Askofu Nyaisonga ataja mambo sita vurugu za Oktoba 29, asisitiza…

Mbeya. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Mbeya, Gervas Nyaisonga amewaongoza waamini na wananchi katika ibada maalumu ya kuwaombea walioathirika kwenye vurugu wakati na baada ya uchaguzi mkuu, huku akitaja malengo sita ya ibada hiyo.

Uchaguzi mkuu ulifanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 ambapo kuliibuka vurugu katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali na miundombinu kabla na wakati wa shughuli hiyo.

Akizungumza leo Jumapili Novemba 9, 2025 katika ibada hiyo iliyofanyika Kanisa Mwanjelwa jijini Mbeya, Askofu Nyaisonga amesema wakati na baada ya uchaguzi ilitokea vurugu zilizosababisha mauaji, majeruhi na uharibifu wa mali za umma na binafsi.

Amesema miongoni maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Mbeya na Songwe, ndio maana Kanisa hilo kuamua kuwaombea waliopoteza maisha, kujeruhiwa na walioathirika na matukio hayo.

“Madhumuni ya misa hii yapo sita, kuwaombea marehemu, kuwaombea majeruhi, kumuomba Mungu asaidie jitihada kuwapata waliopotea wawe hai au wamekufa, kuwapa pole waliopoteza mali zao, kutoa rai ya kujitathimini na kuomba uponyaji kutoka Mungu wetu,” amesema.

“Katika uchaguzi wa mwaka huu kumetokea vifo vya wenye hatia na wasio na hatia, wamo watoto, vijana na wazee, wanawake na wanaume, raia na askari na Novemba 4 nimeshuhudia wingi wa watu waliokuwa wakinunua majeneza, misafara ya magari wakisafirisha vilio kwenda nje ya Mbeya,” amesema Nyaisonga.

Askofu huyo amesema kutokana na matukio kuwa mengi kwa wakati mmoja na haijulikani nani apewe pole au nani aachwe, badala yake misa hiyo inatoa pole kwa ujumla kwa waliofikwa na madhila yoyote.

Akitumia maneno ya wasanii kundi la Msondo Ngoma, walioimba ‘ukiona mtu mzima analia jua kuna jambo…tunatoana roho kwa mali alizoacha baba’ amesema wimbo huo uwekwe kwa muktadha wa Taifa.

Amesema kabla na wakati wa uchaguzi mkuu, watu kadhaa waliripotiwa kupotea kwa mazingira ya kutatanisha na wasio julikana, akieleza wanaomba Mungu asaidie wapatikane kwa mazingira yoyote.

“Tumeshuhudia upotevu na uharibifu wa mali za umma na binafsi, tunawapa pole kwa hasara mbalimbali, Mungu ameleta hili ili tugutuke kutoka kwenye usingizi uliotusahaulisha mambo ya msingi,” amesema.

“Tunatoa mwaliko wa kujitathimini, nchi yetu ilionekanaje wakati moto ukiwaka maeneo mbalimbali…hata mbinguni walishangaa, barabara na madaraja yanajengwa, huduma zinatolewa, lakini unajiuliza kwa nini tufikie hatua hii mbaya,” amesema na kuhoji Askofu Nyaisonga.

Amesema, “lakini yote hayo unaweza kusema labda wanaofanya hivi hawaoni mazuri, labda ni maadui, chuki binafsi au wanatoka nje labda labda labda zitakuwa nyingi ila ukitafakari sidhani kama wahuni wanaweza kujitokeza kwa wingi wakati mmoja hata wahuni hawawezi kufa kwa sababu za kijinga,” amesema Nyaisonga.

Amesema lazima kukubali kuwa zipo sababu za msingi hadi kufikia hatua hiyo na kwamba lazima kutafuta wadhamini safi wenye uwelekeo na utayari wa toba, ili kujua kiini cha tatizo hilo na kutoruhusu baadhi ya watu kutumia fursa za machafuko nchini.

“Tunaomba Mungu aliponye Taifa letu na kuliepusha na migogoro na atuponye sote, kwa unyenyekevu niwaombe wafiwa wasamehe na wawe tayari kuanza upya kama wajasiri kujenga upya kwa faida ya waliopo na wajao,” amesema Askofu huyo aliyewahi kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).