Hofu ya Mungu inavyosaidia kudumisha upendo na amani katika familia

(Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo, kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona (1 yohana 4:20)

Katika Somo lililopita nilifundisha “Namna ya kurejesha hofu ya Mungu Katika familia”. Miongoni mwa vitu nilivyo vizungumzia ilikuwa ni pamoja na kuwa na Upendo (kuheshimiana na kujaliana).

Katika somo hili nitafundisha “Namna hofu ya Mungu inavyosaidia kudumisha upendo na amani katika ndoa na familia”. Kuna wakati wanandoa wanaweza kupitia changamoto kiasi ambacho elimu na fedha walizo nazo zinaweza zisiwe na msaada wowote wa kuwavusha walipokwama isipokuwa Neema ya Mungu pekee.

Mara nyingi hofu ya Mungu inapotoweka ndani ya moyo wa mwanandoa, upendo na amani hutoweka na kusababisha majeraha ya nafsi, yanayopelea mpasuko mkubwa katika familia na jamii kwa ujumla.

Upendo ni hisia za ndani za huruma, kujali, kuthamini na kujitoa kwa ajili ya wengine (Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake (Yohana 15:13).

Ni muunganiko rasmi kati ya mwanamume na mwanamke unaokubaliwa kidini, kijamii, kisheria unaolenga kuishi pamoja kwa upendo, uaminifu, kusaidiana na kuanzisha familia (Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambanata na mkewe nao watakuwa mwili mmoja Mwanzo 2:24)

Katika somo lililopita nilisema familia ni kundi la watu waliounganishwa kwa damu, ndoa au uhusiano wa kiroho na wanaishi pamoja na kushirikiana kwa upendo na kuwajibika. Familia ni shule ya kwanza au msingi wa maisha ambapo mtu anawweza kujifunza kupenda, kusamehe, kuheshimu watu na kumcha Mungu.

 Ukiono jambo lolote zuri kutoka kwa mtu, mara nyingi chanzo chake huwa ni familia aliyotokea, vilevile ukiona jambo lolote lisilo zuri huwa mara nyingi chanzo chake ni familia aliyotokea japo wakati mwingine tabia inaweza kuathiriwa na mazingira.

Namna hofu ya Mungu inavyosaidia kudumisha upendo na amani katika ndoa na familia

1Wakorinto 13:4-7 inasema Upendo huvumilia, hufadhili, hauhusudu, hautakabari, haujivuni, haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake,hauoni uchungu, hauhesabu mabaya, haufurahii udhalimu, hutumaini yote hustahimili yote.

Neno upendo mara nyingi limekuwa likitamkwa kirahisi sana ukulinganisha na uzito lililobeba. Ni rahisi kusikia mtu akisema nakupenda/Nawapenda lakini baada ya muda anasema sihisi kuendelea kumpenda huyu mtu. Kupenda si kazi rahisi ndiyo maana bila msaada wa Mungu ni ngumu kupenda.

Hofu ya Mungu katika ndoa na familia husaidia kuleta;

Uvumilivu (1Wakorinto13:4)

Uvumilivu ni tunda la Roho Mtakatifu ambalo hupatikana tu kwa kumcha Mungu. Kila mwanadamu anaukomo wa kuvumilia na anapofika ukomo wake huchoka kuendelea kuvumilia hivyo hofu ya Mungu humuongezea nguvu ya kuendelea kumvumilia mwezake.

Kwa mfano: Mtu aliye na hofu ya Mungu hatamwacha mwenzake anayempenda kirahisi bali ataendelea kutafuta suluhu kila siku huku akiendelea kuomba msaada wa mungu. Ndiyo maana hapo awali nilisema kupenda siyo kitu rahisi bila msaada wa Mungu.

Hofu ya Mungu huondoa majivuno (1Wakorinto13:4-5)

Nafsi ya mwanadamu hupenda kuonekana bora sana kuliko nafsi ya mtu mwingine. Sifa ya upendo ni kuithamini nafsi ya mtu mwingine. Hofu ya Mungu huondoa ubinafsi katika ndoa na familia. Huondoa tabia ya kusema hiki ni cha kwangu bali husema ni chetu, huondoa tabia ya kusema ni mimimi niliyefanya na kusema ni sisi tumefanya. Upendo haujivuni. Bila hofu ya Mungu mwanadamu hawezi kuacha kujivuna.

Hofu ya Mungu haihesabu mabaya (husamehe)/ (1 Wakorinto13:5-6)

Upendo hauhifadhi kumbukumbu ya mabaya yaliyofanywa na mwenzako kwa ajili ya kutumia baadaye au kutaka kulipiza kisasi. Hulka ya mwanadamu ni kutopenda kushindwa hivyo akifanyiwa kosa hutamani kulipa kisasi. Hofu ya Mungu huhimiza kusamehe. Ni kweli kuna makosa ambayo kibinadamu hayavumiliki ila neno la Mungu husema kama msipowasamehe watu makosa yao hata Baba yenu wa mbinguni hawezi kuwasamehe ninyi makosa yenu (Mathayo 6:14). Ni ngumu kusamehe kila siku bila msaada wa Mungu.

Upendo wa kweli hauoni kasoro” (1wakorinto13:6)

Upendo hautazami tu kasoro za mtu mwingine. Biblia inasema mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii (Mathayo 7:3). Ukiona unaona kasoro nyingi kwa mwenzako tafsiri yake kwako ni mara mbili au zaidi yake. Ni hofu ya Mungu pekee inayoweza kumfanya mtu aone kuwa ni wajibu wake kukamilisha mwenzake na si kumhukumu kwa kasoro alizo nazo.

Ndiyo maana kupenda siyo kitu rahisi kama mtu hana misingi imara ya kumpenda Mungu.

Upendo wa kweli hauoni uchungu” (1Wakorinto13:7)

Miongoni mwa vitu vinavyosababisha msongo wa mawazo, vidonda vya tumbo na magonjwa mengi ya ndani ni uchungu wa muda mrefu. Neno la Mungu linasema Moyo uliochangamka ni dawa nzuri bali roho iliyopondeka hukausha mifupa (Mithali 17:22). Watu wengi tumejikuta tukitembea na uchungu wa miaka kumi, ishiri au hata zaidi kwa sababu ya kuhisi kwamba sisi ndiyo tunaoonewa. Tunashindwa kutambua kuwa hata sisi tunawasababishia wenzetu uchungu na majeraha. Ni hofu ya Mungu pekee inayoweza kumsaidia mtu kuondoa uchungu moyoni na kuona uzuri ulio ndani ya mwenza wake.

Mtu akisema nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake ni mwongo kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona (1 Yohana 4:20). Ndoa familia na jamii zetu kwa ujumla zinapitia maumivu, uchungu mwingi na mpasuko ambao chanzo chake ni kukosa upendo.

Na kama tulivyojifunza hapo awali hakuna mtu anaweza kuwa na upendo wa kweli pasipokuwa na misingi thabiti ya hofu ya mungu.

Wengi wetu tunamtamka Mungu katika vinywa vyetu lakini mioyo yetu iko mbali naye. Tunahitaji kujitafakari sana juu ya mahusiano yetu na Mungu kama ni ya kweli au la.

               Wapenzi na mpendane kwakuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu naye anamjua Mungu (1 Yohana 4:7)

 Mchungaji Dk Ambwene  Kilungeja  anapatikana Kanisa la

Harvest Chapel International-Dodoma (Simu:0754257522