Mashujaa kuna kitu kinapikwa kwa Ismail Mgunda

KOCHA wa Mashujaa, Salum Mayanga amesema anapambana kuhakikisha mshambuliaji wa kikosi hicho, Ismail Mgunda anarejea katika kiwango bora kama mwanzoni, licha ya ushindani mkubwa katika eneo hilo na washambuliaji wengine walio kikosini.

Nyota huyo aliitumikia Mashujaa msimu wa 2024-2025, kisha baadaye kuuzwa kwenda AS Vita Club ya DR Congo dirisha dogo la Januari 2025, ingawa hakudumu ndani ya kikosi hicho, kwa sababu alikichezea kwa miezi sita tu na kurejea tena nyumbani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga amesema mshambuliaji huyo hajaanza vizuri kama wengi wanavyomjua, ingawa anaendelea kupambana kumtengenezea mazingira mazuri kwa kushirikiana na wengine, kwa sababu anamtegemea kutokana na uzoefu wake.

“Moja ya changamoto kwetu msimu huu ni eneo la ushambuliaji na tumeingiza takribani wachezaji tisa wapya, hivyo sio kazi rahisi kutengeneza muunganiko kwao, jambo nzuri nafasi zinatengenezwa hivyo, hilo linatupa matumaini,” amesema Mayanga.

Mayanga amesema katika kipindi hiki cha kupisha mechi za kimataifa ataendelea kukitumia kufanyia kazi eneo hilo kutokana na washambuliaji waliopo, kwani jukumu lake ni kutengeneza namna ya kuwaunganisha pamoja na kucheza uwanjani kama timu.

“Tumecheza mechi sita na ukiangalia bado timu haina balansi nzuri kwa maana ya ushambuliaji lakini hata eneo letu lote la kujilinda, ni jukumu tunalopambana nalo siku baada ya siku, kwa sababu tulipo sio pabaya wala pazuri pia,” amesema.

Mgunda aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo za Ruvu Shooting, Jomo Cosmos ya Afrika Kusini na Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars, kabla ya kwenda Congo aliifungia Mashujaa mabao mawili ya Ligi Kuu Bara na kuasisti matatu.