ALIYEKUWA mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Abdulkarim Segeja, ameachana rasmi na kikosi hicho cha maafande, baada ya kugoma kuongeza mkataba mwingine, huku taarifa zikieleza kuna ofa mbalimbali ambazo menejimenti yake inazifanyia kazi.
Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari 2023, akitokea Copco ya jijini Mwanza, alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea timu hiyo ya maafande, huku mazungumzo ya yeye kuongeza mwingine yakigonga mwamba.
Akizungumza na Mwanaspoti, Segeja amesema ni kweli amefikia uamuzi wa kusitisha mkataba na timu hiyo ya jijini Mbeya, licha ya uongozi wa kikosi hicho kumuwekea mkataba mpya wa kuendelea kuichezea, japo ameona ni muda wa changamoto mpya.
“Kuna mambo ambayo awali hayakwenda vizuri na baada ya kukaa na menejimenti yangu tukaona tuvunje mkataba uliobakia kwa lengo la kuangalia changamoto sehemu mpya, hivyo, ni kweli nimeondoka kwa makubaliano ya pande mbili,” amesema Segeja.
Aidha, mchezaji huyo amesema licha ya kukaa nje ya uwanja kwa muda bila ya kucheza mechi za ushindani, ataendelea kufanya mazoezi kwa nguvu kwa lengo la kujiweka fiti, huku menejimenti yake ikifanyia kazi ofa mbalimbali zilizopo mezani mwao.
Wakati mshambuliaji huyo akizungumza hayo, taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza kuna baadhi ya timu kutoka ndani na za nje zinazomuhitaji, licha ya menejimenti yake kwa sasa kutotaka kuweka wazi kwa sababu bado hazijakamilika.
Nyota huyo wakati anajiunga na Prisons alitokea Copco ya jijini Mwanza iliyokuwa inashiriki Ligi ya Championship, ambapo kwa msimu wa 2023-2024, aliifungia mabao manane, huku akicheza timu mbalimbali ikiwamo TRA United zamani Tabora United.