WAKATI ikielezwa Simba imeshaanza mchakato wa kusaka mbadala wa kipa Moussa Camara anayetarajiwa kufanyiwa upasuaji wa goti, eneo la beki wa kati kikosini hapo ni uhakika huku majembe matano yakiipa jeuri kikosi hicho cha Dimitar Pantev.
Ipo hivi; Simba inapitia changamoto ya kuuguza wachezaji wenye majeraha wawili, kipa namba moja wa kikosi hicho, Camara na beki wa kati, Abdulrazack Hamza ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti.
Hamza aliumia kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii Septemba 16, mwaka huu dhidi ya Yanga na hakumaliza mechi hiyo ambayo Simba ilichapwa bao 1-0.
Chanzo cha kuaminika kutoka Simba, kimeiambia Mwanaspoti licha ya kukosekana kwa Hamza kwenye mechi za ligi hata kimataifa kutokana na kuuguza jeraha lake, uongozi wa timu hiyo hauna mpango wa kurudi sokoni kuziba nafasi yake.
“Ni kweli kuna mchakato wa kutafuta kipa wa kurithi mikoba ya Camara kipindi akiugua lakini eneo la beki wa kati halina presha kwani tuna mabeki wengi ambao wanaendelea kufanya kazi nzuri.
“Simba ina Chamou Karaboue, pia Naby Camara mwenye uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya sita uwanjani ikiwemo kwenye ulinzi. Kuna Rushine De Reuck, Vedastus Masinde na Wilson Nangu wanaocheza mabeki wa kati, hivyo hatuna sababu ya kurudi sokoni,” kimesema chanzo hicho.
Chanzo hicho kimesema usajili uliofanywa eneo hilo ulizingatia mambo mengi, hawakutaka kurudia makosa ya kuwa na idadi ndogo kwenye eneo hilo na akikosekana mchezaji mmoja wanakuwa na presha, hivyo wanaamini katika ubora wa wachezaji wote waliopo wataweza kusaidia kipindi hiki ambacho Hamza anaugua.
Kwa upande wa Camara, alipata changamoto ya goti mechi dhidi ya Gaborone United iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 na alifanyiwa mabadiliko, akaingia Yakoub Suleiman aliyetua Simba msimu huu akitokea JKT Tanzania.
Inaelezwa tayari amefanyiwa vipimo vya awali na majibu kuonyesha ana tatizo kubwa kwenye goti ambalo litamfanya akae nje kwa muda.
Msimu uliopita, Camara ndiye aliyeibuka kinara upande wa makipa waliocheza mechi nyingi bila ya kuruhusu bao na zilikuwa 19 kati ya 28 alizokaa langoni.
Tayari inaelezwa uongozi wa timu hiyo umeanza kuwafuatilia makipa wawili wa timu ya taifa ya Uganda ili mmoja wapo kurithi mikoba ya Camara.
Makipa wawili ambao wapo kwenye rada za Simba na huenda mmoja wapo akasajiliwa dirisha dogo la usajili Desemba 15 mwaka huu ni Joel Mutokubwa anayecheza katika timu ya BUL Jinja na Alionzi Nafian wa Mechal SC.