BAADA ya kukosa uhondo wa Ligi Kuu Bara, huenda mashabiki wa soka jijini Mbeya wakaanza kushuhudia timu zao Mbeya City, Tanzania Prisons pindi ligi hiyo itakapoendelea baada ya uwanja wa Sokoine kufanyiwa maboresho.
Pamoja na uongozi wa uwanja huo kuthibitisha kukamilika maboresho yake, inasubiriwa uamuzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ambao wanatarajia kufika leo kwa ukaguzi.
Uwanja wa Sokoine ulifungwa Oktoba 15, 2025 baada ya kubainika kukosa sifa kwenye eneo la kuchezea ‘pitch’ ikiwa ni siku chache baada ya mechi ya Ligi Kuu kati ya Mbeya City dhidi ya Yanga iliyomalizika bila kufungana.
Kufuatia kifungo hicho, Mbeya City ilihamishia mechi zake za nyumbani kwenye Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam ikicheza dhidi ya JKT Tanzania na Tanzania Prisons, huku ndugu zao Tanzania Prisons wakitangaza kuhamishia makazi Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ilhali KenGold ya Championship ikitimkia wilayani Chunya.
Akizungumza leo Novemba 9, 2025, meneja wa uwanja huo, Modestus Mwaluka amesema baada ya kufungwa, walipokea maelekezo na kuanza kufanyia utekelezaji na kwa sasa ukarabati umekamilika.
Amesema kinachosubiriwa ni wakaguzi kutoka mamlaka za mpira wa miguu hapa nchini TFF na TPLB ambazo zinatarajia kufika kwa ajili ya kujiridhisha na kutoa maelekezo, akitoa matumaini kuwa kazi iliyofanyika mashabiki wasubiri kupata raha.
“Niwashukuru wamiliki wa uwanja (CCM) ambao tangu taarifa za mamlaka ya soka walipokea maelekezo na kutoa sapoti lakini pia wapo wadau waliosapoti kwa kiasi kikubwa na hadi sasa uwanja upo tayari kwa matumizi,” amesema Mwaluka.
Akizungumzia taarifa hiyo, Ofisa Habari wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota amesema ni faraja kwao kama wanufaika wa uwanja huo akieleza kuwa gharama walizotumia nje ya Sokoine zingetumika sehemu nyingine.
“Lakini hata mashabiki walikosa burudani ya timu yao, tuombe uwepo uamuzi mzuri turudi nyumbani, hadi sasa timu inaendelea na maandalizi kwa mechi ijayo ugenini dhidi ya Mashujaa Novemba 22, kisha kuwaleta Namungo,” amesema Mwankota.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Prisons, Godfrey Madegwa amesema kwa sasa wanasubiri uthibitisho wa mamlaka za mpira wa miguu nchini ambapo wakikubaliana, watarejesha mechi zao Sokoine.
“Tukipata taarifa rasmi tutatoa uelekeo wa mechi zetu kwakuwa tunatarajia kucheza dhidi ya Yanga na Simba nyumbani, hivyo kwa sasa tunasubiri TFF na Bodi ya Ligi” amesema Inspekta huyo.