Namna ya kumsaidia mtoto aliyeshuhudia vurugu

Dar es Salaam. Katika jamii yetu ya sasa, matukio ya vurugu, milipuko ya mabomu, milio ya risasi au vitendo vya kikatili yamekuwa yakishuhudiwa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali.

Watu wazima huathirika kisaikolojia, sembuse watoto ambao bado akili zao hazijakomaa kuelewa kinachotokea.

Mtoto anaposhuhudia vurugu za kutisha, hisia zake hujeruhiwa na kama hatapatiwa msaada wa haraka, anaweza kukumbwa na msongo wa mawazo au hata kiwewe cha muda mrefu.

Hivyo katika hili, mzazi au mlezi anayo nafasi muhimu katika kumsaidia mtoto kupunguza athari hizo kabla hazijageuka kuwa tatizo kubwa. Wataalamu wanasema kwanza kabisa, mzazi anatakiwa kumsikiliza mtoto kwa umakini. Mara nyingi watoto huwa na hofu ya kuzungumzia walichokiona kwa kuhofia kukemewa au kuonekana wadhaifu.

Hivyo ni wajibu wa mzazi kumhakikishia mtoto wake kwamba yuko salama na anaweza kusema chochote bila kuogopa.

Kwa sababu kusikiliza kwa upole, tunaambiwa humsaidia mtoto kutoa hisia zilizojificha ndani yake, jambo linalopunguza msongo wa mawazo kwa kiasi kikubwa.

Lakini mzazi au mlezi anapaswa kuwa mfariji wa mtoto na kumpatia uhakika wa usalama. Baada ya matukio ya vurugu, watoto wengi huendelea kuishi kwa hofu kana kwamba tishio bado lipo. Mzazi ndiye anayeweza kusaidia usalama wa kihisia mtoto kwa kumwambia kuwa vurugu zimekwisha na sasa yuko salama.

Pia, ni muhimu mzazi kuhakikisha mazingira ya nyumbani ni tulivu, bila sauti za mabishano au mivutano, kwa sababu hali hiyo inaweza kumkumbusha mtoto tukio alilolishuhudia kwa macho ama kusikia kwa sauti.

Hivyo, wataalamu wa saikolojia tiba wanashauri mzazi ni vema ukazungumza na mwanao kwa lugha lugha rahisi, kumuelezea kilichotokea. Kwa sababu watoto hupenda kuelewa mambo kwa uwazi. Mzazi akijaribu kuficha ukweli, mtoto anaweza kujijengea tafsiri zake zenye hofu zaidi.

Kwa mfano, mzazi anaweza kusema:“Yalikuwa matukio mabaya ambayo yamesababisha watu kuumia, lakini sasa yamedhibitiwa na watu wenye mamlaka wanahakikisha hayajirudii.” Ufafanuzi wa namna hii unaweza kumsaidia mtoto uelewa na kutuliza hofu ya kurudia kwa matukio hayo.

Lakini pia tukumbuke kuwa baada ya vurugu, watoto wengi hupoteza ari ya kucheza, kusoma au kuzungumza. Kumshirikisha katika michezo midogo, kusoma vitabu vya hadithi zenye matumaini au kumshikisha kazi zote za nyumbani anazoweza kuzifanya, kunaweza kumsaidia kurudi katika hali ya kawaida polepole.

Na hata michezo ya kuchora, kuimba au kusimulia hadithi ni njia nzuri ya mtoto kueleza hisia bila maneno.

Ishara kama kukosa usingizi, kutetemeka, kukosa hamu ya kula, kutozungumza, au kuogopa kelele ndogo zinaweza kumaanisha bado ana msongo wa mawazo. Mzazi akiona dalili hizo, asisite kumpeleka kwa mtaalamu wa afya ya akili au mshauri wa kisaikolojia kwa ushauri zaidi.

Jambo jingine muhimu ni mzazi mwenyewe kuwa na utulivu wa kihisia. Watoto hujifunza kupitia mienendo ya wazazi wao. Ikiwa mzazi anaonyesha hofu, hasira au msongo, mtoto naye atachukua hali hiyo. Kwa hiyo, mzazi anatakiwa kujituliza kisaikolojia kwanza, ili aweze kumpa mtoto msaada wa kipekee bila kumzidishia hofu.

Aidha, ushirikiano wa kijamii na taasisi za dini au shule unaweza pia kusaidia. Walimu na viongozi wa dini mara nyingi ni watu wanaompenda mtoto na wanaweza kumtia moyo kupitia mafundisho, michezo au mazungumzo ya pamoja. Hali hii humfanya ajihisi kuwa sehemu ya jamii salama na yenye upendo.

Mzazi asipuuze maombi au imani ya kiroho kama chanzo cha faraja. Sala, mazungumzo ya imani, au kusoma maandiko ya kutia moyo vinaweza kumpa mtoto matumaini mapya ya maisha na kupunguza hofu ya ndani.

Kwa jumla, msaada wa mzazi kwa mtoto aliyeona vurugu siyo wa maneno pekee, bali ni mchakato wa kimatendo, kisaikolojia na kihisia. Mtoto akihisi anapendwa, anaeleweka na yuko salama, hupona haraka kutokana na athari za vurugu. Kila mzazi anapaswa kutambua kuwa mtoto anaposaidiwa mapema, ndivyo anavyopona haraka na kurudi katika maisha yenye furaha na utulivu.