IGP, wenzake wamwekea pingamizi Heche, kesi yaahirishwa

Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na wenzake wengine watano, ambao ni wajibu maombi katika shauri la maombi ya kushikiliwa kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tanzania Bara, John Heche, wamemwekea pingamizi mwanasiasa huyo.

Shauri hilo la maombi lilifunguliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na mawakili wa Chadema kwa niaba ya Heche, wakiomba amri ya Mahakama kuwataka wajibu maombi kumfikisha mahakamani kiongozi huyo au kumwachilia huru kwa dhamana.

Katika shauri hilo, mwombaji ni Heche mwenyewe, wajibu maombi ni IGP, ambaye ndiye mjibu maombi wa kwanza, na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu (Dar es Salaam – ZCO).

Wajibu maombi wengine ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni (RCO), Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Shauri hilo lilipangwa kusikilizwa na Jaji Obadia Bwegoge leo, Jumatatu Novemba 10, 2025, hata hivyo limekwama baada ya wajibu maombi kuwasilisha pingamizi la awali.

Taarifa za pingamizi hilo zimetolewa leo na kiongozi wa jopo la mawakili wa wajibu maombi, Wakili wa Serikali Mkuu, Agatha Pima.

“Mheshimiwa Jaji, shauri hili lilipangwa leo kwa ajili ya usikilizwaji, lakini kabla ya kuendelea tumeleta mapingamizi kuhusiana na shauri hili na tuko tayari kuendelea,” amesema Wakili Pima.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa Heche kwa leo, Seleman Mataukwa, amekiri kupokea kiapo kinzani taarifa hiyo ya pingamizi la awali kutoka kwa wajibu maombi.

“Kwa sababu kuna pingamizi la awali na tumepewa muda mfupi, hatujapata nafasi ya kufanya utafiti kujua namna ya kuuyajibu, kwa hiyo tunaomba ahirisho ili tupate nafasi ya kuyapitia, na ikiipendeza mahakama yako tupewe ahirisho la siku mpaka tarehe 13 Novemba kwa ajili ya usikilizwaji wa pingamizi na maombi ya msingi kama mahakama yako itaelekeza hivyo,” amesema Wakili Mataukwa.

Wakili alipoulizwa na Jaji Bwegoge kama wana lolote, amesema hawana pingamizi kama watapewa muda wa kuyapitia na kujiandaa kwa ajili ya usikilizwaji; “sisi tuko tayari kwa maombi hayo,” amesema Wakili Pima.

Jaji Bwegoge amekubaliana na maombi hayo ya wajibu maombi na kuwapa siku tatu walizoomba kujiandaa na pingamizi hilo.

“Shauri hili limeletwa na waombaji, na kwa sababu wao wenyewe ndio wameomba ahirisho mpaka tarehe 13, mahakama inaridhia maombi hayo, hivyo shauri linaahirishwa mpaka tarehe hiyo, litaendelea Novemba 13, 2025,” amesema.

Jaji Bwegoge ameelekeza shauri hilo liendelee tarehe hiyo saa 4:30 kwa ajili ya usikilizwaji wa pingamizi hilo pamoja na shauri la msingi.

Wakili Pima na Wakili Serikali Mwandamizi, Deborah Mushi, pamoja na Wakili Mataukwa, kwa nyakati tofauti, wameliambia Mwananchi kwamba katika pingamizi hilo wajibu maombi wamebainisha sababu moja, kiapo kinachounga mkono maombi kina kasoro za kisheria.

Heche anashikiliwa na Polisi tangu Oktoba 22, 2025, alipokamatwa nje ya geti la Mahakama Kuu Dar es Salaam, alipokuwa akienda mahakamani, japo kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini.

Baada ya kukamatwa, awali chama hicho kilitoa taarifa kwa umma kuwa Jeshi la Polisi Dar es Salaam liliwaeleza kuwa mwanasiasa huyo atasafirishwa kupelekwa Tarime, Mkoa wa Mara, lakini familia na ndugu zake walipomtafuta katika vituo vya Polisi Tarime na Musoma, hawakumpata.

Hata hivyo, baadaye ilifahamika alipelekewa Dodoma, ambako alikuwa akishikiliwa katika kituo cha Polisi Mtumba, bila kumpatia dhamana wala kumfikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria za nchi.

Katika taarifa iliyotolewa na Wakili Hekima Mwasipu Novemba 4, 2025, Heche alisafirishwa tena siku hiyo kurejeshwa Dar es Salaam, na alifikishwa katika kituo cha Polisi Mburahati, Mkoa wa Kinondoni, na kuhojiwa kwa tuhuma za vitendo vya ugaidi.

“Amepewa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kigaidi kutoka Kimara mpaka Magomeni, na kujihusisha na vitendo vya kigaidi maeneo ya Msewe na External,” alisema Wakili Mwasipu katika taarifa yake.

Hata hivyo, Wakili Mwasipu alisema baada ya kutakiwa kuandika maelezo ya onyo, Heche alitumia haki yake ya kisheria ya kukataa kuandika maelezo, na kwamba atatumia haki hiyo baada ya kupelekwa mahakamani.