Wivu silaha inayoimarisha, kuharibu uhusiano

Katika kila uhusiano wa kimapenzi, kihisia au hata wa kirafiki, wivu ni hisia ambayo haiepukiki. Ni hisia ambayo mara nyingi huonekana kuwa hasi, lakini kwa kiwango fulani, inaweza kuwa kiashiria cha upendo na kujali.

Wivu ni mojawapo ya hisia zinazochanganya sana katika uhusiano: inaweza kukuza ukaribu kati ya wenza wawili, lakini pia inaweza kusababisha migogoro mikubwa, kuvunjika kwa uaminifu, hata kuleta mwisho wa uhusiano.

Swali muhimu ni, je, wivu ni mbaya kila wakati? Au kuna namna fulani ya wivu inayofaa katika uhusiano? Makala hii itachambua nafasi ya wivu katika kukuza na kuharibu uhusiano, pamoja na kutoa ushauri wa kuuweka katika kiwango cha afya.

Wivu ni hisia inayotokea mtu anapohisi tishio la kupoteza upendo, uhusiano au nafasi maalum katika maisha ya mtu mwingine, hasa mpenzi au mwenza. Hisia hii huambatana na hofu, mashaka, hasira au huzuni.

Wivu mara nyingi huibuka pale mtu anapohisi mpenzi wake anatoa au anaweza kutoa muda, upendo au uangalizi kwa mtu mwingine, kiasi cha kuhatarisha uhusiano uliopo.

Ni muhimu kutofautisha wivu na uchungu wa kuona mtu mwingine akifanikiwa au kuwa na kitu unachokitamani kwani hali hiyo huitwa husuda. Wivu huhusisha hofu ya kupoteza kile ulicho nacho, hasa katika muktadha wa uhusiano.

Simulizi za Donald na Rehema

Donald Jonson, mkazi wa Buhongwa jijini Mwanza ana ushuhuda wa namna wivu ulivyoimarisha ndoa yake.Anasimulia:

 “Nilijikuta naanza kumtembelea mke wangu mara kwa mara tena kwa kushtukiza kwenye eneo lake la kazi. Mke wangu ni mtoa huduma za kifedha ana kibanda chake mjini…nilikuja kubaini kuna wanaume wameanza kumzoea.

Wanamtania wakati mwingine wanamtumia ujumbe  nikaanza kuwa na wivu..hivyo nikawa naenda mara kwa mara nampeleka sehemu anakula chakula cha mchana, wakati mwingine namfuata kazini kwake  tunarudi wote nyumbani au siku za Jumamosi nashinda naye kazini kwake.”

Anaongeza: Ilifikia hatua wale wote walokuwa wameanza mazoea wakajua ni mke wa mtu na mume wake anampenda na kumlinda. Hivyo wivu wangu ulinisaidia kutibu tatizo la mke wangu kuzoewa ovyo lakini pia ulifanya uhusiano wetu uwe imara.”

Kwa upande wake, Rehema Yusuph, naye mkazi wa jijini Mwanza, ana simulizi tofauti. Kwake wivu ulikuwa sawa na subiri.

 “Wivu kwa mume wangu ulitaka kuvunja ndoa yetu…alikuwa hataki hata nizungumze na jirani awe mwanaume au mwanamke. Nikitoka hata kwenda dukani nikirudi ni maswali.

Yaani hata niende sehemu nirudi muda huo huo lazima aniambie mbona umechelewa kurudi yaani nilikuwa najitetea hadi ikafikia hatua nikawa naona ndoa chungu. Nikaanza kuhisi au yeye ndo ananisaliti ndio maana anaona na mimi ni kama yeye? “anaeleza.

Anaongeza: Ilifikia hatua nikawashirikisha wazazi. Nikamwambia mama yake na mama angu..wenyewe wakawaambia baba na baba wa mke wangu. Wakatuita kikao  akaeleza anakuwa hivyo Kwa sababu ananipenda sana.Kwa sasa kapunguza kuhoji hoji angalau napumua na najiona nipo huru.”

Mwanasaikolojia, Nasra Khalidi kutoka taasisi ya Akili Platform Tanzania inayojihusisha na afya ya akili, mazingira na haki za binadamu, anasema wivu ni asili ya binadamu isipokuwa ukizidi  ndio inakuwa changamoto.

Anasema kuna aina nyingi za wivu ukiwemo wa kihisia ambao hutokea pale mtu anapohisi mwenza wake ana hisia za kimapenzi na mtu mwingine.

“Aina nyingine ni wivu wa kimwili ambao mtu anahisi mwenza wake anashiriki kimapenzi na mtu mwingine tofauti na yeye, labda kwa kuambiwa au hisia zake tu zinavyompeleka.

“Wivu wa kijamii unaotokea pale mtu anapohisi mpenzi wake anawapa kipaumbele watu wengine kuliko anavyopewa yeye. Mfano anahisi mpenzi wake anatumia muda mwingi na watu wengine wakiwemo marafiki kuliko anavyotumia akiwa na yeye,” anasema.

Kwa kiwango fulani, wivu unaweza kuwa na mchango chanya katika uhusiano. Hii ni kwa sababu wivu huonyesha kujali

Mara nyingi, mpenzi anapoonyesha wivu kidogo, huashiria kuwa anathamini uhusiano wake na hapendi kuuona ukitishiwa. Inaweza kumfanya mwenza mwingine ajisikie kupendwa na kuthaminiwa.

Wivu unaweza kufungua milango ya mawasiliano. Wenza wanapojadili kuhusu kile kinachosababisha wivu, wanaweza kuelewa hisia za kila mmoja kwa undani zaidi na kujenga mawasiliano bora.

Kwa baadhi ya watu, wivu mdogo unaweza kuwa kichocheo cha kurejesha moto wa mapenzi. Mpenzi anapohisi tishio, anaweza kujitahidi zaidi kuonyesha upendo, kukumbatia, na kujali kwa dhati ili kulinda uhusiano wake.

Wivu unapozungumziwa kwa uwazi, husaidia wanandoa kuweka mipaka ya afya,  kujua kipi kinakubalika na kipi hakiwezi kuvumiliwa katika uhusiano.

Wivu unavyoharibu uhusiano

Pamoja na manufaa hayo madogo ya wivu wa kiwango cha chini, wivu wa kupitiliza ni sumu katika uhusiano. Unaweza kuharibu uaminifu, uhuru na hata afya ya akili ya wahusika. Haya ni baadhi ya madhara ya wivu mbaya:

Mwenza mwenye wivu mkubwa huanza kumdhibiti mwenzake akitaka kujua kila anakoenda, anayezungumza naye, au hata kumzuia kuwa na marafiki. Hali hii huondoa uhuru wa mtu binafsi na kuingilia maisha ya mwingine.

Wivu ukizidi, huzaa mashaka yasiyo na msingi. Kila tendo la mwenza linatafsiriwa kwa mtazamo wa usaliti au hila. Hili huua uaminifu na kuharibu misingi ya uhusiano wowote.

Wivu wa kupindukia husababisha ugomvi wa mara kwa mara. Mpenzi mmoja hujihisi kila mara kulazimika kujieleza au kujitetea, hali inayochosha kihisia.

Mwenza anayelengwa na wivu mkali anaweza kuishi kwa hofu na mashaka, akijizuia kuwa yeye halisi au kujieleza kwa uhuru, kwa kuhofia kulengwa au kushukiwa.

Katika hali mbaya zaidi, wivu huzaa manyanyaso ya kimwili, kihisia au hata kijinsia. Watu wengi wamejeruhiwa au hata kuuawa katika uhusiano unaoongozwa na wivu wa kupindukia.

Wivu sio hisia ya ajabu ni kawaida kwa binadamu. Lakini jinsi unavyoushughulikia ndio jambo la msingi. Hapa kuna ushauri wa kuufanya wivu uwe wa afya:

Jiulize, wivu unatoka wapi? Je, unatokana na mwenza wako kutokuwa mwaminifu? Au unatokana na hofu zako binafsi, uzoefu wa zamani au ukosefu wa kujiamini? Kutambua chanzo husaidia kujijibu kwa njia sahihi.

Usinyamaze au kulipuka kwa hasira unapohisi wivu. Zungumza na mwenza wako kwa upole, eleza unavyohisi bila lawama.

Mfano: “Najisikia wivu kidogo unapozungumza kwa ukaribu sana na fulani, naomba unisaidie kuelewa uhusiano wenu.”

Wivu mwingi huanzia kwenye ukosefu wa kujiamini. Jifunze kujipenda, kuthamini nafasi yako katika uhusiano na kutambua kuwa una thamani hata pasipo ushindani.

Kuchunguza simu, barua pepe au mitandao ya kijamii ya mwenza wako huongeza wasiwasi badala ya kuleta amani. Jifunze kumuamini mwenza wako hadi ithibitike tofauti.

Kila uhusiano unahitaji mipaka ya wazi. Muweke wazi kile ambacho kila mmoja anahisi ni sawa au si sawa, kama vile ukaribu wa kupitiliza na watu wengine, au mawasiliano ya muda usiofaa.

Iwapo wivu umekuwa wa kiwango kinachoathiri maisha yako au ya mwenza wako, tafuta ushauri wa kitaalamu. Mshauri wa ndoa au saikolojia anaweza kusaidia kuelewa hisia zako na kukuongoza.

Dini mbalimbali zinaeleza wazi kuhusu wivu na namna unavyopaswa kushughulikiwa, kwa kuzingatia maadili, heshima na uzingatiaji wa mipaka ya kiroho na kijamii. Ingawa dini zote zinatambua kuwa wivu ni hisia ya kibinadamu, nyingi zinaonya dhidi ya wivu wa kupindukia unaoleta madhara.

Katika Uislamu, wivu (ghirah) unagawanyika katika sehemu mbili: Ghirah ya halali (chanya): Ni wivu wa heshima na kujali heshima ya ndoa au mwenza. Mume au mke anaweza kuonyesha wivu wa kulinda uhalali wa ndoa, lakini bila kuvuka mipaka au kudhulumu.

Mtume Muhammad (Rehma na amani zimshukie) alihimiza wivu wa aina hii, akisema:

 “Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye wivu, na mja pia anaweza kuwa na wivu.” (Bukhari na Muslim).

Ghirah ya haramu (mbaya): Ni wivu wa mashaka, udhibiti kupita kiasi, au kudhania mabaya pasipo ushahidi. Wivu huu unakatazwa kwani huvunja uaminifu na kusababisha dhuluma.

Kwa upande wa Ukristo, Biblia inaonya dhidi ya wivu wa uharibifu. Katika Wagalatia 5:19-21, wivu umetajwa miongoni mwa “matendo ya mwili” yanayopingana na Roho Mtakatifu:

“Na dhahiri matendo ya mwili, ndiyo haya; uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira…”

Hata hivyo, Biblia pia inatambua wivu wa Mungu kama ishara ya upendo wake kwa watu wake akilinda uhusiano wa kiroho usiharibiwe. Katika ndoa, mume na mke wanahimizwa kujaliana kwa upendo, si kwa hofu au mashaka.

Kwa ujumla, dini hazikatazi wivu kwa jumla  bali zinahimiza udhibiti wa hisia hiyo ili isiharibu maadili, upendo, na amani ya moyo.

Wivu wa kujali na kulinda uhalali wa ndoa unaruhusiwa, lakini si ule wa mashaka, udhibiti au manyanyaso.

Mwenendo wa kiroho unapaswa kuongozwa na imani, mawasiliano, na heshima, si hofu au wivu usio na mipaka.

Ikumbukwe wivu ni silaha yenye ncha mbili katika uhusiano. Kwa upande mmoja, unaweza kuonyesha kujali na kuimarisha ukaribu kati ya wenza wawili. Kwa upande mwingine, unapopitiliza, unaweza kuwa sumu inayoangamiza kila kitu kilichojengwa. 

Kila mmoja anapaswa kujifunza kutambua wivu, kuutafakari na kuushughulikia kwa hekima. Uhusiano wa kudumu unahitaji uaminifu, mawasiliano na uhuru wa kihisia. 

Wivu, unapodhibitiwa vyema, unaweza kuwa mlinzi wa upendo. Lakini ukiachiwa uhuru kupita kiasi, unaweza kuwa mvunjaji wa amani.