Chama la Wana lakumbwa na ukata

TIMU ya Stand United ‘Chama la Wana’, imeanza kukabiliwa na ukata mapema tu baada ya baadhi ya wafadhili wa kikosi hicho kudaiwa kujiweka kando kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri tangu msimu uliopita iliposhindwa kupanda Ligi Kuu Bara.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo iliyochapwa mechi tatu mfululizo za Ligi ya Championship msimu huu, zinaeleza mmoja wa wafadhili wa kikosi hicho amejitenga kwa sababu ya maelewano mabovu, jambo linaloashiria hali ya hatari huko mbele.

“Ni kweli hali hiyo ipo na inachangia mwenendo wetu wa sasa kwa sababu ya hiki kinachoendelea, tunaamini mambo yatakaa sawa huko mbele ingawa jitihada za mapema zinahitajika kuchukuliwa ili kuepuka aibu,” kilisema chanzo cha timu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Stand United, Fredy Masai, licha ya kutotaka pia kuweka wazi suala hilo, ila alikiri ni kweli kuna mambo hayajakaa sawa ya uongozi, japo kuna hatua za haraka zinaendelea kuchukuliwa kikosini humo.

Msimu uliopita, Stand ilimaliza ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 61, ambapo ilicheza ‘playoffs’ za kupanda Ligi Kuu Bara, ikianza kwa kuiondosha Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56, katika Ligi ya Championship kwa jumla ya mabao 4-2.

Baada ya Stand kuitoa Geita Gold, ikacheza ‘playoffs’ nyingine dhidi ya Fountain Gate iliyotolewa pia hatua hiyo na maafande wa Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-2, ambapo kikosi hicho kilikwama kupanda baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-1.