Dodoma. Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamemchagua Mussa Zungu, mbunge mteule wa Ilala, kuwa mgombea wa nafasi ya Spika wa Bunge la 13 kupitia chama hicho.
Zungu amechaguliwa baada ya kupata kura 348 dhidi ya kura 16 alizopata mshindani wake ambaye ni mbunge wa zamani wa Shinyanga, Stephen Masele, aliyeonekana kupewa nafasi kabla ya upigwaji wa kura kuanza.
Katika uchaguzi wa Spika, atakayeshinda atakuwa Spika wa nane wa Bunge la Muungano ambalo limeshaongozwa pia na maspika wanawake akiwamo Anne Makinda na Dk Tulia Ackson.
Kuchaguliwa kwa Zungu kumekuwa mwendelezo wa manaibu Spika kushika wadhifa huo. Itakumbukwa, Anne Makinda, marehemu Job Ndugai, Dk Tulia Ackson, na sasa Zungu, wote hawa walikuwa manaibu Spika kabla ya kuwa maspika kamili.
Kwa sasa, Zungu anasubiri wagombea wengine nje ya CCM kama watajitokeza kwa ajili ya kushindaniwa kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumanne, Novemba 11, 2025, ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Awali, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ilipitisha majina matatu ya wagombea wa kiti cha Spika, akiwamo Spika aliyemaliza muda wake, Dk Tulia, huku mchuano ulionekana kuwa mkubwa kati ya Dk Tulia na Zungu.
Hata hivyo, Novemba 7, Dk Tulia alitangaza kujitoa katika kinyang’anyiro hicho, hivyo kubaki majina mawili ambayo yamewasilishwa mbele ya wabunge wa chama hicho kwa ajili ya kupigiwa kura.
Mbunge huyo wa Ilala aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2005 na amehudumu katika nafasi mbalimbali, ikiwamo kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa kipindi cha miaka 18.
Tangu mwaka 2016, Zungu amehudumu katika nafasi ya ujumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge (2016–2025), amekuwa kiongozi wa Bunge la Tanzania katika mikutano ya Umoja wa Mabunge ya Nchi za Afrika, Pasifiki na Karibi na Bunge la Jumuiya ya Ulaya.
Nafasi nyingine alizoshika ni kuwa kiongozi wa chama cha Jumuiya ya Mabunge ya Jumuiya ya Madola Tanzania na mwakilishi wake katika vikao vya kimataifa vya jumuiya hiyo.
Amekuwa Mwenyekiti wa Bunge tangu mwaka 2012 hadi 2021 na Naibu Spika kuanzia mwaka 2022 hadi 2025.
Pia, amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa miaka 18, na amewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Kwa upande wake, mshindani wake Masele alishawahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na alihudumu katika nafasi ya Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), nafasi ambayo ilimuingiza katika mgogoro na aliyekuwa Spika wa Bunge, Ndugai, hasa baada ya kunukuliwa akisema hakuwa anapewa heshima yake kama kiongozi wa Bunge la Afrika.
Katika hatua nyingine, leo wabunge wa CCM wamemchagua mbunge wa Babati Vijijini, Daniel Sillo kwa kura 362 kuwa mgombea wao kwa nafasi ya Naibu Spika wa Bunge hilo. Kura mbili ziliharibika. Uchaguzi wake utafanyika baada ya kuchaguliwa kwa Spika na wabunge wote wakisha kula kiapo.
Mgombea huyo wa kiti cha Naibu Spika amechaguliwa baada ya wagombea wenzake, Timotheo Mzava (Korogwe Vijijini) na Najma Giga (Viti Maalumu), ambao inaelezwa walijitoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kubaki jina moja.
Kuchaguliwa kwa Sillo kuwania nafasi ya Naibu Spika kunaendeleza historia ya kupokea kijiti cha Zungu, kwani Aprili 4, 2023, mbunge huyo alipitishwa kwa kauli moja na wabunge na kushika nafasi ya Mwenyekiti, akichukua nafasi ya Zungu ambaye tayari alishachaguliwa kuwa Naibu Spika.
Sillo aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2020 na aliaminiwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, na baadaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, nafasi aliyoitumikia hadi Bunge lilipovunjwa.