SIMBA imeendelea na kasi yake ya ushindi wa asilimia mia moja katika Ligi Kuu Bara baada ya jana Jumamosi Novemba 8, 2025 kuilaza JKT Tanzania katika mechi iliyokuwa kama kushinda vita kutokana na ugumu ilioupata kutoka kwa wenyeji ambao hata hivyo wamekuwa hawana rekodi tamu kwa Wekundu hao.
Ushindi huo wa mabao 2-1 ambao Simba iliupata ikitokea nyuma baada ya kutanguliwa kwa bao la kushtukiza dakika ya 60, uliipeleka timu hiyo hadi kileleni mwa msimamo ikifikia pointi tisa kutokana na mechi tatu ilizocheza, ikilingana na Pamba Jiji iliyoongoza kwa muda baada ya kutoka sare ya 1-1 na Singida Black Stars.
Simba imekuwa timu pekee hadi sasa katika Ligi Kuu msimu huu kushinda mechi tatu mfululizo, licha ya kuwa kati ya zilizoruhusu bao tofauti na ilivyokuwa awali ikiwa moja ya timu zilizokuwa hazijafungwa bao lolote kutokana na kushinda mechi mbili za kwanza kwa 3-0 kila moja.
Pointi hizo tatu, zilihakikishwa na mshambuliaji, Jonathan Sowah aliyeingia uwanjani dakika ya 60 kuchukua nafasi ya Steven Mukwala, akatumia dakika 16 pekee kufanikisha Simba kuwa timu pekee iliyoshinda mechi zote msimu huu katika ligi hiyo.
Sowah aliingia wakati JKT Tanzania imetoka kufunga bao kupitia Edward Songo, kisha Wilson Nangu akasawazisha dakika ya 64, kisha Sowah akafunga dakika ya 76.
Meneja wa Simba, Dimitar Pantev jana alikuwa na dakika 90 za kwanza katika Ligi Kuu Bara, tangu apewe kazi ya kuinoa timu hiyo kutoka kwa Fadlu Davids.
Katika mechi zilizopita, Simba ilikuwa chini ya Seleman Matola, ambaye kwenye makaratasi ndiye kocha mkuu kutokana na Pantev kutokidhi vigezo kikanuni kusomeka kama kocha mkuu.
Hata hivyo, Simba ilionyesha ukubwa wake, ikicheza vizuri na kutawala mchezo huo kwa dakika zote 90 mbele ya JKT na kuendeleza rekodi tamu iliyonayo mbele ya maafande hao kwani msimu uliopita iliipiga nje ndani kwa ushindi wa bao 1-0 kila mechi.
Kitu kikubwa ambacho JKT ilikuwa imekitumia kuwatuliza Simba ni kuwachezea soka la kutumia nguvu nyingi ambapo kipindi cha kwanza wanajeshi hao walitengeneza faulo nyingi (sita) dhidi ya mbili za Simba.
Simba ilionekana kutohitaji mapambano hayo na badala yake iliamua kuweka mpira chini na kukwepa matumizi hayo makubwa ya nguvu.
Kuna muunganiko unakosekana kutoka eneo la kiungo washambuliaji na safu yake ya ushambuliaji ambapo bado hakuna utengenezwaji mwingi wa nafasi za wazi za kufunga ambapo jana ndani ya dakika 45 za kwanza nafasi kubwa ni ile ambayo Joshua Mutale alikaribia kufunga akiwa uso kwa uso na kipa wa JKT, Omar Gonzo lakini kipa huyo akacheza.
Hapa ndipo Pantev anatakiwa kuielekeza akili yake kwasasa ili kuhakikisha timu inaimarika zaidi.
Hili linajionyesha pia kwenye mechi zake mbili za mwisho za nyumbani Kwa Mkapa za Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo timu hiyo ilifunga bao moja tu tena la penalti.
Mabao yote matatu yalitokana na makosa ya maeneo ya ulinzi kukosa utulivu au kushindwa kuwa na hesabu sahihi za kuzima jaribio la wapinzani.
Akiangalia bao la JKT. Wakati wenyeji wakitengeneza shambulizi hilo kutoka wingi ya kulia na krosi inapigwa ndani inamkuta mfungaji Edward Songo alikuwa amesimama mwenyewe akiwa na utulivu na kuwafanya anachotaka mabeki wa wageni ambao walikuwa wachezaji sita dhidi ya wanne wa wanajeshi hao.
Pia mabao mawili ya Simba nayo hali ilikuwa hivyo hivyo beki Wilson Nangu wala hakuhitaji kuruka sana kucheza krosi ya Ellie Mpanzu zaidi ya kupiga tu kichwa akichagua wapi auweke mpira huku akiwa na beki pembeni aliyefanikiwa kushika mwili tu wa mfungaji.
Bao la pili la Simba, kosa lilifanyika pembeni kwa beki kuingiza mpira katikati ya uwanja bila kutambua kwamba ilikuwa n hatari kubwa. Morice Abraham akaunasa na kutumia kasi yake kuingia kwa nguvu ndani lakini pasi yake kwa mfungaji Sowah mabeki Paschal Mussa na Laurian Makame wanashindwa kuokoa mpira uliowapita chini ya miguu na kumkuta mfungaji.
Makosa yote hayo yatawapa kazi ya kufanya makocha wote Ahmed Ally na Pantev kwenda kujipanga upya kwani yalikuwa mabao ambayo yalitokana na umakini mdogo na kukosa utulivu kwa mabeki wao.
JKT ilicheza mchezo wa jana ikimkosa kipa wake namba moja Ramadhan Chalamanda ambaye anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City, lakini Gonzo hakuonyesha udhaifu mkubwa.
Kama sio uimara wa Gonzo JKT ingeweza kupotea mapema kutokana na kipa huyo kuokoa mashambulizi matatu makubwa ya Simba kwenye mchezo huo.
Msimu uliopita mtu bora ndani ya Simba alikuwa Jean Charles Ahoua lakini msimu huu kazini kwake kuna kazi kwani kijana wa Kitanzania Morice Abraham ni mtu na nusu.
Morice ana kasi kubwa anapokuwa na mpira kazi yake inakuwa moja tu kulitafuta lango la wapinzani walipo kama sio kutoa pasi basi atapiga shuti kali, hiyo kasi ndio kitu Ahoua anakikosa.
Morice ameshatengeneza mabao tena akiwa anaingia akitokea benchi. Hili lazima limuamshe Ahoua kama anataka kulinda heshima yake hasa wakati huu ambao kinda huyo mzawa aliyepikwa na kazi ya Shirikisho la Soka Tanzania, anavyozidi kujiongezea mashabiki Simba.
Mshambuliaji Jonathana Sowah jana alifunga bao lake la pili msimu huu, akitokea pia kutengeneza bao kwenye mchezo wa mwisho Simba walioshinda ugenini wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Sowah anaonyesha ukomavu akiingia dakika chache baada ya Simba kutanguliwa akichukua nafasi ya mwenzake Steven Mukwala na kwenda kuibeba timu yake akizidi kutenegeneza imani kwa Pantev wakati huu kocha huyo akiendelea kuitengeneza Simba.