KMC jana ilipokea kipigo cha tano mfululizo katika Ligi Kuu Bara baada ya kufumuliwa na Yanga mabao 4-1, huku klabu ikiwa mkiani mwa msimamo na mmoja ya nyota wa timu hiyo, Daruwesh Saliboko amekiri vipigo hivyo vinawaumiza na wanajipanga upya.
Kikosi hicho cha kocha Marcio Maximo ndio timu iliyofunga mabao machache (mawili) na kufungwa 10 ikiwa ndio iliyoruhusu mengi zaidi kitu ambacho Saliboko aliliambia Mwanaspoti, wanajipanga upya ili kupambana kuondoka katika unyonge huo kupitia mapumziko ya muda mfupi wa Ligi Kuu.
Saliboko aliyefunga mabao mawili ambayo ndio pekee ya timu hiyo katika msimu huu hadi sasa, akianza walipoizamisha Dodoma Jiji kisha jana alipoisawazishia KMC dhidi ya Yanga kabla ya kuzamishwa kwa mabao 4-1, amesema kama wachezaji wanaumizwa na vipigo hivyo.
“Tumeanza msimu vibaya kwa mchezaji unapofungwa mechi mfululizo kuna namna morali inashuka, lakini hatuna budi kuendelea kupambana tuwezavyo ili turejee katika mstari wa ushindani,” amesema Saliboko na kuongeza;
“Ninachokitamani angalau tufunge mechi tatu mfululizo naamini hilo litatufanya kuongezeka kujiamini na kuondoka katika hatari ya kushuka daraja.”
Mbali na Saliboko mchezaji mwingine aliyezungumzia hilo ni kiungo wa wa timu hiyo Ahmed Bakari ‘Pipino’ amesema: “Tumeanza Ligi Kuu kwa kupoteza mechi mfululizo, lakini bado tunayo nafasi ya kujiondoa katika hatari ya kufanya vibaya zaidi. Msimu ni mgumu timu zilijiandaa vizuri, hivyo tunahamasishana kama wachezaji kuona tunarejesha morali ya kuhakikisha tunashinda mechi zinazofuata.”
KMC iliyowahi kuiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika, ilipanda Ligi Kuu 2018 na msimu uliopita ilimaliza katika nafasi ya 10 ikivuna pointi 35 kupitia mechi 30 ikishinda tisa, sare nane na kupoteza 13, ikifunga mabao 26 na kufungwa 43 ikiwa ya sita iliyoruhusu mabao mengi baada ya KenGold (62), Fountain Gate (58), Dodoma Jiji (49), TZ Prisons (46) na Tabora Utd (45).