KIUNGO wa Songea United, Gilbert Boniface, amesema kwa sasa ni wakati wa kuonyesha makali yake ndani ya timu hiyo msimu huu, baada ya kipindi kigumu akiichezea Cosmopolitan iliyoshuka daraja ikitokea Ligi ya Championship hadi First League.
Cosmopolitan ilishuka daraja baada ya kupoteza mechi 20 kati ya 30, ikishinda tano na sare tano msimu uliopita, ikimaliza katika nafasi ya 15 kwa pointi 20 na kuungana na ‘Wanajeshi wa Mpakani’ Biashara United iliyoburuza mkiani kwa pointi zake 16.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gilbert amesema anaamini msimu huu utakuwa ni mzuri kwa timu hiyo kutokana na kuwa na wachezaji bora na benchi la ufundi bora, licha ya kukiri pia ushindani ni mkubwa na umeanza mapema hususani kwa zile mechi za ugenini.
“Bado ni mapema, lakini kuna kitu nakiona katika timu kwa sababu hapa ni mgeni na ninahitaji muda wa kuzoeana na wenzangu na kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza, naamini kwa umoja na mshikamano wetu msimu huu tutafanya vizuri,” amesema.
United inayofundishwa na kocha Abdul Mingange, kabla ya pambano la jana Jumapili ugenini dhidi ya kikosi cha Mbuni cha jijini Arusha, ilicheza mechi tatu msimu huu na kati ya hizo ilishinda moja tu, ikitoka sare moja na kupoteza pia moja.