Hesabu kali za Dimitar Pantev Simba

MASTAA wa Simba wapo mapumzikoni baada ya kukamilisha mechi tatu za Ligi Kuu Bara kibabe kwa kuifumua JKT Tanzania kwa mabao 2-1, lakini meneja mkuu wa timu hiyo, Dimitar Pantev hapumziki akiwa ameanza hesabu mpya ili kuwapa raha mashabiki.

Simba ilipata ushindi huo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam na Jumanne Novemba 11, 2025, wachezaji wa timu hiyo wasiokuwa timu za taifa wanarudi kambini baada ya mapumziko ya siku mbili, ili kuanza maandalizi ya mechi ya kwanza ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Wekundu hao ambao ni kati ya timu nne za Tanzania zilizofuzu makundi ya michuano ya CAF msimu huu, sambamba na Yanga, Azam na Singida Black Stars, inatarajiwa kuwa wenyeji wa Petro Atletico ya Angola katika mechi ya kwanza ya Kundi D itakayopigwa Novemba 23, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mara baada ya mechi hiyo, Simba itaifuata Stade Malien kwa mechi ya pili itakayochezwa kati ya Novemba 28 na 30, 2025 jijini Bamako nchini Mali na Pantev ameiambia Mwanaspoti ameshaanza hesabu za mechi hizo ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

JESHI 01


Pantev amesema ushindi dhidi ya JKT Tanzania akiiongoza Simba kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu, umeongeza morali katika kikosi hicho kabla ya mechi za kimataifa.

Kabla ya hapo, mechi mbili za awali za timu hiyo ilikuwa chini ya Seleman Matola aliyekaimu baada ya kocha mkuu, Fadlu Davids kuondoka klabuni hapo.

Pantev amesema ratiba ya klabu yao inahitaji umakini mkubwa kulingana na aina ya wapinzani ambao watakabiliana nao.

“Ni jambo zuri kuanza kwa ushindi, hili limepita tayari na malengo yetu ni mechi za CAF. Hii ni hatua kubwa zaidi tofauti na awali,” amesema Pantev.

JESHI 02


“Tumetoa siku mbili za kupumzika kwa wale waliobaki kwa kutoitwa timu za taifa, tunataka warejee wakiwa akili zenye nguvu kwa sababu mechi ya CAF, tunajua Petro na hata Malien sio nyepesi, hivyo lazima tujipange ili kuanza vyema hatua ya makundi,” amesema Pantev.

Raia huyo wa Bulgaria amesema atawakosa wachezaji waliopo katika majukumu ya kimataifa kwa takribani siku tano au sita akiwemo Yakoub Suleiman, Shomary Kapombe, Wilson Nangu, Seleman Mwalimu na Morice Abraham, jambo linalowalazimu kutumia mpango wa maandalizi kama ilivyokuwa kabla ya kukabiliana na mechi ya mkondo wa kwanza dhidi ya Nsingizini Hotspurs katika hatua ya pili. 

JESHI 03


“Baada ya kalenda ya FIFA na wachezaji hao kurudi tutakuwa nao pamoja kwa siku tatu au nne tu kabla ya mechi dhidi ya Petro, hivyo tutashea nao kile ambacho tumekuwa tukikifanyia kazi siku chache kabla ya mechi,” amesema Pantev.

Simba itaanza hatua ya makundi nyumbani, jambo ambalo Pantev analiona kama faida wanayotakiwa kuitumia vizuri huku akitaka kuwa na mechi moja au mbili za kirafiki ili kuwaweka sawa wachezaji waliosalia. 

Akizungumzia wapinzani wao, Pantev amesema Petro de Luanda ni timu ya kisasa inayocheza kwa kasi na nidhamu huku akienda mbali kwa kusema imefika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa 2021-2022 na robo fainali msimu uliopita 2024-2025. 

“Nimepata nafasi ya kuwaona japo kwa uchache wanacheza soka la pasi fupi, wanapenda kushambulia kutokea pembeni  kwa hiyo umakini wetu unatakiwa uwe mkubwa wakati tukitekeleza mpango wetu,” amesema Pantev. 

JESHI 04


Katika kundi D, Simba pia itakutana na Esperance Sportive de Tunis, moja ya klabu kongwe na zenye mafanikio makubwa Afrika. Klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1919, imecheza fainali tisa za Ligi ya Mabingwa na kutwaa mara nne kwenye miaka ya 1994, 2011, 2018 na 2019. 

Wapinzani wengine ni Stade Malien, mabingwa wa Mali. Klabu hii imewahi kutwaa Kombe la Shirikisho mwaka 2009.
Baada ya kumalizana na Petro Luanda nyumbani, Simba itaelekea Mali Novemba 28, 2025 kucheza na Stade Malien.