Mama asimulia ndoto za bintiye ‘Tina’ zilivyozimwa kwa risasi

Dar es Salaam. Machozi, ukimya na simanzi vimetanda katika familia ya Christina John Richard, maarufu Tina, msichana aliyekuwa dereva wa malori ya mizigo ya masafa marefu, aliyeuawa kwa risasi Oktoba 30 baada ya vurugu za maandamano yaliyotikisa maeneo kadhaa nchini.

Tina (22), alikuwa dereva wa kampuni ya usafirishaji mizigo ya Super Star Forwarded, akihudumu kama dereva wa masafa marefu kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi nchi jirani za Zambia na Malawi.

Aliwavutia wasichana wengi alipoweka picha mjongeo katika kurasa zake za mitandao ya kijamii ya Instagram na TikTok, zikimwonesha akijiandaa kuanza safari, akiwa safarini, akibadili matairi ya magari njiani, na kazi zake kwa ujumla.


Binti huyo aliyezikwa katika kijiji cha Ngulimi Bolenga, Nyamongo, Wilaya ya Serengeti, Novemba 6, 2025, alianza kufahamika kwa ujasiri na bidii yake katika kazi za ufundi wa magari akiwa na umri wa miaka 17, na baadaye kuwa dereva akiwa na umri wa miaka 19, kazi ambayo mara nyingi imekuwa ikitawaliwa na wanaume.

Mama yake mzazi, Osilo Zedekia Omumbo, amezungumza na Mwananchi kwa njia ya simu na kusimulia hatua kwa hatua za ukuaji wa binti yake, ndoto alizoanza kuitimizia familia, malengo aliyokuwa nayo, na jinsi umauti ulivyomfika.

“Alikuwa tegemeo la familia. Baba yake alifariki akiwa mdogo, akakatiza masomo na kujikita katika ufundi ili akomboe familia. Ndoto zetu zimezimika kwa risasi,” anaanza kusimulia.

Anasema binti yake alizaliwa Novemba 27, 2002 na kuhitimu darasa la saba katika Shule ya Msingi Yogelo iliyopo wilayani Sengerema mkoani Mwanza. Licha ya kufaulu vizuri, alikataa kuendelea na masomo kutokana na hali ya uchumi wa familia.

“Baba yake alifariki akiwa mdogo sana. Alipomaliza shule aliniambia, ‘Mama, naishia hapa, hutaweza hata kununua sare za shule. Siendi sekondari, naona inanichelewesha kwenye ndoto zangu. Nataka kwenda gereji nijifunze ufundi wa magari.’” anasimulia.

Osilo anasema neno lililorudiwa kinywani mwa bintiye lilikuwa ni kukosa mtoto wa kiume mkubwa katika familia, hivyo alimuahidi kusimama kama kiongozi wa familia. Alikuwa tegemeo lao na alifanikiwa kununua nyumba ya familia huko Sengerema na baadhi ya mali.


Anasema alianza rasmi kujifunza ufundi magari katika mojawapo ya gereji akiwa Sengerema, Mwanza, mwaka 2018.

“Baada ya kujifunza makenika, akaniaga, ‘Mama, ngoja niende Dar kutafuta.’ Akaondoka mwaka 2022, akaniambia, ‘Mama, naomba nimlete mtoto, naona ananibana sana na shughuli zangu, nashindwa kuzifanya vizuri.’

“Mwaka jana Septemba akaniita nikaenda Dar. Aliniambia, ‘ninafanya kazi kwa ajili yako na Safina (mwanaye), na sasa nimeshapata ajira kwenye kampuni mpya.’ Alinitafutia nyumba nikawa naishi Kibaha, yeye akatafuta chumba Chamazi ili awe karibu na kazini,” anasema.

Osilo anasema binti yake ameacha mtoto mmoja wa miaka mitano na alikuwa na malengo ya kumfundisha kazi mdogo wake wa kiume aitwaye Isaka. “Wiki iliyopita niliongea naye, akaniambia, ‘Wiki ijayo nitakuja nimpeleke Isaka gereji, kazi ya Mungu huwezi kuizuia.’”

Anasema binti yake alianza kuendesha magari makubwa mwaka 2023, na amefanya kazi katika kampuni tatu tofauti kwa kipindi hicho chote. Desemba mwaka jana, aliajiriwa katika kampuni ya Super Star.


Osilo anasema mara ya mwisho kuwasiliana na bintiye ilikuwa Oktoba 29, saa 8 mchana.

“Alinipigia akaniita kama kawaida yake, ‘Kipenzi, salama?’ Nikamjibu tukaongea. Akasema, ‘Mimi bado niko ndani, nimelala huku hali siyo nzuri. Ikiwa nzuri nitatoka nikurushie hela.’ Lakini alikuwa anapiga sana miayo, nikamuuliza kulikoni, akasema ameshinda amelala.

“Akanikumbusha kuhusu banda la kuku, akasema angenitumia hela. Kesho yake asubuhi saa 4 dada yake akanipigia simu, ‘Mama, Tina amepigwa risasi!’ Nikaanza kupiga yowe, watu wakajwa wamejaa pale nyumbani.

“Baadaye akaulizwa, ‘Umezipata wapi taarifa?’ Akasema, ‘Nimepigiwa na mtu aliyeokota simu akisema mwenye simu amepigwa risasi na amefariki hapohapo,’” anasema.


Anasema walifanikiwa kupata taarifa hiyo kwani aliyeokota simu haikuwa na nywila, ndipo akatafuta jina la dada na kumpa taarifa.

Kwa mujibu wa Osilo, Oktoba 30 asubuhi Tina alikwenda kazini, wakawa wamerudishwa. Walivyoondoka na mwenzake, walipofika Tazara alimshusha kwenye bodaboda, akawa anasubiri basi aelekee Chamazi, ndipo alipigwa risasi akiwa kituo cha daladala.

Anaiishukuru kampuni aliyokuwa akifanya kazi bintiye kwa kufanikisha kupata mwili, kuusafirisha, na kuuhifadhi katika nyumba yake ya milele katika kijiji cha Ngulimi Bolenga, Nyamongo, Wilaya ya Serengeti.

Osilo, mama wa watoto sita, anasema Tina alikuwa mtoto wa tatu kuzaliwa, na sasa amebaki na watoto watano.