Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo imeyakataa maombi ya Jamhuri kusimamisha kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kwa siku 14 kutokana na hofu ya usalama.
Mahakama hiyo imeamuru kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo keshokutwa Jumatano, Novemba 12, 2025, huku ikiitaka Jamhuri kupeleka mashahidi wake.
Katika kesi hiyo namba 19605 ya mwaka 2025, Lissu anakabiliwa na shitaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Anadaiwa kuwa, Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha meneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inayosikilizwa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru akishirikiana na James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, ilianza kusikilizwa ushahidi Oktoba 6 mpaka 24, 2025 ilipoahirishwa kupisha uchaguzi mkuu.
Ilipangwa kuendelea baada ya kumalizika uchaguzi huo, kwa siku 10 za kazi, kuanzia Novemba 3 mpaka 12, 2025.
Hata hivyo, Novemba 3 kesi haikuendelea kutokana na athari za uchaguzi huo, kufuatia maandamano yaliyofanywa na baadhi ya vijana katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na mikoa mingine, hali iliyoilazimu Serikali kusimamisha shughuli mbalimbali hasa za kiofisi.
Hivyo, ilipangwa kuendelea leo, Jumatatu, Novemba 10,2025.
Hata hivyo,leo Lissu hakufikishwa mahakamani.
Mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawabu Issa ameieleza Mahakama kuwa, baada ya kufika mahakamani na kukuta mshtakiwa hajaletwa, wamechukua hatua ya kuwasiliana na Mkuu wa Magereza, ambaye amewaeleza kuwa, wameshindwa kumfikisha mahakamani kwa sababu za kiusalama.
“Lakini pia, shauri hilo liliahirishwa kwa ajili ya kuja kuendelea na usikilizwaji Novemba 3, 2025 kutokana na hali ya kiusalama iliyokuwepo, tarehe hiyo hatukuweza kufika mahakamani shauri likawa limepangwa tarehe ya leo kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji,” amesema Wakili Issa.
Amesema kesi hiyo ilipaswa kuendelea kusikilizwa upande wa mashitaka kuwasilisha ushahidi wao.
Hata hivyo, amesema kutokana na hali ya Jiji la Dar es Salaam kutokuwa kwenye hali ya utulivu, mashahidi waliopaswa kufika walikuwa wanatokea Ruvuma na Mbeya, hivyo katika kusubiri hali ya usalama itengemae wakawa wameshindwa kufika.
“Waheshimiwa majaji, tarehe ya leo hatukupata shahidi kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji kwa sababu hizo. Hivyo waheshimiwa majaji, kama itawapendeza tunaomba shauri hili liahirishwe chini ya kifungu cha 302(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Marejeo ya Mwaka 2025, kwa sababu hiyo ya kutokuwepo kwa mashahidi kutokana na kushindwa kusafiri kutokana na hali ya kiusalama,”amesema Wakili Issa.
“Ikiwapendeza waheshimiwa majaji, mtupatie siku 14 kuangalia hali ya kiusalama ili tuendelee na shauri hili.”
Hata hivyo, Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Ndunguru baada ya kusikiliza hoja za pande zote, imekataa maombi hayo ya Jamhuri ya kuahirisha kesi hiyo kwa siku 14, badala yake imeamua kesi iendelee kusikilizwa Jumatano Novemba 12, 2025.
“Kwa kuwa, mshtakiwa hayupo na hamna mashahidi, shauri linaahirishwa na litakuja mapema Jumatano tarehe 12, 2025 kusikilizwa, upande wa mashitaka mlete mashahidi na samansi itolewe, mshtakiwa aletwe mahakamani kwa ajili ya shauri kuendelea kusikilizwa,” amesema Jaji Ndunguru.
Kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo kupisha uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, tayari mashahidi watatu wa Jamhuri ambao wote ni maofisa wa polisi, walikuwa wameshatoa ushahidi wao.
Shahidi wa mwisho wakati kesi hiyo inaahirishwa kupisha uchaguzi, alikuwa Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, Samweli Eribariki Kaaya (39), Mtaalamu wa Picha kutoka Kitengo cha Picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake wa msingi, alieleza kuwa Aprili 8, 2025 alipokea flash disk na memory card zenye video hiyo ya Lissu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Dar es Salaam kuchunguza uhalisia wake.
Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa, katika uchunguzi wake, alibaini video hiyo ni halisi na haina pandikizi, kisha akaandaa ripoti ya uchunguzi huo.
Oktoba 17, 2025 aliiomba Mahakama hiyo ivipokee vihifadhi data hivyo (flash disk na memory card) zenye video ya Lissu, lakini Lissu aliiwekea pingamizi.
Mahakama katika uamuzi wake Jumatano Oktoba 22, 202 ilikubaliana na pingamizi hilo ikavikataa vihifadhi data hivyo.
Baada ya uamuzi huo, Jamhuri iliomba ripoti ya uchunguzi wa uhalisia wa video hiyo ipokewe kuwa kielelezo cha ushahidi wa Jamhuri.
Lissu alipinga, Mahakama katika uamuzi wake Oktoba 23, 2025, ilikubaliana na pingamizi la Lissu na kuikataa ripoti hiyo.
Shahidi huyo baada ya kuhitimisha ushahidi wake, kiongozi wa Jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Lenatus Mkude aliiomba Mahakama iahirishe kesi hiyo mpaka Oktoba 24, 2025 akisema, wanaendelea kutafakari kuhusiana na uamuzi dhidi ya vielelezo vilivyokataliwa.
Lissu alisema hana pingamizi na ombi la Jamhuri kuahirisha kesi hiyo lakini akaiomba Mahakama kuwa, Jamhuri katika tafakari yake hiyo, itafakari kama baada ya uamuzi huo kuna sababu ya kuendelea na hiyo kesi.
“Wahesimiwa majaji, sina pingamizi kuhusu kesi kuahirishwa mpake kesho (Oktoba 24), lakini nina jambo moja dogo tu. Jamhuri katika tafakari yake hiyo itafakari kama bado kuna sababu ya kuendelea na kesi hii,” alisema Lissu.
Oktoba 24, 2025, Wakili Mkude aliieleza Mahakama kuwa mashahidi wao waliokuwa wanafuata wana uhusiano na vielelezo vilivyokataliwa na kwamba, kutokana na kuvikataa, hawatawatumia tena mashahidi hao.
Alisema kwa sababu hiyo, hawakuwa na shahidi na ndio ilikuwa siku ya mwisho ya kikao cha usikilizwaji kesi hiyo.
Hata hivyo, aliiomba Mahakama iahirishwe kesi hiyo mpaka Novemba 3, 2025.
Lissu alipinga ombi hilo, akidai sababu iliyotolewa si ya msingi, na kwa kuwa kesi hiyo inategemea vielelezo vilivyokataliwa basi hapakuwa na ushahidi mwingine wa kuthibitisha shitaka dhidi yake.
“Kwa hiyo rai yangu ombi la kuahirishwa likataliwe, Jamhuri walete shahidi tuendelee kama ikikubaliwa nipewe dhamana ili nisiendelee kukaa gerezani, mimi siwezi kukimbia kwa sabu sina makosa,” alisisitiza Lissu.
Hoja za Lissu zilipingwa vikali na Wakili Mkude pamoja na Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga kwa hoja na rejea za vifungu vya sheria.
Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote, ilikubaliana na hoja na maombi ya Jamhuri ikaahirisha kesi hiyo hadi Novemba 3, 2025 ndipo ikapangwa kuendelea leo Jumatatu.