Wadau wafunguka kauli ya Nchimbi kuhusu maridhiano

Dar es Salaam. Kukiri makosa, kuepuka kunyoosheana vidole, kuponya majeraha na kusitisha kamatakamata ndiyo mambo yaliyopendekezwa na wadau wa kada tofauti, akiwamo Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza.

Wadau hao wamesema njia hiyo itasaidia kuwezesha kufanyika kwa maridhiano nchini na kufikiwa mwafaka tarajiwa.

Wamesema kwa kufanya hivyo pia, kutaonesha ustahimilivu wa dola kwenye kuusaka mwafaka badala ya hasira.

Mitazamo hiyo ya wadau inakuja, siku mbili baada ya Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi kueleza dhamira ya Serikali kuanzisha maridhiano ili kuhakikisha kila sauti inasikilizwa na kurejesha amani.

“Dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba tunaanzisha mazungumzo ya maridhiano ili kuhakikisha hata hao wachache wanapata nafasi ya kusikilizwa ili kuwa na Taifa lenye amani na umoja na kuendelea kuwa mfano wa utulivu katika Afrika na dunia,” amesema Dk Emmanuel katika mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Hata hivyo, kilichoelezwa na Dk Nchimbi katika mkutano huo, ni sehemu ya ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni zake, aliyeahidi kuanzisha tume ya usuluhishi na maridhiano kusikiliza wananchi.

Katika ahadi yake hiyo, pamoja ya maridhiano na upatanishi, tume hiyo ndiyo itakayoanza mchakato wa awali wa Katiba Mpya kwa kuanzisha tume ya Katiba ndani ya siku 100 za urais wake.

Kwa mtazamo wa Askofu Bagonza, waliotaka maridhiano kabla ya uchaguzi hawayataki sasa, huku walioyakataa kabla ya uchaguzi, wanayataka sasa.

“Damu ni nyingi na mbichi. Isafishwe kwa kuruhusu watu kuzika na kuomboleza. Bila hilo, kuingia katika maridhiano ni kujipaka damu,” amesema.

Hilo, ametaka lifuatiwe na kusitisha ukamataji, kuachia walioshikiliwa kwa kuwa, baadhi ya wanaoweza kukaa mezani ni waliopotezwa au walio mahabusu.

Amesema, pia Taifa linapaswa kuwa salama kwa wanaopongeza na wanaokosoa, akidokeza kwa sasa wakosoaji wanakimbia nchi.

Ili ijulikane maridhiano hayo yawe nani na nani, amesema ni muhimu tume ya kuuweka ukweli hadharani iundwe kujua nani asamehewe, aridhiane na nani, achukuliwe hatua za kisheria, afidiwe ili kuepusha yajayo.

Sambamba na hilo, ametaka ⁠tume au kamati hiyo ya maridhiano iandaliwe utaratibu mzuri wa upatikanaji wake na itawajibika kwa nani ili isipoteze imani kutoka kwa wananchi.

Akizungumzia hilo, Mchambuzi wa Masuala ya Siasa na Utawala, Philemon Mtoi amesema ingawa vurugu hizo zinanasibishwa na masuala ya kisiasa na wanasiasa, kuna umuhimu unapotafutwa mwafaka kupitia maridhiano, yahusishwe makundi yote.

Amesema kwa kuwa ni vigumu kumchukua mwananchi mmoja mmoja, amependekeza watafutwe wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wananchi, lakini wasiwe wabunge kwa kile alichoeleza, hawaaminiki kuwakilisha katika jambo hilo.

Wawakilishi aliowapendekeza Mtoi, ni viongozi wa dini kulingana na madhehebu yao, viongozi wa jumuiya na asasi za vijana ziwe za kisiasa au kijamii, viongozi wa kisiasa vyama vyote na waitwe wenye nguvu na wanaopendwa na wengi.

Wengine aliopendekeza kuwa sehemu ya wawakilishi katika maridhiano hayo, ni viongozi wa vyombo vya dola, ulinzi na usalama na Serikali.

Asitafutwe mshindi, tukubali makosa

Ametahadharisha kusiwepo upande utakaojiona dhaifu mbele ya mwingine katika mazungumzo hayo ya kuusaka mwafaka wa pamoja na kila sauti isikilizwe na kupewa nafasi sawa, huku lengo likiwa ni mustakabali wa Taifa na sio kushinda mazungumzo.

“Wakishaingia hapo, lazima makundi yote yenye masilahi na nchi lazima yakubali kuwa yamekosea. Serikali lazima ikubali imekosea na hata waandamanaji lazima wakubali kuwa kuna matendo walikosea,” ameeleza.

Ili kuwe na maridhiano na upatikane mwafaka, amesema lazima wote wawe katika hali ya kutonyoosheana vidole, waingie wakiwa na nia ya dhati ya kuutafuta mustakabali wa Taifa.

“Naposikia tunasema tunaenda kwenye maridhiano, lakini bado kuna wadau wanaonekana kupata shuruba ikiwamo kukamatwa, hiyo inaleta shida zaidi,” amesema.

Amesema maridhiano mara zote si kumtafuta mshindi au mkosaji, bali kutengeneza makubaliano kwa hoja za pande zote kwa masilahi ya pamoja.

Pia, amesema yote hayo, yanapaswa kufanyika chini ya utashi wa dhati wa kisiasa kwa Serikali na pande zote ili lipatikane suluhisho jumuishi ili kitakachoamuliwa, kitekelezwe kwa nguvu na ari.

“Siamini kwamba hatuwezi kutoka hapa. Asili ya Watanzania hatujafikia hatua ya kuiondoa amani yetu, bado tuna muda wa kuyamaliza. Tusiendelee kuumizana, watu wasikamatwekamatwe hata kama tuna ushahidi wa makosa yao,” amesema.

Katika maridhiano hayo, amesema kila sauti isipuuzwe, bali iangaliwe namna ya kuhakikisha nia na mahitaji yake yanatimizwa kwa masilahi ya wote.

“Utashi wa kisiasa na kutokuwa na kiburi ndilo jambo la msingi. Majadiliano lazima yawe yanayohusisha watu wenye lengo moja la kuwa na mustakabali bora wa Taifa. Isitokee sauti itakayopuuzwa,” amesema.

Kama inavyoelezwa na Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo kwamba, “ili tutoke tulipofika, ni muhimu kama Taifa tuanze kwa kujibu swali kwamba tupo tayari kutoka hapo?”

Dk Masabo amesema swali hilo linapaswa kujibiwa na kila Mtanzania kutoka viongozi wa juu wa Serikali au nchi hadi raia wa kawaida.

“Wajibu wa kutoka tulipo ni wa kila Mtanzania, lakini kiwango cha uwajibikaji kitapishana kulingana na dhamana aliyonayo mtu kwenye nchi husika,” amesema.

Mwanazuoni huyo, amesema mkulima hawezi kuwa na dhamana sawa na mwanasiasa, polisi au kiongozi wa dini. Kila mmoja ana dhamana yake.

Ikishajulikana kuna utayari, amesema ni muhimu kukubali hadi kimetokea kilichotokea, tumekosea na katika hilo asinyooshewe kidole yeyote, makosa yabebwe na kila Mtanzania.

“Nimeona tumeanza kufanya siasa za kunyoosheana kidole kutafuta nani alikosea. Lazima wote tukubali kwamba hilo ni kosa letu. Tukubali zilitokea vurugu, uharibifu wa mali na upoteaji wa maisha, tusikwepe chochote kati ya hayo,” amesisitiza.

Kuponya majeraha, kuwajibika

Dk Masabo amesema hatua hiyo ifuatiwe na kupita mitaani, kuchukua rekodi ya waliopoteza maisha na watu wahifadhiwe kwa mujibu wa imani na tamaduni zao.

“Hicho kitatoa cultural healing (itaponya kwa upande wa tamaduni). Kwa sababu kwetu mtu kufa ni tatizo lakini litakuwa tatizo zaidi, iwapo hatazikwa kwa utaratibu wa kiimani au kitamaduni,” amesema.

Mwanazuoni huyo anapendekeza hatua itakayopaswa kufuata ni kuandaliwa mpango wa angalau kuzifuta machozi familia za wafiwa na waliopoteza mali, ingawa haina thamani sawa na uhai wa mtu, lakini inaonesha umethamini na kujali.

Kisha, amesema waliohusika kwa namna yoyote, kuanzia kuhamasisha, kubeza na kutekeleza kilichotokea wawajibishwe bila kujali ni raia au kiongozi.

Dk Masabo amesema ni muhimu tuhuma zote zinazodaiwa zichunguzwe na kubaini uhalisia wake, ikiwamo kuingia kwa jeshi kutoka nje na wananchi kutoka mataifa ya nje.

‘Anayeaminika asimame kati’

Na kwa kuwa kuna kundi linaloonekana halitaki tena kuridhiana, amesema atafutwe mtu anayekubalika kwenye jamii na apewe dhamana ya kusaidia kuwezesha mazungumzo.

“Lakini bahati mbaya kwa sasa (Tanzania) hakuna mtu anayekubalika kwa pande zote. Hatuna mtu wa kutusaidia na kwa sababu hatuna lazima tuazime mtu kutoka duniani, tunayeweza wote kumsikiliza,” amesema.

Amesema mtu huyo anapaswa kuwa anayesikilizwa, kukubalika na kuheshimiwa na kila upande ili asimame katikati ya mazungumzo kwa dhamira moja ya kuleta mwafaka wa kitaifa.