Minziro afichua kinachoisibu Bigman | Mwanaspoti

KOCHA Mkuu wa Bigman, Fredy Felix ‘Minziro’, amesema sababu ya kuanza vibaya msimu huu kwa kikosi hicho ni kutokana na maandalizi mabovu ya mwanzoni mwa msimu (pre-season), ingawa viwango vya wachezaji kiujumla vinampa matumaini makubwa.

Minziro amezungumza hayo baada ya kikosi hicho kuchapwa mechi tatu mfululizo, ikichapwa bao 1-0, dhidi ya TMA na Kagera Sugar, kisha mabao 2-0 mbele ya Mbuni, huku jana Jumapili ikicheza ugenini na Barberian ambayo zamani ni Kiluvya United.

“Ni kweli mwenendo wetu sio mzuri kwa sababu tumepoteza mechi tatu mfululizo, tulichelewa sana kufanya maandalizi yetu ya msimu, ila kwa kuangalia kiwango cha mchezaji mmoja mmoja kinanipa matumaini mbele,” amesema Minziro.

Minziro aliyewahi kuzifundisha Geita Gold na Tanzania Prisons, aliifundisha Bigman msimu wa 2024-2025, ingawa aliondoka Oktoba 17, 2024 na kujiunga na Pamba Jiji, akichukua nafasi ya Mserbia Goran Kopunovic aliyeondoka pia Oktoba 16, 2024.

Baada ya kuondoka Minziro, timu hiyo ikafundishwa na Zubery Katwila aliyejiunga na Geita Gold msimu huu, ambapo kocha huyo kwa msimu wa 2024-2025, aliiwezesha Bigman kumaliza katika nafasi ya nane katika Ligi ya Championship ikiwa na pointi zake 47.