens imepangwa Kundi B itaanza kucheza dhidi ya Gaborone kisha Novemba 12, 2025 dhidi ya Asec Mimosas na kumaliza makundi Novemba 15, 2025 itakapokabiliana na TP Mazembe.

Hiyo ni mara ya kwanza timu hizo zinakutana, huku JKT Queens ikishiriki michuano hiyo kwa mara ya pili baada ya 2023 kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi A.

Kwa upande wa Gaborone ni mara ya kwanza kucheza mashindano hayo ikichukua nafasi ya mabingwa mara mbili wa CAF, Mamelodi Sundown ambao waliondolewa hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Cosafa wakati wa kufuzu.

Akizungumzia mechi hiyo, Kocha wa JKT Queens, Abdallah Kessy alisema wamefanya tathmini kubwa dhidi ya wapinzani wao kuanzia ubora na udhaifu, na vyote watavitumia ili kuhakikisha wanapata ushindi.

“Mara ya mwisho hatukufanya vizuri. Tumewafanyia tathmini wapinzani wetu ubora na udhaifu wao, mashindano haya kila timu imejipanga kuonyesha ushindani, sisi pia tuko hapa kuwania taji hilo na tunaanza kazi hiyo ingawa tunajua sio mechi rahisi.”

Kipa wa JKT Queens, Najat Abbas alisema kuwa safari yao hadi kufikia hatua hiyo si ya bahati mbaya, hivyo wana kibarua cha kupata matokeo mazuri ili wajiweke kwenye nafasi nzuri kwenye kundi.

“Tumejiandaa vizuri, kila mchezaji anajua tunachokitaka, tunataka kurudi na taji lakini kwanza lazima tupate ushindi kesho (leo) na tufanye vizuri hatua ya makundi, hivyo ni lazima tujitolee, tupambane na tuoneshe nidhamu ya ushindani,” alisema.

Mashindano hayo yameanza jana kwa mechi mbili za Kundi A ambapo 15 de Agosto ya Angola dhidi ya USFAS Bamako kutoka Mali, FC Masar ya Misri wanaokipiga Watanzania wawili, Hasnath Ubamba na Violeth Nickolaus dhidi ya FAR Rabat ya Morocco.

Tamati ya michuano hiyo inayoshirikisha timu nane ni Novemba 21, 2025, huku bingwa akivuna kiasi cha Dola 600,000 (Sh1.5 bilioni za Tanzania).

Mbali na fedha hizo, mshindi wa mwaka huu atapata tiketi ya moja kwa moja kushiriki katika Kombe la Mabingwa la Dunia kwa Wanawake (Fifa Women’s Champions Cup) litakalofanyika mwaka 2026.