Unaanzaje kuwa bahili kwa mwenza wako? 

Katika jamii nyingi za Kiafrika na duniani kwa ujumla, uhusiano wa ndoa unajengwa juu ya msingi wa upendo, mawasiliano, kusaidiana na kujali mahitaji ya kila mmoja. 

Hata hivyo, moja ya changamoto zinazozidi kuonekana ndani ya ndoa nyingi ni suala la ubahili kati ya wenza. Wakati mwingine, mtu anaweza kuwa bahili bila hata kujitambua, jambo linaloathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano wa kimapenzi na hata familia kwa ujumla.

Kwa mujibu wa wataalamu wa saikolojia ya ndoa, mtu bahili ni yule anayekwepa kutumia mali au pesa kwa ajili ya wengine, hata pale ambapo matumizi hayo ni ya msingi au ya lazima. Katika muktadha wa ndoa, ubahili humaanisha hali ya mwenza mmoja kushindwa au kukataa kutumia rasilimali zake kuwasaidia au kuwahudumia wengine katika familia, hususan mwenza wake.

Watu wengi hujua kuwa ubahili ni hali ya mtu kukataa kutoa pesa au mali, lakini kuna njia nyingi ambazo mtu anaweza kuwa bahili kwa mwenza wake bila hata yeye mwenyewe kutambua.Njia hizo ni:

Mosi, kutotoa fedha kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani. Mtu anaweza kuwa na kipato kizuri lakini akakwepa au kukataa kuchangia mahitaji ya chakula, kodi, au ada za watoto.

Pili, kukataa kusaidia mwenza kutimiza ndoto zake. Ikiwa mwenza wako ana ndoto ya kujiendeleza kielimu au kibiashara na una uwezo wa kumsaidia lakini unamnyima, hiyo ni aina ya ubahili wa kihisia na kifedha.

Tatu, kumwekea mwenza mipaka ya matumizi. Hii ni pale ambapo mtu anataka kuwa na udhibiti wa asilimia 100 ya mapato ya familia, huku akimnyima mwenza wake uhuru wa kutumia pesa kwa mahitaji binafsi.

Nne, kunyima zawadi au ishara za upendo zinazohitaji gharama. Hata kama si za gharama kubwa, zawadi ndogo ndogo ni muhimu katika kujenga mapenzi. Kukataa kutoa zawadi kwa sababu ya kupenda “kuokoa” fedha ni tabia ya ubahili.

Tano, kutoa misaada kwa watu wa nje lakini si kwa mwenza. Wengine huonekana wema sana kwa marafiki au familia za nje, lakini ndani ya nyumba hawatoi msaada wowote kwa wenza wao.

Ubahili ndani ya ndoa una madhara makubwa kwa uhusiano wa kimapenzi, ustawi wa familia, na hata afya ya akili ya mwenza, ikiwamo kuvunjika kwa mawasiliano na upendo.

Mara nyingi, mwenza ambaye anaona anapuuzwa au hapewi kile anachohitaji ili kuishi maisha ya kawaida, huanza kujenga hisia za kutengwa na kutojaliwa. Hii inaweza kusababisha migogoro ya mara kwa mara, kutoelewana, na hatimaye kupungua kwa mapenzi.

Ubahili unapoendelea kwa muda mrefu, mwenza anayeathirika huanza kupata msongo wa mawazo kwa sababu ya kuishi maisha yasiyo na usawa. Wanaweza kujihisi kama mzigo au kama hawathaminiwi ndani ya ndoa.

Wengi wamefikia hatua ya kuvunja ndoa kwa sababu ya mwenza kuwa bahili. Pale ambapo mtu anaona kuwa hawezi tena kuvumilia hali ya kunyimwa haki zake za msingi, huchukua uamuzi wa kuondoka ili kutafuta heshima na furaha kwingineko.

Pia, watoto wanaweza kuathirika moja kwa moja kutokana na hali ya kifedha isiyotosha nyumbani, hasa pale ambapo mzazi mmoja ana uwezo lakini anakataa kusaidia. Hali hii huathiri malezi, elimu, na hata afya ya watoto.

Wakati mwingine, mwenza ambaye hana msaada kutoka kwa mume au mke wake huonekana dhaifu au duni mbele ya jamii, jambo ambalo linaweza kuathiri hadhi yake kijamii na hata kiakili.

Kwa nini wenza huwa bahili?

Ingawa ubahili mara nyingi huchukuliwa kama tabia hasi, kuna sababu mbalimbali ambazo huweza kuchangia mtu kuwa na tabia hiyo, ukiwamo utaratibu wa malezi.

 Wengine walilelewa katika mazingira ya uhitaji mkubwa na hivyo wakajenga tabia ya kuogopa kutumia pesa kwa hofu ya kuishiwa.

Baadhi ya watu huhifadhi sana fedha kwa sababu wanaogopa matatizo ya baadaye kama magonjwa au ukosefu wa kazi.

Tamaa au ubinafsi wa hali ya juu. Wengine hufanya hivyo kwa sababu ya kutanguliza maslahi yao binafsi kuliko ya familia au mwenza wao.

Aidha, wataalamu wanaeleza kuwa baadhi ya watu wana matatizo ya kisaikolojia yanayowafanya washindwe kutumia fedha hata pale panapohitajika.