MSHAMBULIAJI Said Khamis ‘Said Jr’ anayeitumikia IFC Malaysia amesema anatamani kuandika rekodi akiwa na kikosi hicho kwa kufunga zaidi ya mabao 20.
Said Jr alikuwa nje ya uwanja kwa takribani nusu msimu na alijiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Malaysia marufu Liga Super Malaysia akitokea FK Jedinstvo UB ya Serbia aliyoitumikia kwa msimu mmoja wa 2023/24.
Akizungumza na Mwanaspoti, Said Jr amesema baada ya kukaa muda mrefu nje ya uwanja anatamani kuandika rekodi akiwa na kikosi hicho na kuisaidia kufanya vizuri kwenye ligi ya Malaysia.
Aliongeza haikuwa rahisi kwake kuanza ligi vizuri hasa Malaysia ambayo asilimia kubwa ya mpira wa nchi hiyo unatumia nguvu na kama haufanyi jitihada binafsi unaweza kukosa nafasi ya kucheza.
“Nashukuru Mungu, unajua hii ni kazi kama kazi nyingine, tofauti ni kwamba hii unaweza kukaa muda mrefu nje, lakini bado ukaendelea kujikimu kwa kutumia pesa uliyopata wakati unacheza (kwa sababu katika soka kipato kinakuwa ni kikubwa kiasi). Pia nashukuru kusajiliwa tu na kuanza kuaminiwa,” amesema Said Jr na kuongeza;
“Malengo kwanza ni kuisaidia timu kisha mimi mwenyewe natamani kuweka rekodi huku nifunge kila ninapata nafasi na kama nitafanikiwa zaidi basi nichukue kiatu cha mfungaji bora.”
Hadi sasa Said Jr amefunga mabao manane kwenye mechi tisa alizocheza, chama lake likiwa na pointi sita katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi hiyo.