Usiwajengee watoto mazingira kuja kuwalaumu

Canada. Ni wazazi wachache wanaofaidi matokeo mazuri ya malezi yao kwa watoto. 

Hali hii inachangiwa na mambo mengi, ikiwemo mabadiliko ya nyakati, mitazamo potofu, na wakati mwingine ujinga wa kimakusudi. 

Kila mzazi anatamani mtoto wake afanikiwe zaidi yake, lakini mara nyingi juhudi hizo huishia kuwaharibu watoto bila kukusudia. Dunia imebadilika, na wazazi wanapaswa kubadilika nayo.

Wazazi wengi wanaamini elimu bora ni sawa na shule ghali. Ni wachache wanaotofautisha kati ya elimu bora na bora elimu. 

Wengi hujipotezea fedha kwa kufuata majina ya shule au lugha za kufundishia badala ya ubora wa elimu yenyewe. Leo hii, shule nyingi za “English Medium” na “International” zimejaa, lakini matokeo yake si ya kuridhisha. 

Wanafunzi wengi wanaomaliza huko hawana stadi za maisha, hawamudu lugha wanazofundishwa, na hawatimizi matarajio ya wazazi.Wazazi wengi wanapeleka watoto shule za kimataifa bila kujua watoto hao wataishi maisha ya kitaifa, si kimataifa. 

Wanafundishwa mambo yasiyowahusu, ilhali mambo muhimu ya mazingira yao yanapuuzwa. Matokeo yake, tunazalisha kizazi kinachojua mengi ya mbali, lakini kisichoweza kujimudu nyumbani.

Mbali na elimu, wazazi wengi hujivunia kuandaa urithi wa mali kwa watoto wao. Wanajitahidi kujenga majumba, kununua mashamba, na kuhifadhi mali kwa gharama yoyote. 

Lakini je, wanawaandaa watoto hao kujimudu bila hizo mali? Historia inaonyesha, watoto wengi wanaorithi utajiri bila malezi sahihi huishia kuufuja, hata kuishia kugombana na kuuana kwa ajili yake. 

Wengi katika wazazi hawa hawakurithi chochote, lakini walijituma na kujenga maisha yao kwa bidii.

Ukweli ni kwamba, mtoto asiyefundishwa kujitegemea ni mzigo. Wazazi wanapaswa kujifunza kutoka kwa wanyama kama simba na chui. Wanyama hawa huwafundisha watoto wao uwindaji kwa vitendo. Huwaletea mawindo hai na kuwaacha wajifunze. Mwanzoni ni kazi ngumu na ya kuchukiza, lakini baadaye huwafanya wawe wawindaji hodari.

Swali ni je, ni wazazi wangapi wanaofundisha watoto wao namna walivyofanikiwa kufika walipo? Wengi wanawalegeza watoto, wakitarajia mafanikio yasiyo na msingi. 

Mwishowe, wanajikuta wakiwalaumu watoto kwa kushindwa, ilhali hawakuwapa maandalizi sahihi.

Suluhisho ni rahisi lakini linahitaji uelewa na uthubutu. Kwanza, wazazi wakubali kuwa dunia imebadilika, na hivyo nao wabadilike. 

Pili, watambue kuwa nyakati na mazingira ya watoto wao si sawa na ya zamani. Tatu, waache kuwaandalia maisha, bali waanze kuwaandaa watoto kwa maisha ya baadaye.

Nne, kabla ya kumpeleka mtoto shule, mzazi ajue aina ya shule, ubora wa elimu, na matarajio yake. Tano, kabla ya kumlaumu mtoto kwa kushindwa, mzazi ajitazame kwanza kuona kama hakuchangia katika kushindwa huko. Sita, waache mashindano yasiyo na maana  kama kuwapeleka watoto shule ghali kwa sababu jirani au ndugu naye kafanya hivyo.

Mara nyingi matangazo yanayovutia kuhusu shule hizo ni ya kupotosha.

Mwisho, wazazi waache kupoteza fedha na muda wa watoto kwa kuwaandaa visivyo, kisha kuwalalamikia matokeo. Badala yake, wajenge msingi wa maadili, bidii, na kujitegemea kwani ndio misingi ambayo haipitwi na nyakati.