Gamondi alia na mastraika Singida Black Stars

KOCHA wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi ameigeukia timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ inayojiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya Kuwait huko Cairo Misri, akitoka kulazimishwa sare ya 1-1 na Pamba Jiji, huku akilia na straika kumuangusha kutoka na ushindi CCM Kirumba.

Gamondi aliyeteuliwa Taifa Stars kuchukua nafasi ya Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema sare dhidi ya Pamba ilitokana na washambuliaji wa Singida kushindwa kutengeneza na kutumia nafasi mbele ya lango la wenyeji.

Timu hizo zilitoka sare hiyo juzi katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Kirumba na kuzifanya zigawane pointi moja moja, Pamba ikifikisha tisa wakati Singida ikifikisha saba zikitofautiana idadi ya mechi ilizocheza.

Singida ilicheza mechi tatu, ikifunga mabao matatu ikiwa na wastani wa bao moja kila mechi, ikiifunga Mashujaa na KMC kila moja kwa bao 1-0 kabla ya sare ya juzi, huku kocha Gamondi amesema tatizo ni mastaa wa timu hiyo kushindwa kutengeneza nafasi.

GAMO 01


Akizungumza jijini Mwanza, Gamondi amesema licha ya changamoto za uwanja katika mchezo huo, lakini kikosi chake kilishindwa kutengeneza nafasi za mabao tofauti na nafasi ya bao lililofungwa na Clatous Chama dakika ya 32 kwa faulo ya kutengwa.

“Kiukweli tunahitaji kutengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini hiki sio kisingizio kwa sababu hata uwanja umetunyima fursa ya kucheza mpira mzuri ambao huenda ungetupatia matokeo mazuri,” amesema Gamondi na kuongeza;

“Ili ushinde mechi unahitaji kutengeneza nafasi, wenzetu walikuwa imara wamelinda vyema na walikuwa wagumu, wakipiga mipira mirefu, hawakuwa na nafasi ya kufanya makosa, na huu ndiyo mpira.”

Amesema pamoja na tatizo hilo, lakini anaridhishwa na matokeo ya timu yake kwani katika mechi 12 za mashindano yote msimu huu wameshinda tisa na sare tatu, kwani kucheza ugenini ni ngumu na vitu vingi hutokea, ambapo wanahitaji kuendelea kufanya kazi ili kuwa bora zaidi.

GAMO 02


Kocha huyo raia wa Argentina, pia aliulalamikia Uwanja wa Kirumba kwa kukosa ubora akidai umesababisha Singida ishindwe kucheza soka tamu na kutumia mbinu zao.

“Kwangu ni vigumu kuwa na mechi nzuri hapa katika uwanja huu, timu moja inalinda na kupiga mipira mirefu hii ni tofauti kabisa na mtindo wetu na inaondoa mpira mzuri,”  amesema Gamondi na kuongeza;

“Hatujafurahishwa na matokeo haya kwa sababu tumekuja hapa kupata ushindi na sababu ya hili ni uwanja. Ni jambo zuri kucheza hapa ni uwanja mkubwa lakini nyasi zake siyo nzuri na kulikuwa na matukio ambayo hayakuwa upande wetu katika mchezo.