Josiah asuka mipango Dodoma Jiji

KOCHA wa Dodoma Jiji, Amani Josiah amesema katika kipindi hiki ambacho Ligi Kuu Bara imesimama anapambana kutengeneza utimamu mzuri wa mwili kwa wachezaji wa kikosi hicho, kabla ya pambano lijalo dhidi ya Namungo ugenini Novemba 21, 2025.

Josiah alijiunga na timu hiyo Oktoba 16, 2025, baada ya kocha raia wa Rwanda, Vincent Mashami, aliyetangazwa kukiongoza kikosi hicho mwanzoni mwa msimu huu kutokuwa na vigezo vya kusimamia benchi la ufundi kama kanuni za Ligi zinavyohitaji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Josiah amesema tangu amekabidhiwa timu hiyo kumekuwa na kuimarika kimbinu na staili pia ya uchezaji kwa wachezaji kama anavyotaka, licha ya kiwango na matokeo wanayoyapata hayaakisi kile kinachotokea uwanjani.

“Ni muda wetu kufanyia kazi eneo hilo kisha ndio tuendelee kuimarisha uwiano mzuri wa timu kiuchezaji na mambo mengine ya ufundi, kwa sasa tunapambana sana na hili la utimamu wa mwili kutokana na kusimama kidogo kwa Ligi,” amesema Josiah.

Josiah aliyewika na timu za Tunduru Korosho, Biashara United ‘Wanajeshi wa Mpakani’, Geita Gold na maafande wa Tanzania Prisons, amesema muda huu utakuwa mzuri kwao pia kwa wachezaji baadhi waliokuwa majeruhi kurejea na kuungana na wenzao.

Tangu Josiah amekabidhiwa kikosi hicho amekiongoza katika mechi tatu za Ligi Kuu, akianza kuchapwa bao 1-0 na Fountain Gate Oktoba 17, akatoka suluhu (0-0) na Mtibwa Sugar Oktoba 22, kisha kupokwa ushindi na Pamba Jiji, Oktoba 25, 2025.

Katika pambano hilo la Oktoba 25, 2025, Pamba Jiji ilipewa ushindi wa bure wa mabao matatu na pointi tatu pia, baada ya mechi hiyo kuchezwa kwa dakika sita tu, baada ya  kutokea kwa hitilafu ya umeme kwenye Uwanja wa Jamhuri jijiji Dodoma.

Hadi mechi inasimama, Dodoma Jiji ilikuwa inaongoza bao 1-0, lililofungwa na Benno Ngassa, japo Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu katika kikao chake cha Oktoba 27, 2025, kilitoa uamuzi wa kuipa Pamba Jiji ushindi huo wa bure.

Sababu ya Dodoma Jiji kupokwa ushindi huo ni kutokana na kutofanya juhudi zozote za kurejesha mwanga kwenye Uwanja wa Jamhuri hivyo, kusababisha mechi hiyo kuvurugika, huku adhabu ikitolewa kwa kuzingatia kanuni ya 32:3 ya Ligi Kuu Bara.

Kutokana na adhabu hiyo na kwa mujibu wa kanuni ya 32:3 ya Ligi Kuu Bara kuhusu kuvuruga mechi, bao la mshambuliaji huyo nyota wa Dodoma Jiji, Benno Ngassa alilolifunga lilifutwa rasmi katika orodha ya mabao yake na ya timu anayoichezea pia.