Dar es Salaam. Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu iliyoahirishwa kupisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, itarejea kesho Jumatatu, Novemba 10, 2025.
Kesi hiyo inayosikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru akishirikiana na James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, ilianza kusikilizwa ushahidi Oktoba 6 mpaka 24, 2025.
Ilipangwa kuendelea baada ya kumalizika uchaguzi huo Oktoba 29, 2025, kwa siku 10 za kazi, kuanzia Novemba 3 mpaka 12, 2025.
Hata hivyo, Novemba 3 kesi haikuendelea kutoka na athari za uchaguzi huo, kufuatia maandamano katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na katika mikoa mingine, hali iliyoilazimu Serikali kusimamisha shughuli mbalimbali zikiwamo za kiofisi.
Taarifa za uhakika mahakamani hapo zilizothibitishwa na mmoja wa mawakili wanaomsaidia Lissu, Hekima Mwasipu zinaeleza kesi hiyo itaendelea tena kuanzia Jumatatu, Novemba 10, 2025.
“Ni sahihi,” amesema wakili Mwasipu alipoulizwa na Mwananchi.
Katika kesi hiyo namba 19605 ya Mwaka 2025, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Anadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha meneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…kwa hiyo tunaenda kukinukisha…sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli… tunaenda kukinukisha vibaya sana.”
Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo kupisha uchaguzi, tayari mashahidi watatu wa Jamhuri, ambao wote ni maofisa wa polisi, walikuwa wameshatoa ushshidi wao.
Shahidi wa mwisho wakati kesi hiyo inaahirishwa kupisha uchaguzi ni Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, Samweli Eribariki Kaaya (39), Mtaalamu wa Picha, kutoka Kitengo cha Picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake wa msingi alieleza Aprili 8, 2025 alipokea flash disk na memory card zenye video ya Lissu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Dar es Salaam kuchunguza uhalisia wake.
Shahidi huyo aliieleza Mahakama katika uchunguzi wake alibaini video hiyo ni halisi na haina pandikizi, kisha akaandaa ripoti ya uchunguzi huo.
Oktoba 17, 2025 aliiomba Mahakama hiyo ivipokee vihifadhi data hivyo (flash disk na memory card) zenye video ya Lissu lakini Lissu aliiwekea pingamizi na Mahakama katika uamuzi wake Oktoba 22, 2025 ilikubaliana na pingamizi hilo ikavikataa vihifadhi data hivyo.
Baada ya uamuzi huo Jamhuri iliomba ripoti ya uchunguzi wa uhalisia wa video hiyo ipokewe kuwa kielelezo cha ushshidi wa Jamhuri.
Lissu aliipinga na Mahakama katika uamuzi wake wa Oktoba 23, 2025, ilikubaliana na pingamizi la Lissu na kuikataa ripoti hiyo.
Shahidi huyo baada ya kuhitimisha ushahidi wake, Kiongozi wa Jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Lenatus Mkude aliiomba Mahakama iahirishe kesi hiyo mpaka kesho yake, Oktoba 24, 2025 lakini akaiarifu kuwa wanaendelea kutafakari kuhusu uamuzi dhidi ya vielelezo vilivyokataliwa.
Lissu alisema hana pingamizi na ombi la Jamhuri kuahirisha kesi hiyo akiieleza Mahakama kuwa, anaiomba Jamhuri katika tafakari yake hiyo pia itafakari kama baada ya uamuzi huo kama kuna sababu ya kuendelea na hiyo kesi.
“Waheshimiwa majaji, sina pingamizi kuhusu kesi kuahirishwa mpaka kesho(Oktoba 24, 2025)… lakini nina jambo moja dogo tu. Jamhuri katika tafakari yake hiyo itafakari kama bado kuna sababu ya kuendelea na kesi hii”, alisema Lissu.
Oktoba 24, 2025, Wakili Mkude aliieleza Mahakama kuwa mashahidi wao waliokuwa wanafuata wana uhusiano na vielelezo vilivyokataliwa na kwamba kutokana na uamuzi huo wa kuvikataa vielelezo hivyo, hawatawatumia tena mashahidi hao.
Alisema kwa sababu hiyo, siku hiyo hawakuwa na shahidi na kwa kuwa ndio ilikuwa siku ya mwisho ya kikao cha usikilizwaji kesi hiyo, akaiomba Mahakama iahirishwe kesi hiyo mpaka Novemba 3, 2025.
Lissu alipinga ombi hilo, kwanza akidai sababu iliyotolewa si ya msingi.
“Kwa hiyo rai yangu, ombi la kuahirishwa likataliwe, Jamhuri walete shahidi tuendelee kama ikikubaliwa nipewe dhamana ili nisiendelee kukaa gerezani, mimi siwezi kukimbia kwa sababu sina makosa,” alisisitiza Lissu.
Hoja za Lissu zilipingwa vikali na Wakili Mkude pamoja na Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga, kwa hoja na rejea za vifungu vya sheria.
Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote ilikubaliana na hoja na maombi ya Jamhuri ikaahirisha kesi hiyo hadi Novemba 3, 2025 ambayo hata hivyo haikuendelea kutokana na sababu za athari za uchaguzi ndipo ikapangwa kuendelea Jumatatu.